DKT NCHIMBI APOKEA MADAWATI ZAIDI YA 2000 KUTOKA BUNGENI KWA NIABA YA MIKOA YA KASKAZINI
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi leo ampokea madawati 2579 kutoka
kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa niaba ya mikoa ya
Manyara, Arusha na Kilimanjaro.
Akipokea
madawati hayo yaliyosafirishwa katika magari 19 ya Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) Dkt Nchimbi amelipongeza jeshi hilo kwa uzalendo huo wa
kuhakikisha mali za umma zinafika Singida kwa ajili ya kuanza
kusambazwa katika halmashauri husika zikiwa salama na katika hali nzuri.
Dkt
Nchimbi amelipongeza Bunge kwa uzalendo wa kumuunga mkono Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika
kuhakikisha sekta ya elimu inaboreka nchini ili kutimiza azma ya
kufikia uchumi wa kati na wa viwanda.
Amesema
madawati hayo yataongeza motisha kwa wanafunzi kujisomea kwakuwa
mazingira yatawawezesha kuandika na kusoma kwa ufanisi zaidi.
Aidha
Dkt Nchimbi amezitaka halmashauri zitakazopokea madawati hayo
kuhakikisha wanayatunza ili yadumu na kuwanufaisha wanafunzi kwa muda
unaostahili.
“Madawati
na yenyewe yanahitaji ukarabati, sio kwakuwa mmepewa basi muyaache tu,
hapana, ukiona ubao unalegea kidogo basi hakikisha unarekebisha na sio
kuanza kusubiri waliotupatia ndo waturekebishie”, amesema na kuongeza
kuwa.
“Ili
madawati haya yadumu waalimu na wanafunzi kwa pamoja wahakikishe
wanayatunza vizuri, hasa walimu wasimamieni wanafunzi na muaelekeze
namna ya kuyatunza kwakuwa hii ni mali yetu sote”, Amesisitiza.
Aidha
Dkt Nchimbi ameongeza kuwa mkoa wa Singida uko tayari kupokea vifaa na
mambo mbalimbali ya kitaifa kutokana na kuwa katikati mwa Tanzania hivyo
kuwezesha usambazaji kwa mikoa mingine kuwa rahisi.
“Tunakaribisha
taasisi, mashirika, na hata serikali kuu kama kuna vifaa vingine leteni
Singida ni katikati na usambazaji utakuwa ni rahisi, lakini pia hata
shughuli zozote za kitaifa mkoa wa Singida uko tayari kabisa kuzipokea”
amesema Dkt Nchimbi.
Kwa
upande wake Afisa Elimu Vifaa na Takwimu wa halmashauri ya Wilaya ya
Meru Frank Paul Mwambachi amelishukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa
kuwapatia madawati ambapo halmashauri yake imepata madawati 400.
Mwambachi
amelishukuru JWTZ kwa kuyasogeza madawati jirani na halmashauri yake
hivyo itakuwa rahisi na salama zaidi kwake kuyasafirisha na kuyafikisha
yakiwa katika hali nzuri na kwa uharaka zaidi.
“Madawati
400 wakikaa wanafunzi watatu watatu ina maana ni wanafunzi 1200
wamenufaika, kwa kweli tunalishukuru sana bunge kwa uzalendo wao, pia
jeshi limetusaidia sana kuyaleta madawati yetu Singida ambapo ni jirani”
amesema Mwambachi.
Aidha
ameongeza kuwa madawati hayo yataboresha mazingira ya ufundishaji na ya
kujifunzia hivyo halmashauri itahakikisha wanayatunza ili wanafunzi
wanufaike kwa kipindi kirefu.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akipokea kwa furaha moja ya
magari ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yaliyokuwa yamebeba
Madawati hayo 2579 yanapelekwa katika mikoa ya Manyara, Arusha na
Kilimanjaro. Madawati hayo yametolewa na bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akimpongeza kwa furaha mmoja wa
mwanajeshi aliyehusika kusafirisha Madawati 2579 yaliyotolewa na bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mikoa ya Manyara, Arusha na
Kilimanjaro. Madawati hayo yamefikishwa Singida kwa ajili ya urahisi wa
kuyasambaza katika mikoa hiyo.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akishirikiana na wanajeshi
kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Askari wa Magereza
kushusha madawati yalitolewa na Bunge. Madawati hayo 2579 yanapelekwa
katika mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro.
Askari
wa Magereza wakipanda moja ya magari ya JWTZ na kusaidia kushusha
sehemu ya madawati 2579 yaliyopokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida kwa
niaba ya mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
Afisa Elimu Vifaa na Takwimu wa halmashauri
ya Wilaya ya Meru Frank Paul Mwambachi akisaidiana na askari kubeba
madawati waliyopatiwa na Bunge ambapo halmashauri yake imepewa madawati
400.
No comments:
Post a Comment