Thursday, 17 May 2018

DC MBULU AVUNJA UONGOZI WA SERIKALI YA KIJIJI CHA TUMATI

 Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Chelestino Mofuga ameuvunja uongozi wa Serikali ya kijiji cha Tumati inayoongozwa na Mwenyekiti wa Chadema kwa madai ya kusababisha migogoro na wananchi wao tangu mwaka 2015 hadi sasa.

Mofuga akitoa uamuzi huo jana kwenye mkutano wa kijiji hicho alimuagiza Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Hudson Kamoga kuitisha upya uchaguzi wa kijiji hicho. 

Alisema hawezi kukubali wananchi wanalalamikia serikali ya kijiji inayoongozwa na Mwenyekiti wake Ezekiel Martin (Chadema) nao wasichukue hatua kwa faida ya jamii. 

Alisema malalamiko mengi yametolewa na wananchi kuwa viongozi hao wanasababisha migogoro kila wakati ni bora waondoke ili serikali nyingine ichaguliwe upya. 

"Wananchi wanahitaji viongozi ambao watawaongoza ili wapate maendeleo na siyo matisho na migogoro hivyo ninyi kaeni pembeni mmeshindwa kazi," alisema Mofuga. 

Awali, kwenye mkutano huo baadhi ya wananchi waliwalalamikia viongozi wa kijiji hicho kuwa wanawanyanyasa kupitia uongozi wao hivyo ni bora waondoke madarakani. 

Mkazi wa kijiji hicho Elias Boay alisema viongozi hao wakiongozwa na Mwenyekiti huyo Wamekuwa wakiwanyanyasa wananchi na kuongoza kibabe. 


Mkazi wa kijiji hicho Elias Boay alisema viongozi hao wakiongozwa na Mwenyekiti huyo Wamekuwa wakiwanyanyasa wananchi na kuongoza kibabe. 

"Kwenye kijiji chetu hakuna utawala bora unaofanyika zaidi ya udikteta kwani Mwenyekiti amekuwa akiwaweka rumande kwenye chumba kimoja mwanamke na mwanaume," alisema Boay. 

Alisema Mwenyekiti na serikali yake ya kijiji huwa haisikilizi kero za wananchi na wajumbe wamekuwa wanawatoza watu faini bila kutoa risiti. 

Mkazi mwingine wa kijiji hicho Magdalena Ombay alimuomba mkuu huyo wa wilaya aivunje serikali hiyo ya kijiji kwani tangu mwaka 2015 hadi sasa ni malumbano yanaendelea hivyo kurudisha nyuma maendeleo yao. 

"Wananchi hatuwataki hawa viongozi waondoke tufanye uchaguzi mwingine ili tuwachague viongozi ambao watatuongoza vyema na kuachana na kelele za kila siku," alisema Ombay. 

Hata hivyo, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Ezekiel Martin alisema siasa zimeingizwa kwenye suala hilo kwa sababu ya itikadi ya Chadema aliyokuwa nayo. 


"Hii mizengwe ilikuwa tangu siku nyingi hata mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti alipofanya ziara yake Mbulu na kufika hapa Tumati baadhi ya watu walimwambia majungu," alisema Martin. 

No comments:

Post a Comment