Tuesday 22 May 2018

WAJASIRIAMALI WAASWA

 Wajasiriamali nchini wametakiwa kuwa na nia ya ushindi wa mafanikio kwa uthubutu kufanya jambo la maendeleo kwa lengo thabiti bila kujali vikwazo vilivyopo kwani kukata tamaa ndiyo mwanzo wa kushindwa.

Mkurugenzi wa asasi ya IBN LLC ya jijini Washington nchini Marekani, mhandisi Elic Elisha Bahunde aliyasema hayo kwenye mafunzo ya ujasiriamali yaliyofanyika mji mdogo wa Haydom Wilayani Mbulu Mkoani Manyara na kuandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Hudson Kamoga.

 Mhandisi Bahunde alisema uthubutu na ubunifu ndiyo siri ya mafanikio yeyote yale hivyo wajasiriamali wawe na moyo wa kujaribu jambo ili wafanikiwe maishani.

"Mshindi huwa hakati tamaa, tuthubutu, tujitume, tusikate tamaa na matatizo ni fursa yatumie kuyatatua kwa kuongeza kipato chako," alisema mhandisi Balance.

Ofisa maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Amoniche Mtweve alisema ujasiriamali ni uwezo wa kukubali kuingia katika biashara na kusimamia jambo kwa ujasiri.

Mtweve alisema mjasiriamali anapaswa kuwa na aina tatu za umiliki wa biashara ikiwemo umiliki wa pekee, ubia wa kawaida na ushirika.



 Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu Hudson Kamoga aliwataka vijana kutoishi maisha yao kwa ndoto za mtu mwingine.

"Jitambue kuwa wewe ni wewe na jitahidi kuishi maisha yako kupitia ndoto ulizonazo huku ukimtanguliza Mungu na kuongeza juhudi kwa kile unachokifanya kwa moyo wa dhati utafanikiwa," alisema Kamoga. 
Mratibu wa kituo cha pembe nne za utamaduni Haydom (4CCP) Eliminata Awet amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa wajasiriamali hivyo wangepaswa kujitokeza kwa wingi.

Awet alisema baadhi ya vijana huwa wanalalamika kuwa serikali haiwapi fursa, lakini Kamoga amejitolea kuandaa mafunzo ya ujasiriamali bila malipo wakajitokeza wachache.

Mmoja kati ya washiriki wa Neema Joel alisema kupitia semina hiyo anatarajia kupiga hatua ya maendeleo kwenye ujasiriamali.

Joel alisema amejengewa uwezo zaidi wa ujasiriamali tofauti na awali alipokuwa akijishughulisha na ufugaji wa kuku wa nyama.

Mwanafunzi wa kidato cha tano wa shule ya sekondari Dk Olsen Carren Amani alisema kupitia mafunzo hayo amebaini kuwa siyo lazima uajiriwe serikali au sekta binafsi ila kupitia ujasiriamali unaweza kujiajiri.


No comments:

Post a Comment