Wednesday 14 January 2015

TUNAZINDUA MADARASA


Mkurugenzi wa Graceland Hotel Ltd na Kamanda Mteule wa UVCCM Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Daniel Ole Materi na Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka, wakizindua madarasa mawili ya shule ya msingi Loorng'oswani iliyopo Terrat aliyojengwa kwa gharama ya sh50 milioni.

Tuesday 13 January 2015

NAKABIDHI MADARASA


Mkurugenzi wa Graceland Hotel Ltd na Kamanda Mteule wa UCCM Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Daniel Ole Materi, akizungumza jana wakati alipokabidhi madarasa mawili ya shule ya msingi iliyopo Terrat aliyojengwa kwa gharama ya sh50 milioni pembeni yake ni Mbunge wa Jimbo hilo, Christopher Ole Sendeka.

Monday 5 January 2015

UBATIZO WA WATOTO WA SHUJAA BARUTI NA BRYAN JULIUS



Sherehe ya ubatizo wa watoto wa Shujaa Baruti na Bryan Julius



Baadhi ya ndugu jamaa na marafiki waliohudhuria sherehe ya ubatizo wa watoto wa Shujaa Baruti na Bryan Julius.



Shujaa Baruti (kulia) na Bryan Julius (kushoto) wakiwa kwenye sherehe ya ubatizo wa watoto wao.

HOFU YATANDA VIJIJI VINAVYOZUNGUKA HIFADHI YA TAIFA TARANGIRE






Hofu imetanda kwenye Vijiji vya Kibaoni na Olasiti Wilayani Babati Mkoani Manyara na Mswakini Wilayani Monduli Mkoani Arusha, baada ya simba wawili wa hifadhi ya Tarangire kudaiwa kuonekana wakizunguka vijiji hivyo.

Hali hii imejitokeza baada ya wiki iliyopita simba sita kuuawa na wananchi wa vijiji vya Kibaoni na Olasiti kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kuonyesha ufahari wa ujana, huku wafugaji watano wakijeruhiwa na simba katika tukio hilo.

Kutokana na hali hiyo jana na juzi wana vijiji wa maeneo hayo walionekana wakitembea kwa makundi huku wakiwa na silaha za jadi ikiwemo fimbo, sime na mikuki, kwa lengo la kujilinda pindi wakikutana na simba hao.

Hata hivyo, wakizungumza na waandishi wa habari jana wakazi hao walidai kuwa Serikali imekuwa ikitumia nguvu kubwa pindi wanyamapori wanapouawa na kutochukua hatua yoyote pale wanyamapori wanapozuru binadamu.  

Walisema wanyamapori wanapoua binadamu, mifugo au kuharibu mazao, hakutolewi tamko lolote, ila baada ya wanyamapori kuuawa Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu amekuwa akitoa matamshi ya kuwatisha wafugaji.

Mkazi wa Olasiti Saning’o Ole Nigi alisema jamii inayozunguka wanyamapori wanaishi kwa hofu, ila wao ndiyo walinzi wa wanyamapori kwa miaka yote kwani hakujawahi kutokea tukio la ujangili lililofanywa na wafugaji.

“Wanyamapori wamekuwa tishio sana kwa wananchi na sisi ndiyo walinzi wakuu wa wanyamapori wa Tarangire kwani wanatuzunguka kila wakati ila Waziri awe anachunguza kwanza jambo kabla ya kutoa kauli,” alisema Ole Nigi.

Naye, Kaimu Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, Mrakibu Mwandamizi (SSP) Christopher Fuime, alithibitisha wafugaji watano kulazwa kwenye hospitali ya wilaya ya Monduli wakidaiwa kujeruhiwa na simba wiki iliyopita.

Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Jackson Saipei (30), Obeid Mollel (23), Jackson Mediteki (23), Karani Saimon (30) na Leseilama Tobiko (28) wote wakazi wa kijiji cha Olasiti ambao wanadaiwa kutoroka hospitali wakihofia kukamatwa kwa kuua Simba hao.

Simba sita waliotoka nje ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na kuingia eneo la Kijiji cha Kibaoni wilayani Babati mkoani Manyara, wameuawa kwa kuchomwa mikuki na wananchi.



Kijiji cha Kibaoni kipo hatua chache kutoka Hifadhi ya Tarangire ambayo ni mojawapo ya vivutio vya kitalii na mara nyingi wanyamapori huzagaa kijijini hapo, hasa nyakati za masika kuepuka majani marefu hifadhini.

Tukio hilo linaloelezewa kuwa ni janga kubwa kwa sekta ya uhifadhi na utalii nchini, lilitokea jana alfajiri na hadi Saa 6.00 mchana na mizoga saba ya Simba ilipatikana, huku mmoja akiaminika kufia kwenye vichaka baada ya kukimbia alipojeruhiwa.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu ameziagiza mamlaka zinazohusika kuwasaka na kuwatia mbaroni wote waliowahamasisha na kuwaongoza wakazi wa kijiji hicho kuwaua Simba hao.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Nyalandu alitoa maagizo kwa polisi kuchunguza uhalali wa bunduki inayomilikiwa na mmoja wa wakazi wa kijiji hicho iliyotumika kuwaua Simba wawili kati ya saba.

