Wednesday 21 March 2018

KOMBA APIGA VITA VIJANA MANYARA KUANDAMANA KUPITIA MITANDAO YA KIJAMII


Mwenyekiti wa UVCCM kata ya Balang'dalalu Emmanuel Gamasa alisema vijana wa mkoa wa Manyara ni watu makini wenye kujitambua hivyo hawatakubali kuambiwa jambo lisilo na umuhimu na kutekeleza. Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Manyara, Mosses Komba (kushoto) akiongoza kula kiapo kwa vijana 20 wa Kata ya Balang'dalalu Wilayani Hanang' waliojitoa Chadema na kujiunga na CCM.

Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Manyara, Mosses Komba akikemea suala la vijana kufuata mkumbo na kutaka kuandamana kwa kupitia mitandao ya kijamii, kulia ni Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Balang'dalalu Wilayani Hanang' Emmanuel Gamasa.

KOMBA APIGA VITA VIJANA MANYARA KUANDAMANA KUPITIA MITANDAO YA KIJAMII



Mwenyekiti wa jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi  (UVCCM) Mkoani Manyara, Mosses Komba amewataka vijana wa mkoa huo kutofuata mkumbo na kushiriki mandamano yasiyo na tija yanayoratibiwa kwenye mitandao ya kijamii.

Komba akizungumza jana na vijana wa kata ya Balang'dalalu wilayani Hanang' alisema kuandamana kwa kufuata mkumbo ni kukosa dira na mwelekeo.

Alisema ana imani hakuna kijana wa mkoa huo atakayeandamana bila mwelekeo kwa kufuata mkumbo ili hali hatambui anaandamana kwa kuunga mkono jambo gani la maana.

"Vijana tunapaswa kuwa makini yaani mtu yupo Marekani au Dar es salaam, amekaa kwenye kiyoyozi halafu anakwambia wewe wa Manyara andamana, mwambie shindwa pepo," alisema Komba.

Alisema huu ni muda wa vijana kufanya kazi kwa bidii katika kuhakikisha wanajipatia mahitaji yao kuliko kuwaza mambo ya maandamano yasiyo na tija.

"Unaandamana kwa kuiunga mkono serikali ya CCM inayoongozwa na Rais John Magufuli, unaunga mkono maendeleo yanayofanywa hapa nchini au unaandamana bila sababu kwa kuambiwa tuu andamana?" alihoji Komba.

Mwenyekiti wa UVCCM kata ya Balang'dalalu Emmanuel Gamasa alisema vijana wa mkoa wa Manyara ni watu makini wenye kujitambua hivyo hawatakubali kuambiwa jambo lisilo na umuhimu na kutekeleza.

"Nikuhakikishie Mwenyekiti jambo hilo halitafanyika kwani vijana wa Manyara wapo kimaendeleo zaidi hawakurupuki kwa mambo ambayo hayawahusu na hayana maslahi kwao," alisema Gamasa.

Alisema vijana wa kata ya Balang'dalalu wamejipanga kuhakikisha wanaendelea kuimarisha na kuijenga jumuiya yao ipasavyo kwani wao ndiyo jeuri ya chama.

"Pamoja na hayo ofisi ya UVCCM kata ya Balangdalalu ina changamoto ya ukosefu wa kompyuta na pia vijana wanaomba wapate mashine ya kufyatulia matofali," alisema.

MWISHO.