Wednesday 5 July 2017

LOIBORSOIT A WAMUOMBA RAIS JOHN MAGUFULI WAWARUDISHIE ARDHI



Wakazi wa Kijiji cha Loiborsoit A, Kata ya Emboreet Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamemuomba Rais John Magufuli kumwagiza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi William Lukuvi awanyan'ganye  vigogo waliojimilikisha bila uhalali wa zaidi ya ekari 26,164.5 za mashamba pori ya kijiji hicho ilihali wananchi wengi wa eneo hilo wamekosa hata ekari moja ya shamba kwa ajili ya kulima. 

Inadaiwa kuwa, baadhi ya vigogo na kiongozi mmoja wa wilaya hiyo wa chama cha kisiasa wamejimilikisha ardhi kwa kugushi nyaraka na kumiliki ekari 8,000 mwingine ekari 6,000 na mwingine ekari 4,000 huku vijana wengi wa eneo hilo wakikosa sehemu za kujishughulisha kwa kilimo. 

Akisoma risala kwenye sherehe za kimila za jamii ya wamasai wakati wa kusimikwa kuwa wazee na kuvuka rika la Irkiponi, mmoja kati ya wakazi hao Haiyo Mosson alisema watu hao walipora ardhi yao na kujimilikisha bila kuiendeleza. 

Mosson alisema wanamuombea Rais Magufuli kumwagiza Waziri Lukuvi afike katika eneo hilo kwa ajili ya kuyarudisha mashamba hayo ya wananchi yaliyoporwa na wajanja wachache wenye tamaa ya ardhi.

Alisema watu hao walijimilikisha na kujiongezea ukubwa wa mashamba pori hayo huku wakilindwa kupitia nyadhifa zao na watawala wachache wanaowaunga mkono. 

"Wakati wa ujana wetu tulijaribu kuyarudisha mashamba pori tukishirikiana na serikali ya kijiji japo hatukufanikiwa kwa asilimia kubwa hivyo tunawasihi vijana wa rika ambalo tunawakabidhi madaraka rasmi leo hii wajitahidi kuyaenzi na kuyaendeleza yote tuliyoyapigania," alisema Masson.



Mmoja kati ya waliosimikwa kuwa wazee kwenye sherehe hiyo, Lee Shinini alisema wananchi wanatambua kuwa suluhishho la tatizo hilo ni kauli ya Rais Magufuli ndiyo itakayonusuru ardhi yao kuporwa hivyo wanamuomba atengue umiliki wa vigogo hao waliopora ardhi ya wananchi. 

"Tuliona kule Bagamoyo mkoani Pwani hivi karibuni Rais Magufuli aliwarudishia wananchi ardhi yao waliyokuwa wanaililia kwa muda mrefu na kupitia fursa hiyo tunaomba atutimizie na sisi wananchi wa kijiji cha Loiborsoit A," alisema Shinini.

Alisema baadhi ya vigogo hao walitumia nafasi ya vyeo na madaraka yao, kuwapora ardhi wananchi wanyonge wa eneo hilo lakini wanatambua suala hilo litahitimishwa kwa kuwanyang'anya na kuwarudishia wananchi wa Kijiji cha Loiborsoit A. 


Diwani wa kata ya Emboreet Christopher Ole Kuya alisema ana imani kubwa na serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli kuwa ni sikivu hivyo suala hilo litatekelezwa na hatimaye wananchi wa eneo hilo kupatiwa ardhi yao. 

"Kauli mbiu yake ya hapa kazi tuu itashindwa kutekelezwa na vijana kwa sababu ya masetla wachache waliopora ekari 26,164.5 na kuwakosesha eneo la kulimia nguvu kazi ya Taifa wanaotegemea kunyanyua maisha yao kupitia kilimo," alisema Ole Kuya. 

Alisema kijiji cha Loiborsoit A ni kidogo lakini vigogo hao wamejimilikisha ardhi hiyo ila kupitia Rais Magufuli, wananchi wataweza kurudishwa maeneo yao na kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo yao na jamii nzima kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment