Friday 8 May 2015

KONGAMANO LA WAANDISHI WA HABARI NA MVIWATA



Waandishi wa habari nchini wametakiwa kuwapa kipaumbele wakulima wadogo kwa kuandika habari zao kiundani kuliko kuegemea kwa wanasiasa peke yao.

Mwenyekiti wa Mtandao wa vikundi vya wakulima nchini (Mviwata), Veronica Sophu aliyasema hayo mjini Morogoro kwenye kongamano la waandishi wa habari wanaoandika habariza wakulima.

Sophu ambaye alikuwa mjumbe wa Bunge maalum la Katiba (BMK) kupitia kundi la wakulima  alisema wakulima nchini wanatakiwa wasikilizwe kwani wana changamoto nyingi zinazowakabili.

“Kuna changamoto ndogo kati ya waandishi wa habari na wakulima kwani vyombo vingi vya habari vimekuwa vinaegemea kwa wanasiasa na kutuacha wakulima bila kuwa na mahali pa kusemea,” alisema Sophu.





Alisema mara nyingi habari za wakulima wadogo hazipewi kipaumbele zaidi ya migogoro kati yao na wafugaji hivyo waandishi wa habari wabadilike kwa kuwatazama na wao.

“Asilimia kubwa ya watanzania ni wakulima wadogo kwani kila kwenye watu 10 kati yao nane ni wakulima hivyo wapewe kipaumbele kwani bila mkulima mdogo hatuwezi kupata chakula nchini,” alisema Sophu.

Naye, Mkurugenzi mtendaji wa Mviwata Stephen Ruvuga alisema mchango wa waandishi wa habari nchini kwa upande wa wakulima mdogo ni wa muhimu hivyo uzingatiwe.

Ruvuga alisema wakulima wadogo wanatakiwa kuungwa mkono na waandishi wa habari kwa kusemewa kwa namna nzuri zaidi kuliko kuripoti tuu habari hizo bila kuingia kwa undani.

“Wakulima wadogo wana nafasi kubwa katika kuchangia uchumi wa Taifa na jamii kwa ujumla hivyo waandishi wa habari msiangalie tabaka la juu pekee na kuacha kutoa habari za wakulima,” alisema Ruvuga.