Friday, 14 July 2017

Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es salaam Mhe. Isaya Mwita atembelea miradi ya maendeleo


Na Christina Mwagala, Ofisi ya Meya wa Jiji
MSTAHIKI Meya wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita leo amefanya ziara ya kutembelea miradi ya Maendeleo ya jiji ambapo ameridhishwa na vikundi vinavyo tengeneza mkaa kwa kutumia malighafi ambapo amesema itasaidia kupunguza uchafu uliopo kwenye maeneo mbalimbali na kuliweka jiji katika hali ya usafi. 
Ziara hiyo ambayo imehusisha Kamati ya Fedha ya Halmashauri ya Jiji, ilitembelea vikundi vya Maendeleo ya ujasiriamali cha Upendo Smart kilichopo mtaa wa Kilimahewa Kata ya Tandika kinachojihusisha na uzalishaji wa mkaa mbadala ( mkaa poa). 
Aidha mbali na kikundi hicho Meya Mwita pia amejionea shuguli za uzalishaji wa mkaa unaofanywa na kikundi cha Maendeleo cha Mwangaza Vikoba kilichopo Pugu stesheni jijini hapa. 
Akizungumza na wanakikundi hao, Meya Mwita amesema kuwa vikundi hivyo vinafanya kazi kubwa kutokana na ubunifu walionao jambo ambalo litasaidia kuweka jiji kwenye hali ya usafi. 
Alifafanua kuwa mbali na kuweka jiji safi pia litapunguza grama kwa wananchi wanaotumia nishati ya mkaa kutokana na nishati hiyo kuuzwa kwa bei nafuu ukilinganishwa na ule unaotumika hivi sasa kwakuwa unagharama kubwa. 
” Mmefanya kazi nzuri sana wakina mama ,nimeona juhudi zenu, lakini nimesikia changamoto kubwa hapa ninamna ya kuwafikia hao watu waweze kununua nishati hii, niwahakikishie madiwani wenu wapo hapa, Meya wenu nipo hapa tutaendelea kuwaunga mkono” amesema Meya Mwita. 
Amesema” wananchi wanatumia gharama kubwa kununua mkaa unaochomwa kwa kutumia miti, lakini unapotumia huu ambao unatengenezwa na vikundi hivi , kwakutumia malighafi , unawezesha kuinua kiuchumi lakini pia tunatoka kwenye matumizi ya mazoea na kuingia kwenye matumizi ya kisasa. 
Awali ziara hiyo ilianzia kwenye mradi wa ujenzi wa viwanda vidogo vidogo katika eneo la karakana ya Mwananyamala ambapo lengo la mradi huo ni kuwahudumia wananchi na wajasiriamali wadogo wadogo ilikuinua hali za kiuchumi hususani wakina mama na vijana. 
Mradi huo unatokana na fedha zilizotengwa na Halmashauri ya Jiji katika bajeti ya mwaka 2016 /2017 ambapo kwa awamu ya kwanza mradi huo umepangwa kutumia kiasi cha shilingi milioni 190, hadi kufikia mwisho wa mwezi huu utakuwa umekamilika kwa asilimia 82. 
Hata hivyo Mhandisi wa mradi huo katika Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam Swalehe Nyenye amesema kuwa awamu ya kwanza ya mradi huo kutajengwa majengo makubwa mawili yenye vyumba vitatu kila moja kwa ajili ya biashara.
Jengo la mradi wa viwanda vidogo vidogo lililopo eneo la Karakana Mwananyamala jijini Dar es Salaam. Awamu ya kwanza ya jingo hilo limepangwa kutumia shilingi milioni 190, ambapo inatarajiwa mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu utakuwa umekamilika kwa asilimia 82.(Picha zote na Christina Mwagala, Ofisi ya Meya wa jiji) 
Mstahiki Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita mwenye shati la kijivu akitoa maelekezo kwa maofisa Utumishi wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam leo alipofanya ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo ya jiji karakana ya Mwananyamala jijini hapa. 
Mhandisi katika Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam Swalehe Nyenye akifafanua jambo kwa Mstahiki Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita alipofanya ziara ya kutembelea ujenzi wa viwanda vidogo Karakana ya Mwananyamala. 
Mkurugenzi wa kampuni ya Kuja na Kushoka tool Manufucture Leodard Kushoka akitoa maelezo jinsi namna ambavyo mashine ya kutengenezea nishati ya mkaa kwa kutumia malighafi inavyofanya kazi wakati wa ziara waliofanya kwenye kikundi hicho kilichopo Tandika. Wa kwanza kulia ni Diwani wa Kata ya Segerea Pratrick Asenga. 
Mashine inayotumika kutengeneza nishati ya mkaa 
Jengo la kikundi cha Upendo Smart kinachofanya shughuli ya kuzalisha nishati ya mkaa kwa kutumia malighafi. 
Mwenyekiti wa kikundi cha Mwangaza Vikoba kilichopo Pugu stesheni Mariam Mzigilwa akisoma risala kwa Mstahiki Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita aliyeambatana na wajumbe wa kamati ya fedha ya jiji leo alipotembelea kikundi hicho, ikiwa ni moja ya ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo ya jiji. 

No comments:

Post a Comment