Diwani wa Kata ya Loiborsiret
Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Ezekiel Lesenga (Mardadi) ameitaka
Halmashauri ya Wilaya hiyo kuwaangalia wananchi wake kwa jicho la huruma ili
waweze kupata huduma ya uhakika wa maji kwani wengi wao wanatumia maji kidogo
yaliyopo kwa kushirikiana na mifugo.
Mardadi alisema wananchi wa kata yake
wanaishi kwenye nyanda kame hivyo halmashauri hiyo ifanye jitihada za kuwezesha
upatikanaji wa huduma hiyo ili waondokane na kero ya maji.
Alisema suala la tatizo la maji ni
kero ya muda mrefu na yeye kama diwani wa eneo husika ataendelea kulisemea hilo
hadi ufumbuzi upatikane kwa wananchi wake wa kata ya Loiborsiret.
"Hali ya wananchi wa eneo hilo
kwenye huduma ya maji ni ndogo kwani hivi sasa wanategemea mabwawa yaliyojaa
maji kutokana na mvua ndiyo wanatumia wao na mifugo," alisema Mardadi.
Alisema wakati wa kiangazi unapofika
maji ya kwenye mabwawa hukauka na kuwapa wakati mgumu binadamu na mifugo kupata
huduma ya maji.
Alisema kwenye kata yake ya
Loiborsiret suala la maji ni tatizo kubwa kwenye vijiji vyote vya Loiborsiret,
Kimotorok na Narakauwo.
Alisema anatarajia halmashauri ya
wilaya ya Simanjiro italiangalia suala hilo kwa upana zaidi ili huduma ya maji
kwenye eneo hilo iwe ya uhakika tofauti na sasa.
"Wakati wa kiangazi jamii ya
eneo hilo hupata wakati mgumu kwani maji yanapatikana kwa shida hivyo
kusababisha mifugo kufa na wananchi nao wanateseka," alisema Mardadi.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa kamati ya
Elimu, Afya na Maji wa baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo Sendeu
Laizer akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita alisema wamepanga kuchimba
kisima kimoja kwenye kata hiyo.
"Kamati yetu kwenye mapendekezo
yake iliazimia kuchimbwe kisima kimoja katika kijiji cha Narakauwo kata ya
Loiborsiret ili jamii ya eneo hilo na mifugo waweze kupata huduma ya
maji," alisema Laizer.
No comments:
Post a Comment