Mji mdogo wa Haydom wa Wilayani Mbulu Mkoani
Manyara na viunga vyake kwa muda wa wiki hii nzima utakumbwa na burudani kubwa
kupitia tamasha la ujasiriamali na michuano ya Kurugenzi Cup '18 iliyoandaliwa
na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Hudson Kamoga.
Pamoja na mada za ujasiriamali kutolewa pia
michuano ya soka itakayoshirikisha timu 10 itatimua vumbi kwenye viwanja vya
Haydom.
Kamoga alisema anatarajia vijana watajinyanyua
kiuchumi kwa kufanya kazi kupitia kauli mbiu ya tamasha hilo isemayo wakati wa
kuwa mzalendo na kujenga nchi yetu, uvivu ni sumu ya maendeleo.
Alisema kwa muda wa wiki moja itakayofanyika
tamasha hilo kutakuwa na mada mbalimbali za ujasiriamali zitakazotolewa na
magwiji mbalimbali waliobobea kwenye uchumi.
"Wilaya ya Mbulu ina fursa nyingi na
vichocheo vya kiuchumi hivyo tutawatumia watu maarufu akiwemo mchambuzi wa soka
Shafi Dauda ambaye atakuja hapa Haydom," alisema Kamoga.
Alisema wanatarajia kuibua vipaji vipya
tofauti kwenye soka na riadha ili vijana wafuate nyayo za mwanariadha maarufu
wa zamani John Stephen aliyeacha historia kwenye michuano ya dunia.
Katibu wa chama cha soka cha wilaya ya Mbulu
(MDSA) Joseph Nicodemus alitaja timu zitakazoshiriki michuano hiyo ni Dongobesh
FC, Young Boys, Airport SC, Qadesh SC, Mlimani City Lambo FC, Stand United,
Makurusa SC, Rema 1,000 na Kidarafa FC ya wilaya jirani ya Mkalama Mkoani
Singida.
Nicodemus alisema michuano hiyo itakayofanyika
kwa muda wa wiki moja itatumia mtindo wa mtoano na siyo ligi, hivyo timu
ikifungwa inatolewa mashindanoni.
Kwenye ufunguzi wa michuano hiyo, timu ya
Dongobesh FC iliifunga timu ya Kidarafa FC ya wilayani Mkalama mkoani Singida
mabao 2-1.
No comments:
Post a Comment