HABARI ZA KITAIFA

5 comments:

  1. MKAZI wa Mji mdogo wa Mirerani Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara Zahari Mussa amesema Katiba mpya ipige marufuku mbio za mwenge hapa nchini kwani unatumia gharama kubwa kukimbizwa huku ukifungua miradi michache.

    Akizungumza mbele ya wajumbe wa Tume ya mabadiliko ya Katiba Mussa alisema mwenge wa uhuru hauna faida unatakiwa uwekwe makumbusho ya Taifa kwani umekuwa mzigo kwa kuchangiwa na watanzania kila mara.

    “Haiingii akilimi mwenge wa uhuru kutumia zaidi ya sh80 milioni kisha uweke jiwe la msingi au uzindue zahanati yenye thamani ya sh20 milioni kwa kweli maana halisi ya mwenge haipo hivi sasa bora uwekwe makumbusho tu,” alisema Mussa.

    Alisema mwenge huo ulikuwa na tija enzi za Mwalimu Julius Nyerere lakini hivi sasa shabaha yake imepitwa na wakati suluhisho lake ni kuwekwa makumbusho kwa faida ya vizazi vijavyo.

    “Tangu mimi nasoma shule ya msingi hadi sasa nina familia mwenge wa uhuru bado upo tu unakimbizwa sehemu mbalimbali hapa nchini hauna faida yoyote kwa jamii napendekeza katiba ijayo iupige marufuku,” alisema Mussa.

    Kwa upande wake,Paulo Sumary alisema Katiba mpya itamke kuwa Rais akiingia madarakani inatakiwa atangaze mali zake ili anapomaliza muda wake watanzania wapate kuelewa Rais wao amechuma mali kwa kiasi gani.

    “Hii itaongeza uadilifu kwa nafasi ya Urais na endapo atabainika kuwa wakati wa utawala wake amehujumu mali ya wananchi anyongwe kama ilivyo China ambapo kuna uadilifu wa hali ya juu,” alisema Sumary.

    MWISHO.

    ReplyDelete
  2. JESHI la Polisi Mkoani Manyara linawashikilia watu tisa wakazi wa mkoa huo kwa kudaiwa kukutwa na bunduki mbili,risasi na maganda ya risasi wakihisiwa majangili wa tembo hifadhi ya Tarangire na wengine wakikamatwa na bangi,mirungi na gongo.

    Akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati leo,Kamanda wa polisi mkoani Manyara Kamishna Msaidizi Akili Mpwapwa alisema watu hao walikamtwa kwenye msako ulioendeshwa na polisi hivi mwishoni mwa mwezi uliopita.

    Kamanda Mpwapwa aliwataja watuhumiwa wa ujangili ni Paulo Issa,Hamis Fidamrisi Diau na Salimu Mohamed wakazi wa mjini Babati ambao walikamatwa na bunduki aina ya Rifle 458 namba 59477,risasi sita,maganda mawili na risasi ndogo mbili hazijafahamika za bunduki gani.

    Alisema watuhumiwa wawili walikamatwa kwenye barabara kuuu ya Babati-Arusha na mtuhumiwa mwingine Giau alikamatwa eneo la Mdori akiwa na bunduki aina ya Rifle 458 namba 987660 ambayo alikiri kutumia kuwindia tembo.

    “Mara baada ya kufanya mahojiano na watuhumiwa hao walikiri kuwa wao ni kweli ni majangili na walikuwa safarini kwenda kuwinda tembo katika hifadhi ya Tarangire kupitia Galapo ,” alisema Kamanda Mpwapwa.

    Kamanda Mlpwapwa alisema pia watuhumiwa wa makosa mbalimbali wamekamatwa kwakukuhusika na matukio ya uhalifu kama kupatikana na kwa bangi,mirungi,gongo na makosa ya usalama barabarani.

    Alisema pia katika msako endelevu wa kuvuia uhalifu uliofanywa na polisi watu sita wanawashikilia ambapo waliokamatwa na kilo 27 za bangi,kilo 160 za mirungi na lita 1713 ya pombe haramu ya gongo.

    Alisema udhibiti wa makosa ya usalama barabarani jumla ya makosa yaliyokamatwa ni 519,makosa ya ubovu wa vyombo vya usafiri 85,makosa mengineyo 434 na sh15.5 milioni zilikusanywa kutokana na faini ya papo kwa hapo.

    Alisema jeshi la polisi limefanikisha zoezi zima la msako na kudhibiti makosa ya usalama barabarani kwa mwezi Julai kutokana na mahusiano mazuri na raia wema kupitia dhana ya ulinzi shirikishi na polisi jamii.

