Tuesday, 8 May 2018

KAMOGA AWATAKA WATUMISHI MBULU KUJITATHMINI

 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Kamoga (kulia) akizungumza kwenye sherehe za wafanyakazi za Mei mosi zilizofanyika mji mdogo wa Haydom.
  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Kamoga (kulia) akipima afya yake kama mfano wa wafanyakazi wa halmashauri hiyo kushiriki kupima afya zao na kufanya mazoezi kila jumamosi ya mwisho wa mwezi.
 Watumishi wa benki ya CRDB Tawi la Haydom Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, wakiwa kwenye banda lao katika sherehe za wafanyakazi za Mei mosi zilizofanyika kiwilaya mji mdogo wa Haydom.
 Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Deogratias Kawogo (wapili kulia) Mkurugenzi wa hospitali ya rufaa ya Haydom Dkt Emmanuel Nuwass (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Hudson Kamoga (watatu kulia) wakiwa kwenye jukwaa kuu wakati watumishi wa serikali na sekta binafsi wakipita jukwaani katika sherehe za wafanyakazi Mei mosi zilizofanyika mji mdogo wa Haydom.


  Watumishi wa benki ya NMB Tawi la Haydom Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, wakiwa kwenye banda lao katika sherehe za wafanyakazi za Mei mosi zilizofanyika kiwilaya mji mdogo wa Haydom.
Watumishi wa serikali na sekta binafsi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, wakiimba wimbo wa mshikamano kwenye sherehe za wafanyakazi za Mei mosi zilizofanyika kiwilaya mji mdogo wa Haydom. 

 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Kamoga amewataka watumishi wa Halmashauri hiyo wajitathmini wao binafsi namna wanavyotoa huduma kwa jamii kama ina tija.

Kamoga aliyasema hayo kwenye sherehe za wafanyakazi za Mei mosi zilizofanyika kiwilaya mji mdogo wa Haydom.

Kamoga alisema watumishi wa umma wanapaswa kujitambua namna wanavyotoa huduma kwa jamii ili faida yake ionekane mahali pa kazi kwa kila mmoja kwenye halmashauri hiyo.

Alisema kila mwananchi wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu anapaswa kuona fahari kwa watumishi wa serikali wanavyotoa huduma nzuri kwao.

"Jamii inapaswa kuona fahari ya uwepo wetu hata baba wa Taifa alikuwa anasema ualimu ni wito na mimi nawaambia utumishi ni wito, alisema Kamoga.

Aliwataka watumishi hao kupitia idara na vitengo mbalimbali kutoa huduma kwa jamii ipasavyo kwani wakifanya kazi vizuri sifa zinakuja kwake na wakiharibu analaumiwa yeye.

"Ninyi ni wawakilishi wangu mtambuwe hilo kuwa mnaniwakilisha mimi kila mahali mlipo kwani mkiharibu mimi ndiyo nitalaumiwa na mkifanya vizuri pongezi zinakuja kwangu," alisema Kamoga.

Meneja wa benki ya CRDB Tawi la Haydom, Ronald Massawe amesema wamejipanga ipasavyo kuhakikisha wanawapatia mikopo yenye riba nafuu watumishi mbalimbali.

Massawe alisema wanatoa mikopo yenye ribaa nafuu kwa watumishi mbalimbali ikiwemo wa miaka sita ambapo riba ni asilimia 20 kwa watumishi wa serikali na watumishi wasio wa serikali watalipia asilimia 21.

Alisema pia benki hiyo huwa inatoa huduma mpya ya mikopo ya sekunde kwa watumishi inayopatikana kwa njia ya simu za mikononi.

Hata hivyo, mwalimu wa shule ya msingi Endagulda kata ya Eshkesh, Emmanuel Maega ameiomba serikali kuboresha maslahi na miundombinu ya walimu wanaoishi maeneo ya pembezoni ili waweze kufundisha vizuri.

Maega alisema walimu wanaoishi maeneo ya pembezoni wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa nyumba za walimu hali inayosababisha wafanye kazi kwenye mazingira magumu.

"Tunaomba sisi tuliopo pembezoni tujengewe nyumba za kutosha za walimu ili tuishi vizuri kwani tuna changamoto ya nyumba chache za kuishi walimu hali inayotupa wakati mgumu katika kutumikia jamii, alisema.






No comments:

Post a Comment