Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
watu wenye ulemavu) Jenista Mhagama amewataka wakazi wa mji mdogo wa
Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kukitumia ipasavyo kituo cha huduma
za ukimwi ili kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi (VVU).
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro mhandisi
Zephania Chaula akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo Alexander Mnyeti
alisema bado maambukizi ya VVU yapo chini kwa Manyara.
Mhagama aliyasema hayo mji mdogo wa
Mirerani wakati akiweka jiwe la msingi wa kituo cha huduma za ukimwi
kitakachotoa huduma kwa zaidi ya watu 49,000.
Alisema wananchi wa eneo hilo na wilaya za jirani na Mirerani wanapaswa kutumia huduma zitakazotolewa na kituo hicho ili kuhakikisha hakutakuwepo na maambukizi mapya ya VVU.
Alisema serikali imeonelea kuwa ni vyema kujenga kituo hicho cha huduma za Ukimwi kutokana na kasi ya maambukizi ya VVU kwani ni eneo ambalo linaongoza hivyo kuwa tishio japo mkoa huo una asilimia ndogo ya maambukizi.
Aliwataka viongozi na wananchi wa
eneo hilo kubadilisha kwa kukitumia kituo hicho cha huduma za Ukimwi ili miaka
ijayo kuwe na mabadiliko makubwa ya VVU pindi upimaji ukifanyika upya.
"Wanaume msiwaache wanawake
wenyewe wapime kwani mnapaswa kupima wote ili mtambue afya zenu zikoje ili kama
kuna aliyeambukizwa aanze kupata ushauri na kutumia dawa," alisema
Mhagama.
Mhandisi Chaula alisema hali ya
maambukizi kwa mkoa huo ni asilimia 2.3 ambapo halmashauri ya mji wa Mbulu
maambukizi yapo chini kwa asilimia 0.64 na wilaya ya Simanjiro inaongoza kwa
asilimia 2.85.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya
wilaya ya Simanjiro Yefred alisema hadi jengo hilo la kituo cha huduma za
ukimwi linalojengwa na wataalamu wa Suma JKT litakapokamilika litagharimu kiasi
cha sh492.5 milioni.
Myenzi alisema awamu ya kwanza ya
ujenzi wa kituo hicho, halmashauri ya wilaya imechangia sh51.5 milioni kutokana
na mapato ya ndani na kinatarajiwa kukamilika Juni 22 mwaka 2018.
Alisema wilaya imeweka uzito wa
kipekee kwenye maeneo hatarishi ikiwemo mji mdogo wa Mirerani uliokuwa na
asilimia 16 ya maambukizi ya VVU mwaka 2015 ila hadi Desemba 2017 imeshuka hadi
asilimia 6.4.
"Mikakati inayotumika Mirerani
ili kupunguza maambukizi mapya ni kuendelea na uhamasishaji wa jamii kwa
kutumia washauri rika na wataalamu wa idara ya afya, kugawa mipira ya kiume ya
kujikinga, upigaji na utoaji wa dawa za kufubaza VVU," alisema Myenzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya
kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dk Leonard Maboko alisema mradi huo umetokana na
jitihada za pamoja kati ya TACAIDS, uongozi wa mkoa wa Manyara na wilaya ya
Simanjiro.
Dk Maboko alisema alifanya ziara mji
mdogo wa Mirerani Desemba 19 mwaka 2016 na kubaini kasi ya maambukizi ya VVU
ilikuwa juu kutokana na shughuli mchanganyiko za kiuchumi na mwingiliano wa
watu.
Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani,
Jafari Matimbwa alisema kituo hicho kitakuwa msaada mkubwa kwa jamii ya eneo
hilo ambayo hivi sasa elimu ya maambukizi ya VVU inatolewa ipasavyo.
Matimbwa alisema kutokana na kutolewa
kwa elimu hiyo wananchi wengi wanatambua namna ya kujikinga na maambukizi mapya
na umuhimu wa kupima afya zao tofauti na awali.
No comments:
Post a Comment