Monday 29 January 2018

ZIARA YA RC MNYETI WILAYANI SIMANJIRO

 Mkuu wa Mkoa Manyara Alexander Mnyeti (mwenye shati la maua) akiangalia mawe yaliyopo eneo la ujenzi wa nyumba ya walimu wa shule ya sekondari Emboreet Wilayani Simanjiro, ambayo ni pekee yenye kidato cha sita, inayojengwa na shirika la ECLAT Foundation na kuwasaidia wanafunzi wa eneo hilo hasa kutoka kwenye jamii ya kifugaji.
 Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti akizungumza na wananchi wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro alipotembelea kituo cha afya Mirerani na kubaini changamoto ya upungufu wa watumishi na uchache wa dawa.
 Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akichoma zana haramu ikiwemo vyandarua, vyavu mlazo, mperampera na makokoro zinazotumika kwenye uvuvi haramu bwawa la Nyumba ya Mungu, kwenye Kijiji cha Magadini, Wilayani Simanjiro.
 Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti akiweka jiwe la msingi kwenye kiwanda cha madini ya Grafite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro, ambayo yatatumika kutengeneza kurunzi. 
Askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wanaojenga ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakichapia ukuta huo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa huo Alexander Mnyeti.  
 Wananchi wa Mji mdogo wa Orkesumet Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakitoa kero kwa Mkuu wa Mkoa huo Alexander Pastory Mnyeti. 


Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na wananchi wa mji mdogo wa Orkesumet Wilayani Simanjiro.
 Wananchi wanne wa Kijiji cha Terrat Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakiwa kwenye gari la polisi baada ya Mkuu wa Mkoa huo Alexander Mnyeti, kuagiza wakamatwe kwa kudaiwa kusababisha migogoro ya Kijiji hicho
 Wananchi wa Kijiji cha Terrat Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakiwa na mabango, yanayoonyesha changamoto na kero walizonazo wakati wa kumpokea Mkuu wa Mkoa huo Alexander Mnyeti. 
 Wananchi wanne wa Kijiji cha Terrat Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakiwa kwenye gari la polisi baada ya Mkuu wa Mkoa huo Alexander Mnyeti, kuagiza wakamatwe kwa kudaiwa kusababisha migogoro ya Kijiji hicho
 Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Terrat Wilayani Simanjiro, ambapo aliwatangazia kuunda tume ya kuchunguza migogoro ya ardhi ya eneo hilo.
 Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akizindua ujenzi wa nyumba ya walimu wa shule ya sekondari ya kidato cha sita ya Emboreet Wilayani Simanjiro, kwa kulima na jembe katika msingi wa nyumba hiyo, ambayo inajengwa kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikalli la ECTAL Foundation.  
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Terrat Wilayani Simanjiro, wakiwa na mabango, yanayoonyesha changamoto na kero walizonazo. 
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akimsikiliza Mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali la ECLAT Foundation alipokuwa akizungumza juu ya maendeleo ya chuo cha ufundi (Veta) kilichojengwa na shirika hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti baada ya kupewa zawadi ya nguo ya jadi na wafugaji wa kata ya Naisinyai kwenye ziara yake Wilayani Simanjiro, kulia ni Mkuu wa wilaya hiyo mhandisi Zephania Chaula na kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Jackson Leskar Sipitieck na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo Arnold Msuya.
Siku ya kwanza ya ziara ya siku saba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti, kwenye Wilaya ya Simanjiro.

HALMASHAURI YA WILAYA YA MBULU YAPITISHA MPANGO WA BAJETI WA SHILINGI BILIONI 43.983

 Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, limepitisha shilingi bilioni 43.983 za mapendekezo ya mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga, akizungumza baada ya kupitishwa bajeti hiyo, alisema vipaumbele vyake ni elimu, afya, maji, kilimo na mifugo.

Kamoga alisema bajeti hiyo imezingatia vipaumbele vya vijiji, kata, halmashauri, mkoa, mpango wa pili wa maendeleo ya Taifa na dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025. 
 Alisema vipaumbele vingine ni mikakati na sera mbalimbali za kisekta, maelekezo mbalimbali ya viongozi wakuu wa kitaifa, na ahadi ya Rais John Magufuli alizozitoa wakati wa kampeni wilayani Mbulu.

Alisema halmashauri hiyo imejikita katika kuongeza mapato ya ndani kwa kuimarisha vyanzo vilivyopo, kubuni vyanzo vipya na kuimarisha mfumo wa kielectroniki. 
"Halmashauri imejikita katika mpango bora wa matumizi ya ardhi kwa makazi, biashara, viwanda vidogo, maeneo ya malisho ya mifugo, kilimo, hifadhi ya mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji," alisema Kamoga.

Mbunge wa jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Massay alipongeza kupitishwa kwa bajeti hiyo ambayo imekidhi kuondoa changamoto mbalimbali.

Massay alisema bajeti hiyo imegusa sekta mbalimbali ikiwemo elimu ya msingi, sekondari, kilimo, mifugo, ushirika, umwagiliaji, afya na maji.

Alisema anatarajia wananchi wa jimbo hilo watapiga hatua kubwa ya maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi ya mpango wa bajeti iliyopishwa na madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo.

Mwanasheria wa halmashauri hiyo, Honoratus Mulokozi alisema bajeti hiyo kabla ya kupitishwa imezingatia sheria namba 9 ya serikali za mitaa ya mwaka 1982.

Mulokozi alisema sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho Januari mosi mwaka 2000 inayotaka kufuata sheria, kanuni na taratibu, wakati wa kuandaa bajeti.