Monday 26 February 2018

WANANCHI 300 WA KITONGOJI CHA KINACHERE,HANANG WAANZA UJENZI WA KISIMA NA TENKI LA KUHIFADHIA MAJI YA MVUA

WANANCHI  300 wa Kitongoji cha Kinachere,kata ya Sirop,tarafa ya Simbay,wilayani Hanang,Mkoani Manyara kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Hanang wameanza ujenzi wa kisima na tanki la kuhifadhia maji ya mvua ili waweze kuondokana na adha ya kufuata huduma hiyo  umbali wa zaidi ya mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji hicho,Peter Qwendo alisema mradi huo utakapokamilika unatarajia kugharimu zaidi ya shilingi milioni 49 na kwamba kati ya kiasi hicho cha fedha nguvu za wananchi ni asilimia kumi ya gharama za mradi huo kwa kufanyakazi ya kukusanya mawe,mchanga,kokoto,kuchota maji na kumwagilia.
Aidha Qwendo ambaye pia ni mmoja wa watu waliokwenda nchini Kenya kupata mafunzo juu ya usimamizi wa shughuli hiyo,alisema wananchi hao wanaoishi katika kaya 107 wamekuwa wakiifuata huduma hiyo katika Kitongoji cha Ghata kilichopo umbali wa takribani kilomita 14 kwenda na kurudi.
Kwa upande wake Msimamizi wa Mpango wa afya wa Kijiji cha Nangwa,Apolei Wilbrod aliweka bayana kwamba wafadhili wa mradi huo ni Medical Missionary Of Mary Nangwa wanaoendesha huduma za kliniki ya mama na mtoto katika wilaya ya Hanang. 
Kwa mujibu wa Wilbrod mradi huo ulioanza tangu mwaka 2014 kwa miradi ya aina nne,kabla ya kuanza kwa mradi huo wa tano na madhumuni yake yalikuwa kuwasaidia wananchi waliopo kwenye maeneo hayo na kwamba unaotarajiwa kukamilika katika kipindi cha mwezi mmoja na utagharimu jumla ya shilingi milioni 49,700,000/=.
Hata hivyo Msimamizi huyo wa mradi alitumia pia wasaa huo kutoa wito kwa wadau wengine kujenga utamaduni wa kushirikiana wakati wote na jamii kwa kufurahia miradi husika ili iweze kuwasaidia wananchi.
Mbunge wa jimbo la Hanang,Dk.Mary Nagu aliyetembelea mradi huo kwenye ziara yake inayoendelea katika jimbo hilo alibainisha kuwa utaratibu mzuri waliojiwekea ni kwamba wananchi wanalazimika kuchangia asilimia kumi na Halmashauri asilimia kumi.
Hata hivyo mbunge huyo aliunga mkono wananchi hao kwa kuwaahidi kuwapatia malori matano ya mchanga na atawasiliana na Halmashauri ili kufahamu imechangia kitu gani katika mradi huo.
“Mradi umechelewa hela zimekuja zikakaa sasa basi tuonyeshe kwamba na sisi tunataka maji kwani maji ni uhai,hamtaki maji,mmenionyesha mnataka kwa sababu mmejitolea na kazi inaenda kwa kasi sana.”alisisitiza Mbunge huyo wa Jimbo la Hanang.
Ramadhani Hamisi ni fundi wa kujenga kisima na tenki la maji katika mradi huo anaweka bayana kwamba tenki hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kujaza lita laki moja za maji na wanatarajia kukamilisha kujenga katika kipindi cha mwezi mmoja.
ananchi wa Kitongoji cha Kinachere,kata ya Sirop,Tarafa ya Simbay wakifanya kazi za mikono kuhakikisha mradi huo unakamilika katika kipindi cha mwezi mmoja na kuanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama.
Mbunge wa Jimbo la Hanang,Dk.Mary Nagu akiungana na wananchi wa Kitongoji cha Kinachere kufanyakazi za kukusanya na kusomba mchanga wa kujengea kisima pamoja na tenki la kuhifadhia maji ya mvua na kuahidi kuchangia lori tano za mchanga.
Mbunge wa Jimbo la Hanang,Mkoani Manyara,Dk.Mary Nagu(wa kwanza kutoka kushoto) akikagua ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji ya mvua linalojengwa juu ya mawe.
mafundi wa kujenga kisima wakiendelea na kazi ya kusuka nondo za kisima kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wake katika kipindi cha mwezi mmoja.(Picha zote Na Jumbe Ismailly)
 Mbunge wa Jimbo la Hanang,Mkoani Manyara,Dk.Mary Nagu(wa kwanza kutoka kushoto) akipata maelezo mafupi ya mradi wa ujenzi wa kisima na tenki la kuhifadhia maji ya mvua kutoka kwa msimamizi wa mradi huo,Apolei Wilbrod.

