Mbunge wa viti maalum wa Mkoa wa
Manyara, Esta Mahawe amemkabidhi mashuka 20 Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na watu wenye ulemavu) Jenista Mhagama,
yatakayotumika na wanawake waliojifungua kwenye jengo la mama na mtoto katika
kituo cha afya Mirerani Wilayani Simanjiro.
Akizungumza wakati akikabidhi mashuka
hayo Mahawe alisema amejitolea kutoa mashuka hayo kwa lengo la kuwafunika
wanawake watakaojifungua watoto wao kwenye kituo hicho cha watoto.
Alisema mashuka hayo yatakuwa alama
ya upendo kwao kwa wanawake na watoto watakaokuwa wanajifunika pindi
watakapokuwa wanapata huduma ya kujifungua kwenye jengo la mama na mtoto la
kituo cha afya Mirerani.
“Pamoja na hayo mheshimiwa Waziri
tunaomba kituo cha huduma za Ukimwi ambacho umeweka jiwe la msingi leo hapa
Mirerani kijengwe pia kule machimboni ambacho kwa kiasi kikubwa kitawasaidia
vijana wetu wanaochimba madini ya Tanzanite,” alisema Mahawe.
Hata hivyo, Waziri Mhagama
alimpongeza Mahawe aliyejitolea mashuka hayo 20 na yeye akaahidi kutoa mashuka
100 yatakayotumika kwa wanawake watakaojifungua kwenye kituo cha afya Mirerani.
“Pia mbunge mwingine wa viti maalum
wa mkoa wa Manyara, Martha Umbullah naye ameahidi kutoa mashuka 50 kwa ajili ya
wanawake na watoto, hivyo wanaume nao wanunue mashuka ambayo watajifunika
wanaume pindi wakifika kutibiwa kwenye kituo hicho cha afya,” alisema Waziri
Mhagama.
Pia ili kuunga mkono zoezi hilo,
Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Manyara Misaile Mussa kupitia ofisi yake
aliahidi mashuka 50 na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa
Manyara, Mosses Komba aliahidi kujitolea mashuka 20.
No comments:
Post a Comment