MNYETI AAGIZA MANYARA IKAMILISHE VIWANDA 100
Mkuu
wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na watumishi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, wakiwemo maofisa tarafa, madiwani,
watendaji wa kata, vijiji, walimu na wenyeviti wa vijiji, juu ya kufanya
kazi kwa uadilifu na kutumikia jamii, kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo
mhandisi Raymond Mushi.
Mkuu
wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Mhandisi Raymond Mushi akizungumza
na wananchi wa Kata ya Madunga juu ya kufanya kazi na kuwahusia kuwa
siku mbili ambazo mtu hawezi kufanya chochote ni jana na kesho hivyo
waitumie siku ya leo kwa kutimiza wajibu wao, kulia ni Mkuu wa Mkoa huo
Alexander Mnyeti na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Nicodemus
Tarmo.
Mbunge
wa Jimbo la Babati Vijijini Mkoani Manyara, Vrajilal Jituson,
akizungumza na wananchi wa Kata ya Madunga ambao wanachangia kwa kiasi
kikubwa maendeleo yao ikiwemo suala la elimu.
Mbunge
wa viti maalum wa mkoa wa Manyara, Esta Mahawe akizungumza na wananchi
wa Kata ya Madunga ambapo alijitoa mashuka 10 kwa ajili ya wagonjwa
watakaotumia kwenye zahanati ya kijiji hicho iliyozinduliwa na Mkuu wa
mkoa huo Alexander Mnyeti.
Mkuu
wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti ameziagiza Halmashauri za Wilaya za
Mkoa huo kuhakikisha zinatekeleza agizo la uanzishwaji wa viwanda 100
na hadi mwezi Septemba mwaka huu viwe vimekamilika.
Mnyeti
akizungumza na watumishi na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Babati, alisema kila halmashauri ya mkoa huo wenye halmashauri saba,
inapaswa iwe na viwanda 15. Mnyeti
alisema serikali ilitoa agizo la kila mkoa uanzishe viwanda 100 hivyo
na mkoa wa Manyara nao unapaswa kuhakikisha unatekeleza agizo hilo kwa
kila halmashauri kuwa na viwanda 15.
Alisema
agizo hilo linatakiwa kutekelezwa kwa kila sekta ikiwemo kilimo na
mifugo ambazo ndizo shughuli kuu za kiuchumi kwa wananchi wengi wa mkoa
huo. “Watumishi
wa umma wanapaswa kutambua kila taaluma waliyoisomea wanapaswa kuwekeza
kwenye fikra ya viwanda kwa kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa sekta
hiyo,” alisema Mnyeti.
Aliwapongeza
mkuu wa wilaya hiyo mhandisi Raymond Mushi na mkurugenzi mtendaji wa
halmashauri hiyo Hamis Malinga kwa kutekeleza agizo hilo la uanzishwaji
wa viwanda vipya. “Kwenye
miezi mitatu iliyopita Halmashauri ya Babati mlikuwa mmeshafanikisha
uanzishwaji wa viwanda nane na hadi kufikia mwezi Septemba mtakuwa
mmekamilisha viwanda 15 hongereni sana,” alisema Mnyeti.
Mkuu
wa wilaya ya Babati, mhandisi Raymond Mushi alisema wananchi wa eneo
hilo ni wachapakazi wazuri na hujishughulisha na shughuli mbalimbali
ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, ujasiriamali na nyinginezo.
Mushi
alisema kwa kiasi kikubwa wananchi wa wilaya yake ni wachapakazi huku
wakishirikiana na serikali katika kufanikisha maendeleo mbalimbali.Mbunge
wa Jimbo la Babati Vijijini, Vrajilal Jitu Son alisema wameshajipanga
kutekeleza hilo kupitia viwanda mbalimbali vilivyopo jimboni humo.
Mkurugenzi
Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Babati, Hamis Malinga alisema kwa
kiasi kikubwa wamefanikisha utekelezaji wa vipaumbele mbalimbali ikiwemo
elimu, afya na maji.“Kwenye
suala la migogoro ya ardhi, kamati ya ulinzi na usalama chini ya
Mwenyekiti wake mheshimiwa mkuu wa wilaya kwa kiasi kikubwa imefanikisha
kusuluhisha japo kuwa maeneo machache yaliyobaki na yanaendelea
kufanyiwa kazi,” alisema.
Jituson
alisema kwenye eneo hilo kuna viwanda mbalimbali vipya vilivyojengwa
vikiwemo vya mafuta, sukari, kukoboa mpunga, unga, na kiwanda cha
vyakula vya mifugo. Alisema
kupitia nafasi ya vijiji vingine 30 kupatiwa umeme wa Rea awamu ya
tatu, itasaidia kuanzisha viwanda vidogo na vya kati kwa wajasiriamali
mbalimbali waliopo kwenye jimbo hilo.
Mkazi
wa Kijiji cha Endanachang’ John Lorry alisema serikali na sekta binafsi
zinapaswa kujipanga na kuanzisha kiwanda cha biskuti ili zao la mbaazi
lipate soko. Lorry
alisema changamoto ya soko la mbaazi imekuwa kero kwa jamii ila kupitia
viwanda wakulima wengi wa eneo hilo wataweza kunufaika kwa kupata
sehemu ya uhakika ya kuuza zao hilo.
No comments:
Post a Comment