    Kamanda Mpwapwa alisema kwamba ili kupambana na uhalifu jeshila polisi mkoani Manyara litaendelea kufanya msako na kuimarisha doria katika maeneo mbalimbali ndani ya mkoa huo.

    MWISHO.

    ReplyDelete
  3. WATU wawili wa ndugu wa familia moja wamefariki dunia Mkoani Manyara baada ya kutokea ajali ya gari walilokuwa wamelipanda kupinduka kutokana na kuacha njia kwenye barabara kuu ya Arusha-Babati.

    Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo,Kamanda wa polisi mkoani Manyara Akili Mpwapwa alisema ajali hiyo ilitokea juzi kwenye eneo la kijiji cha Mdori Kata ya Nkaiti wilaya ya Babati.

    Kamanda Mpwapwa aliwataja ndugu hao waliofariki ni dereva wa gari hilo Valentine Kimei (27) mkazi wa mjini Arusha ambaye ni mtumishi wa idara ya uhamiaji na Felix Kimei (35) mfanyakazi wa hoteli moja mjini Arusha.

    Alisema Valentine alikuwa anaendesha gari aina ya Toyota Mark II yenye namba za usajili T 324 ACW na chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi uliosababishwa na dereva huyo na ambaye alifariki dunia papo hapo baada ya gari kupinduka.

    “Baada ya ajali hiyo Felix alipata majeraha na kukimbizwa hospitali ya mji wa Babati Mrara na hali yake ilipobainika ni mbaya alikimbizwa hospitali ya rufaa ya KCMC mjini Moshi na akafariki dunia kesho yake,”alisema Kamanda Mpwapwa.

    Kamanda Mpwapwa alisema jeshi lake linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na miili ya marehemu hao imehifadhiwa kwenye hospitali ya rufaa ya KCMC kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

    Aliwataka madereva wanaotumia barabara kuu ya Arusha-Minjingu kuwa makini na kuendesha kwa umakini pindi wanapoitumia barabara hiyo kwani inaendelea kutengenezwa kutokana na kuwa na mashimo.

    MWISHO.

    ReplyDelete
  4. MAPIGANO ya wafugaji na wakulima yamezuka Wilayani Kiteto Mkoani Manyara ambapo mkulima mmoja amefariki dunia kwa kuuawa na wafugaji huku wakulima wengine sita wakijeruhiwa vibaya.

    Wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi,baadhi ya wakazi wa Kata ya Bwagamoyo mjini Kibaya wameeleza kuwa mapigano hayo yalitokea jana saa 9 usiku baada ya wakulima kukamata mifugo iliyoingia mashambani mwao na kuharibu mazao.

    Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara,Kamishna Msaidizi,Akili Mpwapwa alithibitisha kutokea kwa mapigano hayo na kumtaja mkulima huyo aliyefariki kuwa ni Daudi Mtakama (18) mkazi wa kitongoji cha Pori kwa pori,kijiji cha Kimana.

    Kamanda Mpwapwa aliwataja wakulima waliojeruhiwa na wafugaji ni Jonas Mazengo,Njile Alfred,Msafiri Songo,Farida Abasi,Msumari Gorida na Aonezi Charles wote wakazi wa kijiji hicho cha Kimana.

    Alisema mwili wa marehemu huyo umehifadhiwa hospitali ya wilaya ya Kiteto na majeruhi hao pia wamelazwa kwenye hospitali hiyo na mmoja wao alisafirishwa kwenye hospitali ya rufaa ya KCMC iliyopo mkoani Kilimanjaro.

    “Chanzo cha mapigano hayo ni kundi la ng’ombe wa wafugaji kuingia shambani kwa mkulima mmoja lililokuwa na mazao ya mbaazi na mahindi na mifugo hiyo ikala mazao hayo ndipo wakulima wakaikamata,” alisema Kamanda Mpwapwa.

    Alisema baada ya wakulima kuikamata mifugo hiyo kwa matarajio ya wamiliki wake kujitokeza ili wazungumze kuhusu fidia ya uharibifu wa mazao yao usiku wafugaji wakawavamia kwa kutumia silaha na ndipo mkulima huyo akauawa.

    “Uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba marehemu huyo aliuawa baada ya kuchomwa na kitu chenye nja kali tumboni kwani wafugaji hao walikuwa na silaha za jadi ikiwemo sime,mikuki,fimbo na marungu,” alisema Kamanda Mpwapwa.

