Saturday 30 December 2017

KOMBA MWENYEKITI WA UVCCM MANYARA KUPAMBANIA ASILIMIA 5 ZA MIKOPO YA VIJANA

 Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Manyara, Mosses Komba (kulia) akiwa na vijana wenzake wakichagua mahindi ya kuchoma walipofanya ziara ya siku moja ya kutembelea wilaya ya Mbulu. 
 Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Manyara, Mosses Komba (wa pili kulia) akipokea bendera ya Chadema kutoka kwa aliyekuwa mjumbe wa kamati tendaji ya Chadema Wilaya ya Mbulu Stephano Geje wa mji mdogo wa Haydom ambaye yeye na wanachama wengine 10 walijiunga na CCM mjini Mbulu.

 Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Manyara, Mosses Komba (watatu kushoto) akikagua jengo la UVCCM Wilayani Mbulu jana, ambalo liliungua na kuteketezwa na moto Desemba 14 mwaka jana.
 Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Manyara, Mosses Komba (wapili kushoto) akikagua jengo la UVCCM Wilayani Mbulu jana, ambalo liliungua na kuteketezwa na moto Desemba 14 mwaka jana.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoani Manyara, Mosses Komba akizungumza kwenye kikao cha baraza la UVCCM Wilaya ya Mbulu katika ziara yake ya kutembelea wilaya hiyo.

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoani Manyara, Mosses Komba  amesema ameanza mchakato wa kuhakikisha Halmashauri za Wilaya za Mkoa huo zinawapatia vijana mikopo kupitia asilimia 5 ya mapato ya ndani.

Komba aliyasema hayo mjini Mbulu wakati akizungumza kwenye kikao cha Baraza la UVCCM la wilaya ya Mbulu.

Alisema ameshatembelea baadhi ya halmashauri na kukutana na wakurugenzi watendaji hao ambao wamempa utaratibu wa namna ya vijana hao kupata mikopo.

Aliwataka vijana hao kujipanga kwenye hilo kwa kuanzisha vikundi ili mikopo itakapoanza kutolewa wawe wamejiandaa kupitia umoja wao kwa ajili ya kufanikisha suala hilo na kuagiza viongozi wa UVCCM wa wilaya hiyo kusimamia hilo.

"Nilipofika hapa Mbulu nilipita kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya Chelestino Mofuga ili kuzungumza naye aweke msukumo kwenye hilo nikamkosa kwani yupo likizo, lakini nimeacha ujumbe juu ya hilo, hivyo vijana mtumie fursa hiyo," alisema Komba.

Katibu wa UVCCM wilayani Mbulu, Malkiori Pantaleo alisema jumuiya hiyo ina wanachama 15,477 kati yao wanaume ni 9,105 na wanawake ni 6,372.

Pantaleo alisema hivi sasa wana mradi mmoja wa jengo na wamefanikiwa kurejesha ekari 12 za shamba la UVCCM lililokuwa na mgogoro tangu mwaka 2012 kwenye tawi la Getesh kata ya Tumati.

Alisema wapo kwenye mchakato wa ujenzi wa jengo la UVCCM la wilaya hiyo lililoungua kwa moto Desemba 14 mwaka jana, ambalo lilikuwa linaingiza kipato kwenye jumuiya hiyo.

Mbunge wa jimbo la Mbulu mjini Paul Zacharia Isaay, amewataka vijana kupitia ilani ya CCM na kutangaza mazuri yaliyofanywa na chama hicho.

Isaay alisema vijana wakiwa wanajibu hoja kwenye vijiwe mitaani na katika mitandao itasaidia kuweka ukweli hadharani pindi wapinzani wakipotosha maendeleo yaliyofanyika.

Mbunge wa jimbo la Mbulu Vijijini Flatei Massay amewataka vijana wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali pindi zikijitokeza ikiwemo uenyekiti wa vitongoji, vijiji, mitaa, udiwani na ubunge.


Massay alisema vijana wanapaswa kuchangamkia fursa hizo kwa kudhubutu kuchukua fomu na kuacha woga kwani hata yeye alianza kuwa chipukizi, UVCCM na hivi sasa ni mbunge. 

MAGAZETI YA JUMAMOSI LEO DECEMBER 30,2017


SERIKALI YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA ‘DOLA’ KUANZIA JANUARI 1 MWAKA 2018


* WATALII KURUHUSIWA KWA KIBALI MAALUMU


Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Hali ya uchumi na utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/18 ambapo alitoa agizo kwa vyombo vya ulinzi kuwakamata wanaowalazimisha watanzania kufanya malipo kwa Dola badala ya Shilingi, mkutano ulifanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.


Na Said Mwishehe,Blogu ya  Jamii
SERIKALI imepiga marufuku matumizi ya fedha za kigeni ikiwamo ‘dola’ kuanzia Januari 1 mwaka 2018, na kueleza bei zote za huduma na bidhaa zitangazwe kwa Shilingi ya Tanzania.

Akizungumza Dar es Salaam leo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.Philip Mpango wakati anaelezea mwenendo wa hali ya uchumi na utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018.

Dk.Mpango kabla ya kutoa agizo hilo,amefafanua suala la matumizi ya fedha za kigeni sambamba na Shilingi ya Tanzania nchini linasimamiwa na Sheria ya Usimamizi wa fedha za kigeni ya mwaka 1992, sheria ya Benki Kuu ya Tanzania(BoT) ya mwaka 2006, na tamko la Serikali ya mwaka 2007 kuhusu matumizi ya fedha za kigeni kulipia bidhaa na huduma katika soko la ndani.

Amesema matumizi ya fedha za kigeni sambamba na Shilingi ya Tanzania wakati wa kufanya miamala mbalimbali yanaweza kuwa na athari kiuchumi ikiwa pamoja na kudhoofisha thamani ya shilingi.

“Sheria iliyopo kwa sasa haikatazi jambo hili bali inasisitiza sarafu ya Tanzania ndio fedha halali na mtu au taasisi yoyote itakayekataa kuupokea malipo ya shilingi yetu tutachukua hatua za kisheria.

“Hata hivyo suala hili limeendelea kuwa kero kwa wananchi kutokana na ugumu wa kusimamia matakwa ya sheria.Inafahamika kuwa baadhi ya wateja wanapewa kiwango cha thamani  ya kubadilisha fedha ambacho kiko juu kuliko thamani halisi iliyoko kwenye soko,”amesema.

Ameongeza hali hiyo inaumiza zaidi mteja husika. Hivyo suala hilo linahitaji kufanyiwa marekebisho ya sheria.”Ili kukabiliana na hali kero kama hizo wakati utaratibu wa kurekebisha sheria unaendelea ,Serikali inaagiza yafuatayo kuaniza Januari 1,mwaka 2018.”
Kwa mujibu wa Dk.Mpango maagizo hayo ni bei zote nchini kutangazwa kwa Shilingi.Bei hizo zinajumuisha kodi ya nyumba za kuishi na maofisi.

Pia bei ya ardhi, gharama za elimu na afya, bei za vyombo vya usafiri na vifaa vya kieletroniki.

Amesema vyombo vya dola vihakikishe vinasimamia maagizo hayo na watakaoendelea kutoza huduma na bidhaa kwa fedha za kigeni wachukuliwe hatua.

Ameongeza kwa bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni.

“Bei hizo zinajumuisha gharama za usafirishaji kwenda nje ya nchi kupitia Tanzania, gharama za mizigo bandarini kwenda nje ya nchi, gharama za viwanja ndege na visa kwa wageni.

“Na gharama za hotelikwa watalii kutoka nje ya nchi.Hata hivyo walipaji wanaotumia fedha za kigeni watambuliwe kwa vitambulisho vyao kama pasi ya kusafiria na nyaraka za usajili kwa kampuni.

