Mashindano ya Kurugenzi CUP ’18 yaliyoandaliwa
na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson
Kamoga yameendelea kutimua vumbi leo Mei 16 kwenye viwanja vya shule ya msingi
Haydom kwa timu ya soka ya Young Boys kuifunga mabao 6-0 timu ya Qandach FC.
Mabao ya Young Boys yalifungwa na Chunga Elia kwenye
dakika ya 9 kwa shuti kali ndani ya eneo la hatari na kumshinda mlinda mlango
wa timu ya Qandach FC Israel Petro.
Bao la pili la Young FC lilifunga na Enea Sule
kwenye dakika ya 24 kwa kichwa baada ya kupokea krosi kali iliyopigwa kiufundi
na winga wao Shondo Silvin aliyevaa jezi nambari 5 mgongoni.
Yule yule mfungaji wa bao la kwanza Chunga Elia
mnamo dakika ya 30 aliwainua mashabiki wa timu ya Young Boys ambao walijaa
kwenye uwanja huo wa shule ya msingi Haydom licha ya mvua kali kuendelea
kunyesha kwa kufunga kwa shuti kali la umbali wa mita 25 na kuandika bao la
tatu.
Mchezaji kiungo mkabaji Yoram Thomas wa timu
ya Young Boys aliipatia timu yake bao la 4 mnamo dakika ya 49 ya kipindi cha
pili kwa kufunga baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa timu ya Qandach FC.
Bao la
5 la Young Boys lilifungwa na mchezaji wao machachari Elmalek Malley aliyeingia
kuchukua nafasi ya Yoram Thomas kwa shuti kali baada ya kupewa pasi safi na
mchezaji Zacharia Simon (Dokta) kwenye dakika ya 78 ya mchezo huo.
Chunga Elia alihitimisha karamu ya mabao kwa timu
hiyo kwa kufunga bao la kiufundi la sita baada ya kuwachambua walinzi wa timu pinzani
na kuachia shuti kali lililomshinda kipa na kuzama kwenye nyavu ndogo ambapo
hadi mwisho wa mchezo huo Young Boys waliibuka kidedea kwa mvua ya magoli 6 na
Qandach 0.
No comments:
Post a Comment