WATUMISHI WA UMMA MSINYANYASE WACHIMBAJI WADOGO – BITEKO

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (mwenye kipaza sauti) akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu kwenye machimbo ya Kitunda ya Wilayani Sikonge, Mkoani Tabora. Biteko alifanya ziara kwenye machimbo hayo ili kujionea shughuli zinazoendelea sambamba na kuzungumza na wachimbaji.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Peres Magiri wakiwa kwenye mkutano na wachimbaji wadogo wa machimbo ya dhahabu ya Kitunda yaliyopo Wilayani Sikonge, Mkoani Katavi.
Wachimbaji wadogo wa dhahabu kwenye machimbo ya Kitunda wilayani Sikonge wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) alipofika kwenye machimbo hayo ili kujionea shughuli wanazofanya pamona na kujadiliana nao masuala mbalimbali ikiwemo ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali za Serikali.
Baadhi ya Wachimbaji wadogo wa dhahabu kwenye machimbo ya Kitunda wilayani Sikonge wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) alipofika kwenye machimbo hayo ili kujionea shughuli wanazofanya pamona na kujadiliana nao masuala mbalimbali ikiwemo ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali za Serikali.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) akiwasilikiza baadhi ya Wachimbaji wadogo wa dhahabu kwenye machimbo ya Kitunda wilayani Sikonge wakiuliza maswali na kuelezea changamoto mbalimbali ziazowakabili kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (mwenye kipaza sauti) akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu kwenye machimbo ya Kitunda ya Wilayani Sikonge, Mkoani Tabora. Biteko alifanya ziara kwenye machimbo hayo ili kujionea shughuli zinazoendelea sambamba na kuzungumza na wachimbaji.

……………….

Serikali imesema itawachukulia hatua za kinidhamu watendaji wanaotumia madaraka yao vibaya kwa kuwanyanyasa wachimbaji wadogo wa madini nchini ili kujipatia kipato kinyume na taratibu.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko kwenye mkutano na wachimbaji wadogo wa madini katika machimbo ya Dhahabu ya Kitunda yaliyopo Wilayani Sikonge, Mkoani Tabora.

Wakielezea changamoto zinazowakabili, wachimbaji wa machimbo hayo kwa nyakati tofauti walimueleza Biteko masikitiko yao juu ya unanyasaji wanayofanyiwa na baadhi ya Maafisa wa Serikali wasiowaaminifu wakiwemo Askari Polisi na Maafisa Madini.

Wachimbaji hao walisema kumekuwepo na tabia ya kushinikizwa kutoa rushwa ama kugawana faida kwa vitisho kuwa watazuiwa kuendelea kufanya shughuli zao kwenye maeneo husika.

“Kuna baadhi ya Maafisa Madini na Askari Polisi wamekuwa wakitulazimisha nao tuwape mgawo wa mawe tunayochimba vinginevyo watafukia maduara yetu,” alisema Alfred Kulwa mmoja wa wachimbaji kwenye machimbo hayo.

Kufuatia malalamiko hayo, Naibu Waziri Biteko alitoa onyo kwa watendaji wenye tabia hiyo kuacha mara moja na alimuagiza Afisa Madini kushirikiana na Mkuu wa Polisi wa Wilaya husika kuhakikisha wanafuatilia suala hilo na watakaobainika hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

“OCD, tendeni haki, hawa wawe salama. Askari atakayebainika ananyanyasa mchimbaji madini achukuliwe hatua za kinidhamu haraka bila kuchelewa,” aliagiza Naibu Waziri Biteko.

Biteko alisema Afisa yeyote anayehitaji kujishughulisha na biashara ya madini aache kazi ili ajikite katika biashara hiyo na sio kutumia cheo chake kuwanyanyasa wachimbaji.

Aliongeza kuwa hairuhusiwi Mtumishi wa Umma kutumia cheo kujinufaisha. “Marufuku watendaji wa Serikali ama wamiliki wa leseni za uchimbaji madini kutumia madaraka yao vibaya. Kama unataka ingia uchimbe mwenyewe. Serikali hii ya Awamu ya Tano inatutaka tuondoe manyanyaso,” alisema Biteko.