“Viwango vya kubadilisha fedha vitakavyotumika katika kuweka hizo bei katikka sarafu mbili viwekwe wazi na visizidi vile vya soko.

“Ifahamike kuwa ni benki na maduka ya fedha za kigeni tu yanayoruhusiwa  kupanga viwango vya kubadilisha fedha kutokana na ushindani katika soko la fedha za kigeni kupanga viwango vya kubadilisha fedha, amesema Dk.Mpango.

Ametumia nafasi hiyo kueleza mkazi yoyote wa Tanzania asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yeyote hapa nchini kwa fedha za kigeni na vyombo vya dola viwachukulie hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka maagizo hayo ya Serikali.

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII AFANYA ZIARA KATIKA HIFADHI YA SAADANI


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (katikati) akioneshwa ramani ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani na Mwakilishi wa Mkuu wa Hifadhi za Taifa, Vitalis Kuluka huku akishirikiana kuonesha eneo hilo na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo,Erica Yigella ( wa pili kulia) mahali kilipo Kitongoji cha Uvinje ambapo wakazi wa eneo hilo wamegoma kuhama ndani ya hifadhi hiyo na wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea hifadhi hiyo jana. Wa kwanza kulia ni Afisa Wanyamapori, Godfrey Maro na Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Stephano Msumi na pande wa kulia nyuma ya Katibu Tawala ni Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa, Fredrick Mofulu 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ( wa pili kulia ) akizungumza na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani , Stephano Msumi ( katikati) wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea hifadhi hiyo jana kwa ajili ya kujionea changamoto mbalimbali zinazoikabili . Wa kwanza kulia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo, Erica Yigella, Wa kwanza kushoto ni Mwakilishi wa Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Vitalis Kuluka, wa tatu kushoto ni Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa, Fredrick Mofulu 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akizungumza jana na Wananchi wa Kitongoji cha Uvinje ambao wamegoma kuhama ndani ya hifadhi hiyo, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea kwa ajili ya kuzungumza nao ili kujua ukubwa tatizo la mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 10 sasa .
Bango lililopo katika geti la Gama linalokuelekeza sheria na taratibu ukiwa unaingia katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani iliyopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ( kushoto ) akipatiwa maelezo na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani , Stephano Msumi ( katikati) wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea hifadhi hiyo jana kwa ajili ya kujionea changamoto mbalimbali zinazoikabili .Wa kwanza kulia ni Mwakilishi wa Mkuu wa Hifadhi ya Taifa, Vitalis Kuluka, nyuma ya Mhifadhi wa Saadani ni Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa, Fredrick Mofulu
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ( mbele ) akiwa na baadhi ya viongozi wa Hifadhi za Taifa pamoja kamati ya ulinzi na usalama kutoka Wilayani Bagamoyo akiongoza kwenda kuangalia sehemu kunakofanyika utalii wa boti katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea hifadhi hiyo jana kwa ajili ya kujionea changamoto mbalimbali zinazoikabili .
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (wa pili kulia) akipatiwa maelezo na Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa, Fredrick Mofulu ( wali kushoto) kuhusiana na sehemu kunakofanyika utalii wa boti katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani . Wengine ni baadhi ya viongozi wa Hifadhi za Taifa pamoja na kamati ya ulinzi kutoka Wilayani Bagamoyo . 
Picha na Lusungu Helela



Wananchi wa Kitongoji cha Uvinje kilichomo ndani Hifadhi ya Taifa ya Saadani iliyopo wilayani Bagamoyo Mkoani wa Pwani wamesema hawapo tayari kuhama wala kulipwa fidia ili kupisha hifadhi hiyo.

Kitongoji hicho, ambacho ni kati ya vitongoji nane vya Kijiji cha Saadani, kilitakiwa kiondolewe tangu mwaka 2005 baada ya hifadhi hiyo kupandishwa daraja kutoka pori la akiba na kuwa hifadhi kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 281 la Septemba 16, 2005.

Akizungumza mbele ya kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Bagamoyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga wakati alipofanya ziara jana katika kijiji hicho aliwambia wananchi hao kuwa lengo la ziara yake ni kutaka kuwasikiliza juu mgogoro huo na sio kuwahamisha.

‘Mimi ni mgeni kidogo kwenye Wizara hii, Nimekuja kuangalia sio kuwahamisha kwa kuwa sijui eneo hili lina ukubwa kiasi na lina kaya ngapi lakini nimekuja kutembelea hifadhi na maeneo yote yenye changamoto. ‘’ alisema.Alisema amefika kwa ajili ya kuwasikiliza ili aweze kujua jinsi mgogoro ulivyo kwa sababu hakutaka kusikia upande mmoja wa TANAPA pekee.

Naye , Kaimu Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Hassan Akida alisema wakazi wa eneo hilo hawapo tayari kuhama na wala kulipwa fidia kwa vile ni ardhi yao tokea enzi za mababu zao.’‘Tumesema hapa ndo kwetu mnataka kutuhamisha mtupeleke wapi wakati sisi tumezoea maisha yetu hapa’’ alisema Akida.

Aliongeza kuwa kitongoji hicho kimekuwapo kwa muda mrefu na waliishi bila shida hadi pale pori hilo lilipobadilishwa na kuwa Hifadhi ya Taifa.“Wakati hili ni pori la akiba tuliishi vizuri tu na wazazi wetu walikuwa ni wafanyakazi wa pori. Lakini tangu iwe hifadhi imekuwa taabu. Sasa tunafukuzwa wakati tumezaliwa hapa na wazazi wetu wamezikwa hapa hapa,” anasema Hassan Akida. 

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Saadani, Adam Mwandosi alisema mgogoro huo umedumu kwa muda mrefu na umekuwa ukileta chuki kati ya Serikali na wananchi.Amesema wananchi wa eneo hilo muda mwingine wamekuwa wakimuona hata yeye Mwenyekiti wao kama anawasaliti kwa vile tokea mgogoro huo ulipoanza viongozi wengi wamekuwa wakifika hapo lakini wamekuwa hawana majibu ya kumaliza mgogoro huo.

Mhifadhi Mkuu wa Saadani, Stepahano Msumi amesisitiza kuwa kitongoji hicho kimo ndani ya hifadhi kinyume cha sheria.Alisisitiza kuwa sheria za hifadhi za Taifa haziruhusu makazi ya watu ndani yake.

“Kwa ufupi tu ukiangalia GN (Tangazo la Serikali) linaonyesha kuwa eneo lote la kitongoji cha Uvinje liko ndani ya hifadhi. Ni kweli lilikuwa eneo la watu ambao walikuwa watumishi wa pori la akiba tangu lilipoanzishwa mwaka 1968. Waliombwa kuondoka lakini waliendelea kuongezeka,” anasema.

Anasema katika makubaliano, iliamuliwa kuwa walipwe fidia kwa taratibu lakini hata hivyo licha ya kutekeleza utaratibu wa fidia bado wamegoma kuipokea mbali ya wachache kujitokeza.

Ikumbukwe kuwa, Saadani ni hifadhi pekee ya Taifa nchini na Afrika Mashariki yenye fukwe za bahari na inayotazamana na Bahari ya Hindi na fukwe zake zinakutana na uoto wa asili wa nchi kavu.

Inapatikana katika mikoa ya Tanga na Pwani. Uwepo wake ni matokeo ya pori la akiba la Saadani, ranchi ya Mkwaja na sehemu ya kaskazini, sambamba na akiba ya msitu wa asili wa Zaraninge.

