Tuesday 8 May 2018

NAIBU WAZIRI OLE NASHA AWAPA MWEZI MMOJA MAMIRE KUPATA HATI YA KIWANJA


 NAIBU Waziri  wa Elimu Sayansi  na Mafunzo ya Ufundi, William Ole Nasha ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mkoani Manyara na uongozi wa chuo cha ualimu Mamire kukamilisha mchakato wa kuhakikisha wanapata hati miliki ya ardhi ya chuo hicho ndani ya mwezi mmoja.

Ole Nasha alilitoa agizo hilo kwenye mahafali ya tatu ya kuwaaga walimu 102 waliofuzu masomo yao kwa kipindi cha miaka miwili waliyosoma kwa ngazi ya cheti.

Alisema chuo hicho kuendelea kutokuwa  na hati miliki ya ardhi inayotumia jina la chuo ni  moja ya sababu ya kuifanya serikali ishindwe kukijengea miundo mbinu ya  kutosha  kwa kuwa serikali inafanya ukarabati wa vyuo vya ualimu vyote ila kipaumbele ni kwa wale wenye hati miliki ya vyuo vyao.

“Nawataka ndani ya mwezi mmoja muwe na hati miliki ya chuo iliyoandikwa kwa jina lenu na siyo jina la WDC  ili kuruhusu shughuli zingine za kiserikali ziweze kufanyika  vizuri na chuo kiweze kujengewa miundo mbinu,’’ alisema.


“Mfanye haraka kukamilisha  mchakato huu na tayari nimeishaongea na mwanasheria wa wizara ya ardhi kuhusu jambo hili ameniambia linawezekana  na akasema hata kama mkiamua kua na hati ya kimila huku mnaendelea na mchakato huu,’’ alisema.

Alikubali kupunguza kero ya miundo mbinu michache  iliyoibuliwa na mkuu wa chuo hicho  Nada Nyabasi  wakati akisoma risala ambapo aliwaahidi kuwapatia gari moja la chuo, kujenga nyumba mbili za watumishi, kujenga vyumba viwili vya mafunzo ya sayansi kwa vitendo na kuwapatia mhasibu haraka huku mchakato wa kuwaajiri watumishi wengine ukiendelea.

Alisema kama chuo hicho kisingekuwa na tatizo la kukosa  hati miliki ya ardhi yake mwaka huu kingepewa  fedha kwa ajili ya kuboresha miundo mbinu lakini  hicho ndiyo kikwazo cha wao kuondolewa kwenye bajeti  hii.

Alikipongeza chuo hicho kwa kufaulisha miaka miwili mfululizo kwa asilimia 100 ambapo mwaka 2016 na 2017 wanafunzi waliomaliza walifaulu kwa asilimia 100 jambo ambalo kwenye vyuo vingine hakuna.

Awali, mbunge wa Babati Vijijini Vrajilal Jituson alimshukuru Ole Nasha kwani alikuwa msaada mkubwa kabla hajawa kiongozi alikuwa mwanasheria wa shirika la So They Can akitoa ushauri namna ya kufanikiwa hivyo naye anastahili kuwa miongoni mwa waasisi.

“Tunatarajia wewe ambaye uko jikoni utaweza kutupatia upendeleo fulani  kwa ajili ya chuo chetu ili tuweze kukifanya chuo hiki kuwa chuo cha mfano katika nchi hii na hata nje ya nchi hii kwa kuwapika walimu  wazuri,’’ alisema Jituson

Alisema walimu wanaozalishwa na chuo hicho  wapo imara na makini kitaaluma na iwapo serikali itawapangia vituo vya kazi watakapoajiri wawape kipao mbele ili waweze kulitumikia taifa kwa umahiri mkubwa.

Mkurugenzi wa shirika la So They Can kwa upande wa Tanzania anaye iwakishisha nchi ya Australia  ambako ndio makao makuu Terry Anderson alisema  chanzo cha So they can kufadhili masuala ya elimu hapa Babati ni baada ya Peter Hunt aliyekua ameambatana naye wakitalii kutoka Hifadhi ya Taifa ya Tarangire kufika kijiji cha Gijedabung kuona mazingira ya shule hiyo yalivyokuwa yamechakaa.

Anderson alisema ndipo walianza jitihada za kuisaidia shule hiyo na hatimaye kuamua kushirikana na wadau ili kuanzisha chuo cha ualimu kwa ajili ya kupata walimu walio mahiri kuweza kuwafundisha watoto.

Alisema shirika lake litaendelea kuwaunga mkono katika chuo hiki na kukifanya kiwe chuo bora zaidi hapa nchini na nje ya nchi lakini na atazidi kushirikiana na serikali  na amefurahishwa na ahadi ya Naibu Waziri kuwa watawaajiri wanachuo waliomaliza hapa.


No comments:

Post a Comment