Biteko alisema mchimbaji atakayenyanyaswa atoe taarifa Polisi na pia amfahamishe kwa njia ya simu kuhusiana na manyanyaso hayo ambapo alitaja namba zake za simu ili kukitokea hali ya sintofahamu wasisite kumfahamisha.

Hata hivyo, Biteko aliwataka wachimbaji hao kuacha kuwasilisha taarifa za uwongo ikiwemo kusingiziana na mara zote wasimamie haki ili kuepusha migogoro baina yao na Serikali.

MAENEO YA KITALII YANAYOPATIKANA KUSINI MWA TANZANIA

Miongoni mwa maeneo ya kitalii ambayo hayapewi kipaumbele au kutokuwa maarufu ni pamoja na Kusini mwa Tanzania. Tofauti na vivutio vya kitalii vya kanda ya Kaskazini kuwa maarufu kama vile Mlima Kilimanjaro, Hifadhi za Serengeti na Ngorongoro, kuna uwezekano mkubwa kwamba Kusini mwa Tanzania kuna hazina kubwa ya vivutio kwa watalii ambavyo havitangazwi au kuvumbuliwa na wengi.
Miongoni mwa sababu ambazo zimekuwa zikikwamisha shughuli za kitalii kwa ukanda wa Kusini ni pamoja na miundominu hafifu kama vile barabara, viwanja vya ndege ambavyo hupelekea maeneo hayo kufikika kwa ugumu pamoja na upungufu wa malazi kama vile hoteli za kisasa na zinazokidhi vigezo.

Kwa kutambua umuhimu wa ukanda huu, serikali ya awamu ya tano imekuwa ikifanya jitihada za makusudi ambazo zitakuwa ni chachu katika kukuza utalii. Jitihada hizo ni pamoja na kuzinduliwa kwa mpango wa uwekezaji katika miundombinu ya mradi wa kuendeleza utalii ukanda wa Kusini mwa Tanzania (REGROW) eneo la Kihesa, Kilolo mkoani Iringa. Mradi huo ulizinduliwa hivi karibuni na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Bi. Samia Suluhu na kuhudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Dkt. Hamisi Kigwangala. 
Pamoja na jitihada hizo watalii na watanzania kwa ujumla wanahitaji kujua vivutio vinavyopatikana katika eneo hilo. Kwa kutambua umuhimu wa kutoa elimu juu ya vivutio mbalimbali nchini Tanzania, Jumia Travel imekukusanyia vivutio na shughuli zifuatazo za kitalii pindi utembeleapo eneo la Kusini mwa Tanzania.
Iringa. Mkoa wa Iringa ni kivutio tosha kutokana na historia yake ndefu tangu enzi za utawala wa kikoloni wa Wajerumani. Ni eneo ambalo Wajerumani walijenga ngome yao kwa ajili ya kupambana na vuguvugu za harakati za kukataa kutawaliwa kutoka kwa kabila la Wahehe ambazo ziliongozwa na Chifu Mkwawa. Mji huu ambao ulijengwa tangu karne ya 19 una mambo mengi ya kujifunza na kujionea pindi utembeleapo ambayo hayapatikani sehemu yoyote nchini. 
Isimila. Mbali na harakati za wazi za kupinga ukoloni wa Wajerumani, eneo la Kusini linasifika kwa kupatikana kwa mabaki ya historia za kale. Eneo hili limegundulika kuwa na masalia ya kutosha ya zana za kale za Zama za Chuma kuliko eneo lolote duniani, ambapo inasemekana ni maeneo ya mwanzo kabisa kuzalisha zana za viwandani na vichwa vya mishale.
Bonde la Kilombero. Ukubwa wa bonde hili ambalo hujaa maji kwa msimu umelifanya kuwa ndilo kubwa katika ukanda wa Afrika ya Mashariki. Kuna shughuli nyingi za kufanya kama mtalii na mambo kadhaa ya kujifunza pindi utembeleapo eneo hili linalopatikana mkoani Morogoro. Miongoni mwa shughuli za kufurahia ni pamoja na kujionea ndege wa aina mbalimbali wa kuvutia pamoja na shughuli za kijadi za wakazi wa eneo hilo kama vile uvuvi.
Hifadhi ya Taifa ya Mikumi. Kama unaishi Dar es Salaam itakuchukua mwendo wa nusu siku kwa gari ili kufika kwenye mbuga hiyo. Ikiwa imezungukwa na safu ya milima, hifadhi hiyo ya taifa inatoa mandhari nzuri ya mawio na machweo. Mikumi ni mahali pazuri kwa kujionea wanyama wa aina mbalimbali wanaoonekana kwa urahisi na ndani ya muda mfupi. Lakini pia ni sehemu ambayo unaweza kuvinjari aina tofauti za ndege.  

Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Mbuga hii ni maarufu kwa kujionea wanyama mbalimbali ambao watalii wengi hupendelea kuwaona. Ukiwa kwenye hifadhi hii wanyama kama vile chui, duma, simba na mbwa mwitu ni jambo la kawaida kuwaona. 
Selous. Hii ndiyo hifadhi inayoshikilia rekodi ya ukubwa duniani kama ulikuwa haufahamu. Kutokana na ukubwa huo hutoa fursa ya kuwatazama wanyama kwa utulivu zaidi kwani watalii sio wengi tofauti na ukanda wa Kaskazini. Hifadhi ya mbuga ya Selous ni nyumbani kwa wanyama wakubwa kama vile simba, chui, mbwa mwitu, viboko na makumi ya maelfu ya tembo. 


Milima ya Udzungwa. Hifadhi ya Taifa ya milima ya Udzungwa ni hifadhi ya misitu ambapo hurusiwa kutembea pekee. Miongoni mwa vivutio ukiwa hapa ni pamoja na kuvinjari matembezi katikati ya msitu wenye miti mirefu yenye urefu wa takribani mita 60 na kujionea maporomoko marefu ya maji yanayotiririka kutoka milimani. Safu ya milima ya Udzungwa ina utajiri wa takribani 40% ya misitu na wanyama wa aina mbalimbali. 


Milima ya Uluguru. Badala ya kufunga safari kwenda mikoa ya Kaskazini unaweza kutembelea safu ya milima ya Uluguru ambayo ipo umbali mchache kutokea mji wa Morogoro. Ikiwa na urefu wa takribani mita 2300, milima hii itakupatia wasaa mzuri wa kuepuka pilikapilika za jiji la Dar es Salaam. Kama kupanda milima hiyo haitoshi, eneo hili pia limepakana na Hifadhi za Taifa za Selous na Mikumi.  
Zipo shughuli nyingi za kufanya na mambo ya kuvutia pindi utembeleapo vivutio vilivyopo eneo la mikoa ya Kusini. Lakini ni karibu zaidi na hivyo kuokoa gharama za usafiri kwani hakuna umbali mrefu. Faida nyingine ni kwamba kutokana na watalii wengi kumininika ukanda wa Kaskazini, maeneo ya Kusini hutoa fursa ya kujionea vivutio vingi zaidi kwa utulivu bila ya kuwa na msongamano mkubwa.

Friday 23 February 2018

WAKUU WA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA WATEMBELEA UKUTA MIRERANI



Mkuu wa majeshi ya ulinzi ya wananchi Tanzania, Venance Mabeyo (kushoto) akionyeshwa ramani na Mkurugenzi mwendeshaji wa Suma JKT ujenzi, mhandisi Morgan Nyonyi, ya ukuta uliojengwa kuzunguka migodi ya madini ya Tanzanite ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, alipotembelea eneo hilo jana, katikati ni mkuu wa polisi nchini, IGP Simon Sirro.



Wakuu wa vyombo vya ulinzi, usalama, magereza na uhamiaji nchini, wakiwa kwenye lango la ukuta uliojengwa kuzunguka migodi ya madini ya Tanzanite yaliyopo Mji mdogo wa Mirerani.



Mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP Simon Sirro, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea eneo lililojengwa ukuta katika machimbo ya madini ya Tanzanite, Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.

Wakuu wa vyombo vya ulinzi, usalama, magereza na uhamiaji nchini, wakiwa kwenye lango la ukuta uliojengwa kuzunguka migodi ya madini ya Tanzanite yaliyopo Mji mdogo wa Mirerani.


Mkurugenzi mwendeshaji wa Suma JKT ujenzi, mhandisi Morgan Nyonyi, akionyesha ramani ya ukuta uliojengwa kuzunguka migodi ya madini ya Tanzanite ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kwa viongozi wa kitaifa wa kamati ya ulinzi, usalama, magereza na uhamiaji walipotembelea eneo hilo.