    Hata hivyo,alisema wafugaji hao walikuwa na silaha za moto kwani milio ya kutumiwa kwa bunduki ilisikika hewani wakati wa mapigano hayo lakini polisi wahakufanikiwa kupata ganda la risasi iliyotumika ili kubaini silaha hizo.

    Kwa upande wake,Diwani wa kata ya Bwagamoyo,Yahaya Masumbuko alisema tukio hilo liliwapata wakazi wake kwenye kata ya Partimbo ila baada ya wafugaji hao kufanya tukio hilo walitoroka.

    Alisema ameshangazwa na hatua iliyochukuliwa na wafugaji hao kwani mara nyingi wafugaji na wakulima ni watu wanaoishi kwa ushirikiano siku zote hivyo ameshangazwa na tukio hilo la kushambuliwa kwa wakulima.

    Mkuu wa wilaya hiyo,Matha Umbulla,akizungumza na Mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu alisema baada ya kutoka bungeni Dodoma ndiyo ameingia wilayani humo jana hivyo baada ya kutembelea eneo hilo ndipo atatoa tamko lake kuhusu tukio hilo.

    MWISHO.

    ReplyDelete
  5. WAKAZI wa Mji mdogo wa Mirerani Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara walio na nyumba pembeni ya barabara ya Kia-Mirerani zimewekwa alama ya X na wakala wa barabara nchini (Tanroads) mkoani humo wameazimia kuifikisha Serikali Mahakamani kutokana na kutowafahamisha namna ya kuwalipa fidia hasa wakati huu barabara hiyo inapotarajiwa kujengwa.



    Katika kuunga mkono kwenda Mahakamani watu 77 kati ya 97 waliohudhuria kikao hicho walichangia sh1.5 milioni kwa ajili ya kuwasilisha kisheria suala hilo kupitia kwa wakili wao ambapo gharama ya awali imebainika ni sh800,000.



    Akizungumza juzi mjini humo Mwenyekiti wa kamati ya watu waliowekewa alama ya X kwenye mali zao Nobert Olomi alisema wakili wao anatarajia kuandika barua ya kusudio la kuishtaki Serikali kupitia halmashauri ya wilaya ya Simanjiro na Tanroads mkoa wa Manyara.



    Olomi alisema hawapingi maendeleo ya ujenzi wa barabara ila wanachopinga ni kutobainishwa haki zao za msingi kwani barabara hiyo imepandishwa hadhi na kuwa ya wilaya na mkoa wakati wao walishajenga hivyo barabara hiyo imewakuta wao.



    Alisema Serikali kupitia mkuu wa mkoa huo Elaston Mbwilo na Meneja wa Tanroads mkoa huo Yohani Kasaini walipokutana nao Septemba mwaka jana walipewa mapendekezo matatu ambayo bado hayajatekelezwa hadi sasa.



    “Walipendekeza kuwa watatulipa fidia au kuangalia uwezekano wa barabara kupita nje ya mji au barabara hiyo kutengenezwa bila kubomoa mali yoyote lakini hadi sasa hakuna jibu na sisi hatuwezi kukaa kimya,” alisema Olomi.



    Alisema kila barua waliyoandika walisisitiza kupatiwa majibu kwa njia ya maandishi lakini hawakupatiwa majibu yoyote na zaidi mbunge wa Jimbo hilo Christopher Ole Sendeka ambaye walitarajia angewatetea amekaa kimya bila kuwasemea chochote.



    Naye,Mwenyekiti wa mtaa wa Songambele A,Ombeni Charles alisema alimsikia Meneja wa Tanroads mkoa wa Manyara Yohane Kasaini akisema watalipa fidia kuanzia mita 15 kutoka barabarani na kuacha mita 7.5 zilipwe na halmashauri ya wilaya ya Simanjiro.



    “Serikali inatakiwa kulichukulia jambo hili kwa umakini mkubwa na isilifanye suala la kisiasa kwani watu wanadai haki zao na wanatakiwa kupatiwa haki hiyo kwani barabara ndiyo imewakuta,wao hawakujenga barabarani,” alisema Charles.



    Kwa upande wake,mmoja kati ya waathirika wa tatizo hilo John Ninie alisema nyumba zao zimewekewa alama ya X bila wao kupewa taarifa wala kushirikishwa na wataweka wakili ili wapate haki zao.



    “Hatuwezi kukubali hali hii ni bora twende kwenye vyombo vya sheria ili tujue kuwa tunapata haki zetu au tunakosa kuliko kusubiri na kukaa kimya wakati mali zetu zitabomolewa huku tukiangalia,” alisema Ninie.



    MWISHO.

    ReplyDelete