Tuesday 17 October 2017

HONGERA DC SIMANJIRO ZEPHANIA CHAULA

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Mhandisi Zephania Chaula akivishwa vazi la asili na wananchi wa Kijiji cha Emboreet baada ya kuwazindulia madarasa mawili na nyumba ya walimu kwenye shule ya msingi Emboreet.


RC BENDERA AWATAKA WAKULIMA WA MBAAZI MANYARA KUTOKATA TAMAA


Mkuu wa mkoa wa Manyara,  Dk Joel Bendera amewataka wakulima kutokata tamaa ya kulima zao la mbaazi kutokana na zao hilo kutokuwa na bei nzuri kwa mwaka huu 

Dk Bendera aliyasema hayo kwenye mkutano mkuu wa 10 wa Mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA) mkoani Manyara uliofanyika kwenye ukumbi wa White Rose mjini Babati.

Alisema anajua fika kuporomoka kwa bei ya zao hilo kumewaathiri wakulima wengi kwani ndilo zao kubwa la biashara ambapo mwaka jana walipambania bei ya zao hilo na kufikia kuuzwa sh1,600 kwa kilo na mwaka huu zao hilo kufikia kuuzwa kwa sh250 kwa kilo kutokana na wanunuzi wakubwa wa zao hilo ambao wapo India kudai kuwa wametosheka na mbaazi.

"Wakulima wanalima kulingana na soko, kwa bei hii ya mbaazi nani utamshawishi alime mbaazi mwakani, ndio maana tunasisitiza pamoja na kilimo tuwe na viwanda ili tuongeze thamani mazao yetu wenyewe," alisema Dk Bendera.

Alisema baada ya zao la pamba kushuka bei  wakulima walihamia kwenye mbaazi na mbaazi imeshuka bei wakulima watakosa la kufanya ila wasikate tamaa waendelee kulima, kwani kutatengenezwa kiwanda cha kubangulia mbaazi ili ifungashwe kwenye mifuko kisha ikauzwe nje ya nchi siyo lazima India pekee.

Aliwataka maafisa ugani wa halmashauri kuacha kukaa maofisini na badala yake kushirikiana na Mvitawa ili kuboresha teknolojia ya kilimo katika mkoa wa Manyara na kuwafundisha wakulima namna ya kulima kisasa, kuacha nafasi, kutumia mbolea na mbegu bora za kutumia.

"Hatuna maofisa ugani wa kutosha, angalau kila kata wawepo watatu, lakini hata hao waliopo kazi yao si kukaa maofisini watoke nje watu bado wanalima kienyeji  kazi zao zote wamewaachia Mviwata, kupitia halmashauri tutoe wataalamu wa wa kilimo kwa kushirikiana na Mviwata," alisema Dk Bendera.
Tatizo la  mbegu za bandia nchini bado ni changamoto kubwa kwa wakulima, kwani wakulima wa mkoa wa Manyara wamekuwa wakinunua mbegu ambazo wakizipanda zinakaa ardhini kwa muda mrefu bila mazao kuota hali inayolalamikiwa na wakulima wengi.

Mratibu wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) mkoani Manyara, Martin Pius alisema pamoja na nia nzuri ya Serikali ya kutaka kukuza kipato cha mkulima kwa kuongeza bei ya chakula  anaiomba serikali upatikanaji wa bembejeo ya urahisi na gharama nafuu kwani kumekuwa na utolewaji wa pembejeo bandia na kwa bei ya juu kutoka kwa wakala wanaopewa kazi hizo na serikali.

“Kutokana kubadilika kwa tabia ya nchi mbegu zilizobadilishwa vinasaba siyo njia ya kutatua changamoto hiyo, hivyo wataalamu wa kilimo wanapaswa kutafuta njia nyingine zitakazoleta tija kwa mkulima na siyo zitakazoongeza changamoto,” alisema Pius.

Alisema mkutano wa mwaka huu umebeba kauli mbiu inayosema ‘uhakika wa mbegu kwa uhakika wa chakula' lakini kauli mbiu hiyo anaeleza bado ni changamoto kwani mbegu zinazosambazwa sio halisi.

Alisema baadhi ya wakulima wa mkoa huo wamekuwa wakiuziwa mbegu bandia za kilimo hali inayowarudisha nyuma katika shughuli za kilimo na pia kuwasababishia njaa.

FAINALI YA KOMBE LA USALAMA MANYARA KUFANYIKA OCTOBA 20

 Fainali ya soka ya mashindano ya Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Manyara, Usalama Cup inatarajiwa kufanya Octoba 22 mwaka huu. 

Msemaji wa mashindano hayo, Masudi Fupe akizungumzia michuano hiyo alisema mshindi wa mashindano hayo atapata kombe na sh1 milioni. 

Fupe alisema fainali hiyo itafanyika kwenye uwanja wa Kwaraa mjini Babati ambapo mshindi wa pili atapata zawadi ya 700,000. 

Alisema nusu fainali ya kwanza itawakutanisha timu ya Kariakoo ya Gidas kata ya Bonga dhidi ya City boys ya mjini Babati. 

Alisema nusu fainali ya pili itazikutanisha timu ya Veta SC ya Wang'warai dhidi ya Stend FC (chama la wana). 

"Pia mshindi wa tatu atapata zawadi ya sh450,000 mshindi wa nne atapata sh200,000 na kipa bora, mchezaji bora na timu yenye nidhamu atajipatia sh30,000 kila mmoja," alisema Fupe. 

Alisema timu 16 zilijitokeza kushiriki michuano hiyo kwa makundi manne na kila kundi lilitoa timu mbili zilizoingia robo fainali. 

Alisema lengo la mashindano hayo ni kutoa elimu kwa jamii juu ya kupunguza uhalifu, kupiga vita ujangili, kupinga mimba za utotoni na jamii kuwa karibu na polisi. 

"Siku ya fainali tunatarajia mgeni rasmi atakuwa mkuu wa mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera ambaye atakabidhi kombe kwa washindi na zawadi nyinginezo," alisema Fupe. 

Friday 6 October 2017

KIKAO CHA BARAZA LA MADIWANI HALMASHAURI YA WILAYA YA MBULU

 Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mkoani Manyara, Flatei Gregory Massay akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo.
 Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, wakiwa kwenye kikao cha baraza hilo.
 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Michael Faaray akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.
Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Manyara, Marthu wa Umbullah akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu.