Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya
Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, limepitisha kutolewa kwa zaidi ya sh100
milioni kwa ajili ya mikopo ya kuwezesha wanawake na vijana kwa lengo la
kuwanyanyua kiuchumi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya
ya Simanjiro Jackson Sipitieck akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani
kilichofanyika mji mdogo wa Orkesumet, alisema fedha hizo zimetokana na
asilimia 10 za mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.
Sipitieck alisema baraza la madiwani
wa halmashauri hiyo wamekuwa na kawaida ya kupitisha fedha hizo ambazo kwa
namna moja au nyingine zitafanikiwa kubadili maisha ya vijana na wanawake wa
eneo hilo.
“Tumefanikiwa kugawa fedha hizo
kwenye kata mbalimbali za halmashauri ya wilaya yetu ambayo ina kata 18 na tutaendelea kuzigawa kwa haki
kwa vikundi vingine vilivyokidhi masharti na vigezo vya kupatiwa,” alisema Sipitieck.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya hiyo Yefred Myenzi alisema hadi hivi sasa fedha hizo sh100 milioni
zimetolewa kwa vipindi tofauti na kikao cha baraza hilo kimepitisha fedha
nyingine sh32.6 milioni zitakazopatiwa kwenye kata sita.
Myenzi alitaja kata hizo sita za
Mirerani, Oljoro namba tano, Shambarai, Komolo, Loiborsiret na Msitu wa Tembo
ambapo vimetolewa kwa vikundi 16 vya wanawake na vijana wa Simanjiro.
Alisema halmashauri hiyo itaendelea
kutoa fedha hizo pindi itakapokuwa inakusanya makusanyo yake ya ndani hivyo
wanawake na vijana wachangamkie fursa hiyo kupitia asilimia 10 za mapato ya
ndani.
Diwani wa kata ya Loiborsiret,
Ezekiel Lesenga Mardadi amewataka wanawake na vijana wa kata hiyo waliopatiwa
mikopo hiyo kuitumia kwa malengo sahihi ili waweze kurejesha kwa wakati.
Mardadi alisema endapo vijana na
wanawake hao wataitumia vizuri mikopo hiyo watajinyanyua kwenye biashara zao na
watarejesha kwa wakati ili wengine nao waweze kufaidika.
Diwani wa kata ya Shambarai Julius
Mamasita alisema vijana na wanawake wa kata yake wana ari kubwa ya kutumia
mikopo hiyo kwa lengo la kujinyanyua kiuchumi na wametoa ahadi kuwa
watafanikisha hilo.
“Naishukuru halmashauri ya wilaya ya
Simanjiro kwa kutupatia mikopo hii nasi wananchi wa kata ya Shambarai tutaweza
kutumia mikopo hii ipasavyo na kisha kuirejesha kwa wakati,” alisema
Mamasita
No comments:
Post a Comment