Tuesday, 11 July 2017

MASAUNI ALIAGIZA JESHI LA POLISI KUFUNGUA KITUO MAKAZI YA KABILA LA WAHADZABE

MASAUNI ALIAGIZA JESHI LA POLISI KUFUNGUA KITUO MAKAZI YA KABILA LA WAHADZABE



Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (watatu kushoto) na Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Massay (wapili kulia) wakicheza ngoma ya Wabarbaig/Watatoga kabla ya Masauni kuzungumza na mamia ya wananchi wa Kabila maarufu la Wahazabe na makabila mengine yaliyopo katika Bonde la Yueda Chini, Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara. Masauni aliiagiza Jeshi la Polisi mkoani humo, kujenga Kituo cha Polisi kwa uharaka ili jamii hiyo ambayo inaishi pembezoni mwa mji wa Mbulu. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
HAZA2
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na mamia ya wananchi wa Kabila maarufu la Wahazabe na makabila mengine yaliyopo katika Bonde la Yueda Chini, Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara. Masauni aliiagiza Jeshi la Polisi mkoani humo, kujenga Kituo cha Polisi kwa uharaka ili jamii hiyo iweze kupata ulinzi wa kutosha katika eneo hilo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
HAZA3
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akijadiliana na maafisa wa halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara pamoja na watendaji mbalimbali wa wilaya hiyo, ndani ya jengo la mifugo lililopo Yaeda Chini katika makazi ya Wahazabe, ambalo linatarajiwa kufunguliwa Kituo cha Polisi. Kulia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi mkoani Manyara (RPC), Francis Massawe, na kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Massay. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
HAZA4
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akiwafafanulia jambo Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Massay (kulia) na Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini, Zakaria Isaay mara baada ya Naibu waziri huyo kukagua Jengo la Mifugo (nyuma yao) ambalo linatarajiwa kufunguliwa Kituo cha Polisi ili kuwasaidia wananchi wa kabila la Wahazabe na wengineo wanaoishi katika Bonde la Yueda Chini, Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara kuleta ulinzi wa raia hao pamoja na mali zao. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
HAZA5
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto), akimsikiliza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Francis Massawe alipokuwa akijibu maswali mbalimbali ya uhalifu ambayo yaliulizwa na wananchi (hawapo pichani) wa Kijiji cha Yueda Chini Wilaya ya Mbulu mkoani humo, ambalo kuna makazi ya jamii ya Kabila la Wahazabe.  Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
HAZA6
Wananchi wakimshangilia Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (hayupo pichani) wakati alipowatangazia kufunguliwa Kituo cha Polisi hivi karibuni katika Kijiji cha Bonde la Yueda Chini, lililopo wilayani Mbulu, Mkoa wa Manyara. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
…………………………………………………………..
Na Felix Mwagara (MOHA)
 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amelitaka Jeshi la Polisi mkoani Manyara kufungua Kituo cha Polisi katika Makazi ya Kabila la Wahazabe wanaoishi katika Bonde la Yueda Chini, wilayani Mbulu.
Masauni alisema hayo jana wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa kabila  hilo mara baada ya kukagua jengo la mifugo katika eneo la bonde hilo ambalo jamii hiyo ilijitenga kwa kuweka makazi pembezoni mwa Mji wa Mbulu.
“Hivi karibuni Kituo cha Polisi kitafunguliwa hapa ili kulinda usalama wenu katika eneo hili ambalo lilikua halina kituo cha Polisi kwa miaka mingi. Serikali ya Rais Magufuli ni sikivu ndio mana nimekuja hapa kuwasikiliza matatizo yenu na kuwatekelezea.” Alisema Masauni huku akishangiliwa na wananchi hao.
Aliongeza kuwa, mchakato wa kujenga kituo hicho umeanza na tayari ametoa maelekezo kwa Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa huo, kwa kushirikiana na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Wabunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini na Mbulu Mjini.
 Pia aliongeza kuwa, uhalifu katika eneo hilo sasa umepata tiba kwa maana Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi watahakikisha hali ya usalama unaimarishwa zaidi katika eneo hilo ambalo lipo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Massay alisema wananchi wa jimbo lake wanavamiwa, wanaporwa mali zao ikiwemo mifugo, wanajeruhiwa na wanaingizwa katika umaskini zaidi kutokana na waalifu kuwa wengi kutokana na ukosefu wa Kituo cha Polisi.
“Nilimuomba na nilimsumbua sana Naibu Waziri kule Bungeni ili aweze kufika katika eneo hili, ninamshukuru sana kwa kufika na kutoa maelekezo ya kufunguliwa kituo cha polisi, sasa wakazi wa eneo hili tunatarajia kupata ulinzi wa kutosha baada ya kituo hicho kufunguliwa hivi karibuni,”alisema Massay.
Mkuu wa Jeshi la Polisi mkoani humo, Francis Massawe alisema amepokea maelekezo kutoka kwa Naibu Waziri na mchakato utaanza rasmi na hatimaye kituo cha Polisi kitakuwepo katika eneo hilo na wananchi wataendelea na shughuli zako za kutafuta mahitaji yao kwa usalama zaidi.

No comments:

Post a Comment