MAVUNDE AZITAKA TAASISI BINAFSI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUTATUA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI WATU WENYE ULEMAVU

Naibu waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu kazi,vijana na ajira Anthony Mavunde akimkabidhi fimbo mwenyekiti wa chama cha wasioona mkoa wa Dodoma Omari Lubuva ikiwa ni msaada uliotolewa na Next Generation Microfinance.
Naibu waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu kazi,vijana na ajira Anthony Mavunde akiwa na baadhi ya viongozi wa chama cha wasioona mkoa wa Dodoma na meneja wa Next Generation Microfinance wakijaribu kutumia fimbo zilizotolewa na taasisi hiyo kwa ajili ya watu wasioona mkoa wa Dodoma.
Naibu waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu kazi,vijana na ajira Anthony Mavunde akizungumza wakati wa kukabidhi fimbo kwa ajili ya watu wasioona mjini Dodoma,kushoto kwake ni mwenyekiti wa UWT mkoa wa Dodoma Neema Majule na kulia kwake ni meneja wa Next Generation Microfinance Sospeter Kansapa.
Katibu wa chama cha wasioona(TLB)mkoa wa Dodoma Enock Mbawa akizungumza wakati wa kupokea msaada wa fimbo kwa ajili ya watu wasioona,kushoto kwake ni meneja wa Next Generation Microfinance Sospeter Kansapa na kulia kwake ni mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Dodoma Bill Chidabwa.
Meneja wa Next Generation Microfinance Sospeter Kansapa akizungumza wakati wa kukabidhi fimbo kwa ajili ya watu wasioona mkoa wa Dodoma.
Naibu waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu kazi,vijana na ajira Anthony Mavunde akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa jumuiya za CCM mkoa wa Dodoma na wafanyakazi wa Next Generation Microfinance baada ya kukabidhi fimbo kwa ajili ya watu wasioona wa mkoa wa Dodoma.



……………..

NAIBU waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi,Vijana na Ajira Mh Anthony Mavunde leo amekabidhi msaada wa fimbo za kisasa thelathini (30)kwa ajili ya watu wasioona wa mkoa wa Dodoma huku akitoa rai kwa taasisi binafsi na jamii kuweka utaratibu wa kusaidia makundi yenye mahitaji.

Msaada huo umetolewa na taasisi inayojishughulisha na kutoa huduma ya mikopo(NEXT GENERATION MICROFINANCE).

Akikabidhi msaada huo Mavunde ambaye ni mbunge wa Dodoma mjini ameipongeza taasisi hiyo kwa kutumia faida waliyoipata kusaidia watu wenye mahitaji maalum jambo ambalo linapaswa kuwa chachu kwa taasisi nyingine pia.

“Ndugu zanguni mlichokifanya leo kina maana kubwa sio duniani tu bali hata mbinguni,mmeona ni busara kutumia faida mliyoipata kwa ajili ya kusaidia wenzetu wenye mahitaji badala ya kutumia kufanya party,naomba utaratibu huu usiishie leo tu bali muendelee kugusa na makundi mengine yenye uhitaji,”alisema Mavunde.

Katika kusaidia makundi hayo ameiomba pia taasisi hiyo kusaidia chama cha waandishi wa habari wa mkoa wa Dodoma ili waweze kuwa na ofisi yao inayoendana na hadhi ya makao makuu.Ametoa rai pia kwa viongozi wa chama cha wasioona mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanagawa fimbo hizo kwa walengwa bila ya upendeleo wowote.

Akitoa neno la shukrani baada ya kupokea msaada huo katibu wa chama cha wasioona(TLB)mkoa wa Dodoma Enock Mbawa ameishukuru taasisi hiyo kwa kusaidia serikali kupunguza changamoto walizonazo na kuahidi kuhakikisha fimbo hizo zinafika kwa walengwa waliokusudiwa.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi meneja wa Next Generation Microfinance Sospeter Kansapa amesema wameamua kuitikia wito wa rais John Magufuli wa kuwataka wadau wa maendeleo kote nchini kujitokeza kutoa mchango katika ustawi wa Taifa wakiamini kuwa fimbo hizo zitakuwa chachu katika kuleta maendeleo ya Taifa.