Friday 7 July 2017

DC MBULU ASITISHA UCHIMBAJI DHAHABU HAYDOM



Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Chelestino Mofuga amepiga marufuku uchimbaji wa madini ya dhahabu kwenye machimbo ya Haydom hadi hapo mwekezaji atakapokamilisha mkataba na Halmashauri ya wilaya hiyo.

Pia, Mofuga ameagiza kukamatwa kwa mmiliki na dereva wa lori la tani 10 lililokutwa limebeba mchanga wa dhahabu (makinikia) kutoka machimbo ya Haydom likipeleka mkoani Singida kuchenjua.

Alisema aliamua kufanya ukaguzi wa kushtukiza kwenye machimbo ya dhahabu ya Haydom na kukuta lori la tani 10 likiwa na mchanga unaopelekwa mkoani Singida.



Alisema alipata taarifa kuwa lori hilo lilishabeba mchanga huo zaidi ya mara sita kabla ya kukamatwa na kuamuru kusitisha kwa zoezi hilo la kwenda kuchenjua dhahabu hiyo mkoani Singida badala ya Haydom. 

“Nimeagiza mmiliki na dereva wa lori hilo lenye namba za usajili T 662 AWT mali ya Mohamad Ally mkazi wa jijini Arusha kushikiliwa kwenye kituo cha polisi Haydom hadi uchunguzi ufanyike,” alisema Mofuga.

Alisema ametoa amri ya kusitishwa kwa uchimbaji wa dhahabu kwenye eneo hilo hadi hapo mwekezaji atakapokamilisha mikataba na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Hudson Kamoga.

No comments:

Post a Comment