Wednesday, 12 July 2017
VIONGOZI WA USHIRIKA MSIINGIZE SIASA-MASWI
Viongozi wa chama kikuu cha ushirika cha Rift Valley Cooperative Union (RIVACU) na vyama vya msingi vya ushirika Mkoani Manyara, wametakiwa kuwatumikia ipasavyo wanachama wao wa ushirika na kutoingiza siasa kwenye shughuli zao.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Eliakim Maswi aliyasema hayo kwenye mjini Babati kwenye kikao cha vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) vya wilaya za mkoa huo.
Maswi alisema viongozi hao wanapaswa kuwatumikia wanachama wa vikundi hivyo na siyo kuingiza siasa kwenye ushirika na maendeleo jambo ambalo litasababisha kurudisha nyuma maendeleo yao.
Alisema viongozi wa vyama vya ushirika wanapaswa kushuka chini kwenye wanachana na kuzungumza nao ili kujua changamoto na matatizo waliyonayo ili kuyatatua na wasibaki juu kwenye chama.
Alisema huu ni wakati wa mabadiliko kwa kupiga hatua ya maendeleo kwa vyama vya ushirika hivyo watumie fursa hiyo kubadilika na kutumia nafasi zao ipasavyo na kuachana na maneno matupu.
“Unakuta kiongozi kwa muda wote wa miaka mitatu hafanyi jambo lolote la maana zaidi ya kuzua migogoro na kula fedha za ushirika, hiyo tabia ikome kwani wote tutawachukulia hatua,” alisema Maswi.
Mwenyekiti wa Rivacu, Lohay Langay alisema madhumuni ya chama hicho kikuu cha ushirika ni kukusanya, kutafuta masoko, kusindika na kuuza mazao ili kusaidia kukuza hali ya uchumi kwa wanachama wake.
Langay alisema wanatarajia kuendeleza kilimo cha mahindi, pamba, kahawa, alizeti, mazao ya mikunde na mazao mengine kwenye wilaya za Babati, Hanang’ Mbulu na Ngorongoro na Karatu mkoani Arusha.
“Hivi sasa Rivacu inaendesha shughuli zake kwa kukodisha mashamba na majengo hali ambayo ni hatari kwa ustawi wa chama ila tunatarajia kuongeza mapato kwa vyanzo vingine,” alisema Langay.
Alitaja vyanzo hivyo ni kuongeza hisa za chama, mikopo, kodi ya mazao na tozo nyingine, ununuzi wa mazao kwa mkopo wa benki ya maendeleo ya kilimo, mradi wa uvunaji mbao na mradi wa nyuki.
Mrajisi msaidizi wa ushirika mkoa wa Manyara, Venance Msafiri alisema hivi sasa wanatembelea kwenye vikundi mbalimbali na kuwajengea uwezo wa kuhakikisha wanapiga hatua.
Msafiri alisema kwa kusaidiana na maofisa ushirika wa wilaya wanavitembela vikundi na kuwapa elimu na vile vyenye changamoto na migogoro ya uongozi wanaitatua kwa kuhakikisha inamalizika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment