Wataalamu wa kilimo kwa kushirikiana
na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani ( FAO) wamewajengea uwezo wakulima wa
wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara juu ya namna ya kupambana na viwavijeshi vamizi
vinavyoshambulia zao la mahindi.
Sehemu mbalimbali za mkoa wa Manyara
wakulima wengi wanalalamikia mazao yao ya mahindi yaliyopo mashambani hivi
yameshambuliwa na wadudu hao.
Wataalamu hao waliwasilisha mada tatu
juzi wilayani Kiteto ambazo ni utambuzi,
uchunguzi, ufuatiliaji na udhibiti wa wadudu hao viwavijeshi vamizi.
Akiwasilisha mada ya kwanza ambayo ni
utambuzi , Ofisa kilimo Sergea Mutahiwa
alielezea namna ya kumtambua kiwavijeshi vamizi, mzunguko wa maisha
yake, tabia zake na muonekano wake.
Pia ameeleza kuhusu hali ya viwavi
jeshi nchini, ushirikishwaji wadau, usambazaji wa machapisho, ushiriki wa
vyombo vya habari na mtazamo wa jamii kuhusu viwavijeshi vamizi .
Alisema mtazamo wa jamii na uelewa
mdogo ni tatizo juu ya uelewa kwa viuatilifu vinavyopendekezwa na jinsi ya
kutumia dawa za kuangamiza wadudu hao hatari kwa kushambulia mazao.
Alisema wakulima wameendelea kutumia viatilifu vingi vya aina mbalimbali na katika maeneo mengine wakulima hutumia
dozi kubwa kutokana na mashambulizi kujirudia .
Mutahiwa alisisitiza kuwa matumizi
yasiyo sahihi ya viatilifu yanaweza kusababisha kuua wadudu wasiolengwa na
kudhuru afya za binadamu, vilevile kusababisha usugu kwa visumbufu vya mimea.
Alisema viatilifu vinavyoshauriwa
na Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu
(TPRI) na serikali kupitia wizara ya kilimo inatarajia kuzichukua ili kudhibiti kisumbufu hicho.
Ofisa kilimo Grace David alitoa mada
ya ukaguzi na ufuatiliaji kwa kufuatilia ukuaji wa mimea shambani, kwamba mimea
inatakiwa kufuatiliwa katika ukuaji wake.
Alielekeza namna ya kufanya ukaguzi
kuwa ufanyike zigizaga, usifuate mstari
ili kuwakilisha shamba zima na
usichukue zaidi ya dakika 15.
Alisema ukaguzi ni muhimu ili
kubaini uwepo na kiasi cha viwavijeshi
vamizi, na kufanya tathmini ya madhara ili kuweza kujua njia sahihi ya kufanya
udhibiti.
Pia, aliwaelezea wakulima hao namna
ya kutumia mtego maalum wenye harufu kwa ajili ya kukamata viwavijeshi vamizi.
Ayubu
Nchimbi akitoa mada ya tatu ya udhibiti viwavijeshi vamizi alisema
udhibiti wa kiwavijeshi vamizi unaanza na utambuzi.
Nchimbi alisema lazima kumtambua
kisumbufu, mzunguko wa maisha yake, dalili za mashambulizi na kiasi gani
mashambulizi yamefanyika.
Alisema dalili za mashambulizi ndizo zitakazomuongoza
mkulima kujua kiasi cha mashambulizi na
njia atakazotumia ili kudhibiti kisumbufu.
Alisema udhibiti sahihi wa
viwavijeshi vamizi katika ukuaji wa
mimea ya mahindi unategemea na muda wa utambuzi wa mashambulizi ya mdudu
kupitia ufuatiliaji na ukaguzi wa mimea shambani.
No comments:
Post a Comment