UCHUMI NA BIASHARA

2 comments:

  1. ASASI isiyo ya Kiserikali ya Haki Madini inatarajia kuandaa jukwaa la wachimbaji wadogo na wataalam wa sekta ya madini toka mataifa ya Ghana,Trinidad na Tobago pamoja na wataalam wa sekta hiyo wa chuo kikuu cha Dar-es-salaam.

    Akizungumza na Mireranitanzanite Mratibu wa Haki Madini Tawi la Mirerani,David Ntiruka alisema Haki Madini wameandaa jukwaa hilo linalotarajiwa kufanyika mwezi Agusti mwaka huu jijini Dare-s-salaam.

    Ntiruka alisema Haki Madini wameamua kuandaa jukwaa hilo lenye lengo la kuwajengea uwezo zaidi wachimbaji wadogo ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya kazi zao katika mazingira magumu.

    Alisema miongoni mwa watoa mada kwenye jukwaa hilo ni pamoja na maprofesa,wataalamu wa uchumi,maprofesa na wanaharakati mbalimbali wa hapa nchini na wengine kutoka Ghana na Trinidad na Tobago.

    “Hivi sasa Mkurugenzi wa Haki Madini Amani Mustapha yupo kwenye mchakato wa kuandaa jukwaa hilo pamoja na kuonana na wataalamu hao ili kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda vizuri,” alisema Ntiruka.

    Asasi ya Haki Madini yenye makao yake makuu mjini Arusha imekuwa ikiwatetea wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani,Dhahabu mkoani Singida na Tomarini ya kijani wa mkoani Tanga.

    Kupitia Mkurugenzi wake Amani Mustapha,Haki Madini ambayo ilianza na ofisi yao mji mdogo wa Mirerani imejipatia umaarufu mkubwa hapa nchini kutokana na kutetea maslahi ya wachimbaji wadogo na jamii zilizopo pembezoni.

    Baadhi ya wachimbaji wadogo walidai kuwa Haki Madini imekuwa msaada mkubwa kwao kutokana na kuwajengea uwezo ili watambue namna ya kupata haki zao za msingi katika sekta hiyo.

    MWISHO.

    ReplyDelete
  2. Joseph Lyimo,Babati
    JAMII imetakiwa kutojenga makazi karibu na hifadhi za Taifa kwani wanachangia uharibifu wa maeneo hayo ikiwemo vifo vya wanyamapori ambao wanategemewa na Taifa kwa kuongeza fedha za kigeni kupitia utalii.

    Hayo yameelezwa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Dk Rehema Nchimbi kwenye tafrija ya kumuaga aliyekuwa Mhifadhi mkuu wa hifadhi ya Taifa ya Tarangire,Martin Loibooki na kumkaribisha Mhifadhi mwingine Steveen Quolli.

    Dk Nchimbi alisema hifadhi ya Taifa ya Tarangire ambayo sehemu yake ipo Mkoani Manyara na wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma na wilaya ya Monduli Mkoani Arusha inatakiwa ienziwe na kutunzwa kwani inafaida kubwa kwa Taifa.

    Alisema hifadhi ya Taifa ya Tarangire yenye tembo wakubwa zaidi duniani pia ni hifadhi ya tatu kati ya hifadhi 16 nchini,kwa kuingiza mapato kupitia fedha za kigeni,inatakiwa kutunzwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya maslahi ya Taifa.

    “Jamii inayoishi pembezoni mwa hifadhi za Taifa inatakiwa kutozidi kukaribia hifadhi hizo kwani uchumi wa nchi unategemea mapato kutoka kwenye mbuga zetu ambazo zinaingiza kwa wingi fedha za kigeni,” alisema Dk Nchimbi.

    Aliwataka baadhi ya wanasiasa kutopotosha jamii kwa kutoa kauli zisizo na mashiko kwa kuwaambia Serikali ina thamini wanyama kuliko binadamu kwani wanyama,ndege na samaki wakipotea dunia itakuwa kwenye wakati mgumu.

    Kwa upande wake,Mkuu wa mkoa wa Manyara,Elaston Mbwilo alisema katika eneo la Kibaoni Minjingu kuna baadhi ya watu wameiingilia hifadhi ya Tarangire kwa kujenga kwenye njia ya kupita Tembo hivyo kuwaathiri wanyama hao.

    Mbwilo alisema jamii inatakiwa ielimishwe maana ya kuwa na hifadhi za Taifa kwa kuwaiga wakazi wa wilaya ya Simanjiro ambao kipindi cha mwezi Januari hadi Aprili huishi na wanyamapori bila kuwadhuru kwa kuwawinda.

    MWISHO.

    Joseph Lyimo,Babati
    IMEELEZWA kuwa matukio ya ujangili kwenye Hifadhi ya Taifa ya Tarangire yamezidi kupungua kwani kwa muda wa miezi sita iliyopita hakukuwepo na matuki makubwa ya kuuawa tembo wa hifadhi hiyo.

    Hayo yalisemwa juzi na aliyekuwa mkuu wa hifadhi ya Tarangire,Martin Loibooki ambaye hivi sasa ni mkurugenzi wa uhifadhi wa hifadhi za Taifa (Tanapa) wakati wa tafrija ya kumuaga na kuukaribisha mwaka mpya.

    Loibooki alisema hivi sasa ujangili umepungua kwa kiasi kikubwa kwenye hifadhi hiyo ambayo sehemu yake kubwa ipo wilayani Babati mkoani Manyara na eneo la wilaya Kondoa mkoani Dodoma na wilayani Monduli mkoani Arusha.

    Alisema ujangili huo umepungukua kwa kiasi kikubwa kutokana na ushirikiano wanaopewa na jamii inayozunguka eneo hilo,askari wao na askari polisi kwani walifanikiwa kukamata silaha mbalimbali ikiwemo bunduki kubwa na risasi.

    Alisema miongoni mwa changamoto zinazowakabili ni migogoro ya mipaka baina ya hifadhi hiyo na vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo ikiwemo kijiji cha Kimotorok cha kata ya Loiborsiret wilayani Simanjiro.

    “Tunashukuru hivi sasa mgogoro huo umefikia tamaki kwani Mwenyekiti wa kijiji hicho na wananchi wake wametambua umuhimu wa hifadhi hii ya Taifa ya Tarangire ambayo ni ya tatu kwa kuingiza mapato nchini,” alisema Loibooki.

    Naye,mkuu wa mkoa wa Manyara,Elaston Mbwilo alisema baadhi ya watu wanaohujumu hifadhi za Taifa kwa kufanya ujangili hawana uzalendo na hawatangulizi maslahi ya Taifa kwani hifadhi zinaingiza fedha nyingi za kigeni.

    “Fedha za kuwalipa mishahara walimu,madaktari,askari wetu na watumishi wengine wa Serikali zinatokana na fedha zinazoingia kupitia utalii hivyo jamii inapaswa kutunza hifadhi ili hifadhi nazo zitutunze,” alisema Mbwilo.

    Kwa upande wake,mkuu wa mkoa wa Dodoma Dk Rehema Nchimbi alisema kufanya kazi kwenye hifadhi ya Taifa kunahitaji uzalendo,uvumilivu na upendo wa kutumikia nchi.

    “Pamoja na hayo nawapongeza sana waandishi wa habari kwani kupitia runinga,redio na magazeti wameshiriki kuendeleza hifadhi kwa kutangaza hifadhi zetu katika vyombo vyao vya habari,” alisem Dk Nchimbi.

    MWISHO.

    ReplyDelete