Sunday 29 May 2016

UVUVI BABATI



Vijana wa mjini Babati Mkoani Manyara, wakivua samaki kwenye mitaro ya mitaani baada ya ziwa Babati kujaa maji na kusababisha wingi wa samaki kwenye mitaro hiyo


Saturday 28 May 2016

OLE MILLYA KUANZISHA KAMATI YA MAENDELEO SIMANJIRO



Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya amesema ataanzisha kamati ya wadau wa maendeleo ya Simanjiro, itakayoongozwa na aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Singida Parseko Kone. 

Ole Millya alisema hawezi kuwaweka kando wasomi wa wilaya hiyo, hivyo atawakumbatia kwani Simanjiro haiwezi kuendelea bila ushirikiano wa wadau mbalimbali wenye maono ya kuifikisha mbali.

Alisema ameshapata msaidizi wake, Joshua Kuney ambaye ni katibu wa mbunge hivyo kilichobakia ni kuhakikisha timu hiyo inakutana mara moja kwa kushirikiana na wazee wa mila watafanikisha maendeleo.



Diwani wa kata ya Naberera Haiyo Mamasita, alisema hivi sasa uchaguzi umeshapita hivyo kinachotakiwa ni kuhakikisha maendeleo ya wananchi yanapatikana ikiwemo huduma muhimu za kijamii za maji, elimu na afya.

“Changamoto kubwa iliyopo hivi sasa ni kuhakikisha suala zima la elimu linafanikiwa kwenye kata yetu ya Naberera na nitahakikisha wanafunzi waliokuwa wanakosa hiyo fursa wanafanikiwa,” alisema Mamasita.



Ole Millya alisema miongoni mwa wadau wa maendeleo na wasomi watakaokuwa kwenye kamati hiyo ambayo haitajadi itikadi za kisiasa ni mkuu wa wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma Peter Toima na Katibu wa Chadema Simanjiro Frank Oleleshwa.

“Siwezi kuwakataa wasomi wa Simanjiro kwani tutashirikiana nao tupate maendeleo, nataka mwisho wa siku ikifika uchaguzi kama kunipa mnipe ninyi wenyewe na kama kuninyima mninyime wenyewe,” alisema Ole Millya. 

Alisema huwezi kufanikiwa maendeleo ya wananchi wa Simanjiro ili hali unaogopa kushirikiana na wasomi, kwani japokuwa wengine wapo nje ya eneo hilo lakini kupitia ushirikiano waliouanzisha watafanikisha mambo mengi.

SIMANJIRO WAASWA KUTUMIA MBOLEA



Wakulima wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wametakiwa kubadilika kwa kulima kitaalamu ikiwemo kutumia mbegu bora na mbolea za kupandia na kukuzia ili kuondokana na dhana potofu kuwa mbolea inafubaza ardhi.

Ofisa kilimo na umwagiliaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Claudy Losiock akizungumza mbele ya mkuu wa wilaya Mahmoud Kambona na madiwani waliofika shambani kwake, alisema ameamua kuandaa shamba hilo ili atoe somo.

Losiock alisema kupitia shamba darasa hilo la kwake viongozi na wananchi watajifunza na kuwaelimisha wakulima wengine faida ya kulima kitaalamu kwa kutumia mbegu bora, mbolea za kupandia na kukuzia.

Alisema kwa sababu ya taaluma yake ameandaa shamba lake lenye ukubwa wa ekari nne na akalima zao la mahindi kwa ajili ya mafunzo kwa wakulima wa eneo hilo ili wafahamu faida ya kulima na kutumia mbolea na mbegu bora.   



Akizungumza kwenye shamba hilo, mkuu wa wilaya hiyo Kambona alisema ni vizuri viongozi wa kisiasa wenye ushawishi mkubwa kwa jamii za kifugaji kupata somo hilo la kilimo bora ili wakatoe elimu kwa wapiga kura wao nao waige.

“Dhana potofu ya kuwa mbolea zinaharibu ardhi hivi sasa zimepitwa na wakati kwani wakulima bora hulima kitaalamu kwa kuwatumia maofisa ugani wanaowaelimisha na kupata mazao mengi na yenye tija,” alisema Kambona.

Diwani wa kata ya Terrati Jackson Ole Materi, alisema kupitia shamba darasa la Losiock, naye amepata somo zuri kwa ajili ya kuwaeleza wakulima wa eneo lake na yeye atatumia shamba lake kwa ajili ya kulima mahindi kitaalamu zaidi.

“Kazi ya kilimo ni nzuri na endapo utafuata vigezo utafanikiwa kupata mazao bora kwani kuna baadhi ya watu wanalima kwa mazoea ekari 20 na kupata mavuno sawa sawa na yule aliyelima ekari 10 kitaalamu,” alisema Ole Materi.



Diwani wa kata ya Naberera Haiyo Mamasita, alisema atawachukua baadhi ya wakulima wa eneo lake kwa ajili ya kufika kaya ya Orkesumet lilipo shamba hilo ili wajionee ubora ulivyo na kupata funzo ya shamba darasa hilo la ofisa kilimo.

“Tumezoea kuona baadhi ya watu wanakuwa na taaluma fulani lakini hawana matokeo mazuri kwenye uhalisia, kwani kuna mafundi seremala hawana hata stuli lakini huyu ofisa kilimo ana shamba darasa zuri,” alisema Mamasita.