“Kuua idadi kubwa ya Simba kwa wakati mmoja, tena katika siku ya kwanza ya Mwaka Mpya ni jambo la kusikitisha na linastahili kulaaniwa na wote wenye mapenzi mema na uhifadhi ndani na nje ya nchi,” alisema Nyalandu na kuongeza:

“Hatuwakamati wakazi wote 100 walioshiriki kuwaua simba hawa, bali tutashughulika na wale waliochochea mauaji ili kutoa fundisho kwa wale wanaochukua sheria mkononi kwa kuwaua wanyamapori,” alisema Nyalandu.

Hifadhi ya Taifa ya Tarangire inakadiriwa kuwa na Simba kati ya 200 hadi 250 na Tembo wanaokadiriwa kufikia 3,000 na wanyama wengineo zaidi ya 10,000.

Mmoja wa wanakijiji aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina gazetini kwa sababu za kiusalama, alisema Simba hao waliuawa baada ya kudaiwa kumla punda kihongwe kwenye moja wa maboma ya wakazi wa kijiji hicho ambao ni jamii ya wafugaji wa Kimasai.

“Usiku kundi la Simba zaidi ya 12 walionekana wakizunguka katika maeneo ya karibu na kambi ya Watalii ya Zion Campsite. Ilipofika alfajiri, watu wakaanza kupiga mayowe kuashiria hatari baada ya Simba hao kusambaa kijijini,” alisema na kuongeza;

“Kelele hizo ziliwashtua Simba na kuwafanya waanze kuunguruma, hali iliyozua taharuki na vijana (Morani), wakaanza kupambana nao na kuwaua mmoja baada ya mwingine hadi kufikia Simba saba na mmoja alikimbia akiwa na mkuki mwilini.”

Alisema vijana wawili walijeruhiwa vibaya baada ya Simba mmoja kuwashambulia.
Meneja Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Paschal Shelutete alisema mara nyingi mauaji ya wanyamapori wakali wakiwamo simba, chui, chita huambatana na kisasi cha wafugaji baada ya mifugo yao kujeruhiwa au kuliwa.

“Katika tukio hili, Simba hawakuvamia mifugo wala maboma ya wafugaji.
“Hawa walionekana tu kijijini. hawakuwa na madhara, wamewaua kwa makusudi,” alisema Shelutete.

Alisema hata kama kungekuwepo uvamizi, askari wa TANAPA wangefika eneo hilo ndani dakika zisizozidi tano iwapo wangetaarifiwa kwa sababu eneo hilo liko hatua chache kutoka makao makuu ya hifadhi ya Tarangire.

Mkuu wa mkoa wa Manyara, Joel Bendera, aliyeripoti kituo chake hicho kipya cha kazi wiki iliyopita alitembelea eneo la tukio jana asubuhi na kushuhudia mizoga ya Simba hao ambayo baadaye yalihamishiwa makao makuu ya hifadhi ya Tarangire.

Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas licha ya kukiri kupata taarifa za tukio hilo, alisema linapaswa kuzungumziwa ni Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara, Mrakibu Mwandamizi Christopher Fuime. Eneo la tukio liko mpakani mwa mikoa ya Arusha na Manyara.

Akizungumza kwa njia ya simu jana mchana, Kamanda Fuime alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kulizungumzia tukio hilo baada ya kukamilisha ukusanyaji wa taarifa zote muhimu kutoka eneo la tukio.

Siri ya kuuawa simba  sita waliotoka kwenye Hifadhi ya Taifa ya Tarangire inayopatikana kwenye mikoa ya Manyara na Arusha imebainika na kama ilivyoelezwa awali kwamba mauaji hayo yalifanywa na wananchi wa vijiji vya Olasiti na Kibaoni wilayani Babati,  Mkoa wa Manyara.

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Tarangire, Stephano Qolli alisema kuwa kutokana na uchunguzi wao wakazi wa vijiji hivyo hawana tabia ya kufanya ujangili dhidi ya wanyamapori bali kitendo walichokifanya kililenga  kuonyesha ufahari wa kutambulika na jamii kwa kuua simba.

“Haya maeneo kuna ujangili ambao mara nyingi unafanywa na wananchi kutoka nje ya eneo hilo, lenye jamii za Wamasai na Wamang’ati ambao kijana akimuua simba anapata heshima kwa jamii inayomzunguka, anaonekana ni jasiri anayeweza kulinda jamii yake dhidi ya hatari zote,” alisema Qolli.

Alisema kitendo walichokifanya hakikubaliki kwani kilionyesha nia yao ilikua kuwaua simba hao na siyo kuwafukuza waondoke kwenye kijiji hicho, baada ya kuwazingira na kuwashambulia kwa silaha za jadi hadi kufa simba wanne huku wawili wakiuawa kwa risasi.

Mizoga ya simba hao ilionekana ikiwa imekatwa mikia na miguu baada ya kuwaua jambo ambalo linatafsiriwa linalenga kuweka kumbukumbu ya ushujaa kwa jamii hiyo. Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akizungumza na waandishi wa habari Januari Mosi, mwaka huu jijini Arusha, alisikitishwa na mauaji hayo ambayo alidai yameitia doa sekta ya utalii siku ya Mwaka Mpya.