Tuesday, 22 May 2018

WATUMISHI MBULU KUFANYA MAZOEZI KILA MWISHO WA WIKI

 Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara wamejipanga na utaratibu wa kufanya mazoezi kila mwisho wa wiki kwa lengo la kuimarisha afya ya mwili, akili, moyo na kupambana na magonjwa yasiyoambukizwa ikiwemo shinikizo la damu, kisukari na magonjwa ya moyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Hudson Kamoga akizungumza wakati wa kufanya mazoezi hayo mji mdogo wa Haydom, alisema wameanzisha utaratibu huo wa kufanya mazoezi kila mwisho wa wiki badala ya mara moja kwa mwezi ili waweze kuimarisha afya zao.

 Kamoga alisema kupitia mazoezi wanayofanya watumishi hao, hata ari ya kufanya kazi huongezeka zaidi kwani mwili na akili huwa  zinashirikiana ipasavyo.

Alisema binadamu bila kuwa na afya bora hawezi kufanya jambo lolote la maana zaidi ya kuitwa mgonjwa hivyo waepuke hayo kwa kufanya mazoezi kila mwisho wa wiki.

"Sisi watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, tunamuunga mkono Makamu ya Rais mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa agizo lake kufanya mazoezi kila mwisho wa mwezi Kwan kushiriki kila wiki," alisema Kamoga.

Mkurugenzi wa hospitali ya rufaa ya Haydom Dk Emmanuel Nuwass alisema mazoezi ni jambo jema kwa binadamu ambaye anatakiwa kufanya mazoezi nusu saa kwa kila siku.

Dk Nuwass alisema kupitia mazoezi, binadamu huwa na amani moyoni na kuepukana na hasira, msongo wa mawazo na damu kupita kwenye mishipa ya mwili ipasavyo.


Ofisa mtendaji wa kijiji cha Harara, Bertila Mwinuka alisema kufanya mazoezi husababisha kuimarisha mwili na kuongeza upendo na umoja.


No comments:

Post a Comment