Saturday, 20 May 2017

HAKI MADINI KUANDAA MDAHALOWachimbaji wadogo wa madini, wachuuzi na madalali wa madini nchini wanatarajia kufanya mdahalo wa kitaifa juu ya umuhimu wa sekta ya madini na namna ya kuwanufaisha zaidi.

Mkurugenzi wa shirika la Haki Madini Amani Mhinda, akizungumza mji mdogo wa Mirerani na viongozi wa chama cha wachimbaji madini mkoani Manyara (Marema) alisema mdahalo huo utafanyika mkoani Geita.

Mhinda alisema lengo la mdahalo huo ni kuwaleta wadau mbalimbali kwa pamoja ili kuzungumzia changamoto zinazoikabili sekta hiyo kwa wachimbaji wadogo na kutafakari kitaifa maono ya wachimbaji.  

Alisema wanatarajia kufanya mdahalo huo mwishoni mwa mwezi Juni kwa kushirikiana na shirika kiongozi duniani la maendeleo la International Institute for Environment and Development (IIED).“Haki madini tunarajia mpango huu utatoa jukwa hitajika kwa wadau kushirikiana na kubadilishana ujuzi na kukuza utawala bora kuwa sauti kubwa, usalama na utengenezaji,” alisema Mhinda.

Alisema uchimbaji mdogo wa madini unaweza kutoa mchango chanya wenye umoja na usawa wa maendeleo endelevu na ukuaji wa uchumi, kwani husaidia mamilioni ya watu hasa wanawake na watoto.

Katibu wa Marema Tawi la Mirerani, Abubakari Madiwa alisema kupitia mdahalo huo wanatarajia wachimbaji mdogo kunufaika kwa kujengewa uwezo hivyo wamejiandaa kushiriki mara utakapofanyika.

“Haki madini imekuwa msaada mkubwa kwa wachimbaji madini wadogo kwani tumekuwa pamoja bega kwa bega kwa kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata haki zao,” alisema Madiwa.

MBUNGE MARTHA UMBULLAMbunge wa Viti maalum Mkoani Manyara, Martha Umbulla akizungumza na wanachi wa Mji mdogo wa Haydom juu ya kuwezesha vikundi vya maendeleo.

DED MBULU HUDSON KAMOGAMkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Starnley Kamoga akizungumza na wananchi wa mji mdogo wa Haydom juuu ya kuchangia maendeleo yao.

DC MBULU AWAASA WANANCHIMkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Chelestino Mofuga amewataka wakazi wa Kijiji cha Guye kuacha malumbano na kujenga madarasa ya shule ya msingi kwa muda wa mwezi mmoja.

Mofuga akizungumza na wananchi wa kijiji hicho, alisema anahitaji apatiwe mpango wa maendeleo wa kijiji, apatiwe taarifa hiyo ofisini kwake ikiwemo kujenga madarasa kwa mwezi mmoja.

Alisema pamoja na serikali kuwa na sera ya elimu bure na elimu bila malipo lakini wananchi wanapaswa kujenga madarasa ya shule ili wanafunzi wao waweze kupata elimu kwenye mazingira mazuri.

“Ni kijiji cha ajabu kweli kweli, yaani ninyi mnakaa mwaka mzima lakini hakuna shughuli za maendeleo, kule watoto wanasoma wenu wanasoma kwa mazingira magumu ya madarasa,” alisema Mofuga.

Alisema endapo kuna mapungufu mengine kwenye shule hiyo ikiwemo nyumba za walimu, wananchi hao wanapaswa kuhakikisha yanajengwa kwani hiyo ni kwa jaili ya faida ya watoto wao.

Mkazi wa kijiji hicho cha Guye, John Akonaay alisema anasikitishwa na kitendo cha baadhi ya wananchi wa kijiji hicho kuwa na mwamko mdogo wa kuchangia kutokana na ufujaji wa fedha uliofanyika.

“Tunashukuru mkuu wa wilaya leo (juzi) umeagiza yule mtendaji wa kijiji aliyefuja fedha zetu amekuja na kujibu tuhuma kuwa atazilipa ila tukichanga tena huyu mtendaji mpya asizifuje,” alisema Akonaay.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho Adam Sule alisema anasikitishwa na kitendo cha kuambiwa kuwa wakili aliyekuwa anafuatilia kesi ya ufujaji wa fedha za kijiji anawadai sh1.5 milioni hivyo walipe.

“Tulishamlipa huyo mwanasheria lakini hivi sasa bado tunaambiwa tunadaiwa ili hali kwenye taarifa ya awali inaonyesha alishalipwa sh150,000 ya usafiri wa kutoka Babati hadi hapa,”  alisema Sule.

MWISHO.