Tuesday, 11 July 2017

WACHIMBAJI WA MADINI YA TANZANITE WAISUBIRI KWA HAMU TUME YA SPIKAWachimbaji madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wanaisubiri kwa hamu kamati ya wabunge tisa itakayochunguza sekta nzima ya madini ya Tanzanite.

Wachimbaji hao walidai kuwa wana imani kamati hiyo iliyoundwa mwezi uliopita na spika wa bunge Job Ndugai kwenye bunge la bajeti, itatoa majibu ya matatizo yao.

Mmoja kati ya wachimbaji hao Hassan Juma alisema kwa muda mrefu kumekuwa na tatizo la mgogoro wa wachimbaji wadogo na wakubwa ila kupitia kamati teule hiyo ya wabunge tisa wanatarajia itawasaidia.

“Kwenye kamati hiyo kuna mbunge wa jimbo letu la Simanjiro James Ole Millya, tunaimani na kijana wetu ambaye alisababisha spika Ndugai aunde tume baada ya kutoa malalamiko yake,” alisema Juma.Mchimbaji mwingine John Mollel alisema tume nyingi ziliundwa ikiwemo ya Jaji Mark Bomani na zikafika Mirerani kujionea hali ilivyo ila hazikumaliza matatizo yaliyopo hivyo anaimani na tume ya bunge.

“Tulimchagua kijana mdogo James Ole Millya akaenda bungeni ambapo amekuwa sauti ya wanyonge wala hajali tumbo lake zaidi ya kutoa malalamiko yetu tunayolalamika kila siku,” alisema Mollel.

Akiwa bungeni Spika Ndugai aliunda tume ya wabunge tisa itakayoongozwa na Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya nishati na madini Dotto Biteko.

Akitoa maelezo kwa wabunge alisema ametumia kanuni ya 5, kanuni ndogo ya 1 ya kanuni za kudumu za bunge toleo la Januari 2016 inayompa uwezo wa kuunda kamati yoyote ili kuleta ufumbuzi wa jambo Fulani ambalo ataikabidhi serikali kwa hatua ya utekelezaji.

Wajumbe wengine wa tume hiyo ni mbunge wa jimbo la Simanjiro James Ole Millya, Balozi Adadi Rajab, Ezekiel Maige, Dk Mary Mwanjelwa, Subira Mgalu, Juma Hamad Omari, Abdalah Mtopea na Mohamed Mchengerwa.

Alisema kazi ya kamati hiyo ni nyingi ikiwemo kuchambua mkataba kati ya shirika la madini la Taifa, State Mining Cooperation (Stamico) na kampuni ya TanzaniteOne mining Ltd, kwa lengo la kubainisha manufaa 
na hasara ambazo nchi imepata kutokana na mkataba huo.

Alisema kazi nyingine ni kutathmini mfumo wa uchimbaji, usimamizi na udhibiti wa biashara ya madini ya Tanzanite ili yaweze kuchangia ipasavyo kwenye uchumi wa Taifa.

Alisema pia watachambua taarifa ya tume na kamati mbalimbali zilizowahi kuundwa na serikali kipindi kilichopita kwa ajili ya kushughulikia maboresho yake na kuona namna ambavyo utekelezaji 
wake umefanyika.

Spika Ndugai aliipa siku 30 kamati hiyo iliyoanza kazi rasmi mwezi Julai baada ya vikao vya bunge la bajeti kuahirishwa na itafanya kazi kwa mwezi mmoja na kurudisha taarifa bunge la mwezi Septemba.

No comments:

Post a Comment