Saturday 26 March 2016

RAISA WA FEMATA ATEMBELEA MIGODI YA TANZANITE


Rais wa shirikisho la vyama vya madini nchini (Femata) John Bina amesema migogoro mingi ya madini baina ya wachimbaji wadogo na wachimbaji wakubwa inasababishwa na sheria mbovu za madini zinazotumika hivi sasa.

Bina alidai kuwa sheria nyingi za madini ambazo ni mbovu zimenakiliwa kutoka nchini Uingereza, ambapo hakuna madini ya vito ya Tanzanite na kutumika hapa nchini hivyo kusababisha migogoro ya mara kwa mara ambayo haimaliziki.

Akizungumza kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite ya mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, alisema inatakiwa sheria hizo kandamizi ziondolewe ili wachimbaji wadogo wafanye kazi zao bila kuonewa.

Alitaja miongoni mwa sheria zinazowakandamiza wachimbaji wadogo kuwa ni sheria ya kuchimba madini ya vito ya Tanzanite kwa njia ya wima ili hali jiolojia ya madini hayo yanataka yachimbwe kwa njia ya mshazari.

Alisema kutokana na madini hayo kuwa Tanzania pekee, ingetakiwa sheria, kanuni na taratibu za uchimbaji wa madini ya Tanzanite uwe wa kipekee, kuliko hivi sasa wanapochukua sheria za nje na kuendelea kuzitumia hapa nchini.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoani Manyara (Marema) Sadiki Mneney alisema japokuwa tume nyingi ziliundwa na serikali ili kuhakikisha migogoro hiyo inamalizia lakini hazikufanikiwa.

“Tume nyingi zimeundwa na kufika Mirerani ili kumaliza migogoro yetu na mchimbaji mkubwa ila zikashindwa kumaliza ikiwemo ya Brigedia Jenerali Robert Mboma, Mang’enya, Jaji Mark Bomani na wabunge 25,” alisema Mneney.

Friday 11 March 2016

MAONYESHO YA MADINI YA VITO MIRERANI


Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Mahmoud Kambona amewaagiza wote waliovamia na kujikatia viwanja au kujenga kwenye eneo huru la usafirishaji bidhaa nje (EPZA) waondoke na kubomoa kabla hawajaondolewa kwa nguvu.

Inadaiwa kuwa vigogo watatu wa mji mdogo wa Mirerani, wamejenga nyumba za kuishi kwenye eneo hilo na watu wengine zaidi ya 11 wamejimegea viwanja kiubabe na kujiandaa kujenga ili hali mradi huo unatarajia kuanza kujengwa.



Akizungumza juzi wakati akifungua maonyesho ya madini ya vito ya siku mbili yaliyofanyika mji mdogo wa Mirerani, Kambona alisema mchakato wa kuwalipa fidia waliokuwa wanamiliki eneo hilo upo tayari hivyo wavamizi hao waondoke. 

 Alisema baada ya kuwalipa waliokuwa wamiliki wa eneo la EPZA, mchakato wa ujenzi utaanza mara moja kwani kutajengwa kituo kikubwa cha biashara za kuuza nje ikiwemo soko la madini ya Tanzanite litakalojengwa sehemu hiyo.




Hata hivyo, alipongeza Wizara ya Nishati na Madini kufanya maonyesho hayo kwa mara ya kwanza kwenye mji mdogo wa Mirerani, sehemu yanapopatikana madini ya Tanzanite, kwani itasaidia kuboresha soko la madini katika eneo hilo.

“Ni heshima kubwa tumepatiwa watu wa Simanjiro hususan mji mdogo wa Mirerani, hivyo tutumie fursa hii kwa wachimbaji kuleta madini yetu kwenye maonyesho haya ili kuboresha uchumi wetu,” alisema Kambona.



Mmoja kati ya wachimbaji wa madini ya Tanzanite Saniniu Laizer alisema maonyesho kama hayo yanachangia kutangaza madini hayo, kwani kuna baadhi ya watu wana dhana potofu kuwa yanachimbwa nchi ya jirani.

“Kupitia maonyesho haya tunaiomba serikali iboreshe zaidi sekta ya madini ya vito kwa kuwapa kipaumbele wachimbaji wadogo kwani wana changamoto nyingi zinazowakabili ikiwemo bei kubwa ya zana za milipuko,” alisema Laizer.  



Kwa upande wake, kaimu kamishna wa madini kanda ya kaskazini Elias Kayandabila alisema maonyesho hayo yanafanyika kwa mara ya kwanza mji mdogo wa Mirerani na yanatarajia kufanyika tena mwakani kwenye eneo hilo.

Kayandabila alisema kupitia maonyesho hayo wafanyabiashara wadogo kwa wakubwa wa madini ya vito ikiwemo Tanzanite, Tomarine ya kijani, Garnet ya kijani, Roadlite na mengineno, watanufaika nayo kwa kuboresha masoko yao.

Maonyesho hayo yameandaliwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Nishati na Madini kanda ya ya kaskazini na vyama vya wachimbaji madini (Remas), chama cha madalali wa madini (Tasgedo) na chama cha wauzaji wa madini (Tamida).