Sakata la kifo cha
mchimbaji wa madini ya Tanzanite wa mgodi wa Gem & Rock Venture wa mji
mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, unaopakana na kampuni ya
TanzaniteOne, limechukua sura mpya baada ya mgodi huo na ule wa CT
kufungiwa.
Takribani kwa muda wa
siku tano mfululizo kulikuwa na vurugu zilizotokea kwenye migodi hiyo
iliyopakana huku kila upande ukituhumu mgodi mwingine kuwa unawarushia mabomu
ya kutengeneza kienyeji, kupitia mitobozano iliyopo.
Kutokana na vurugu hizo
mchimbaji wa mgodi wa Gem & Rock Venture, Lembris Mbatia (22) alifariki
dunia na wengine 13 kujeruhiwa baada ya kudaiwa kupigwa bomu la kutengeneza
kienyeji na kulipuliwa mgodini humo na wafanyakazi wa kampuni ya TanzaniteOne.
Kamishna msaidizi wa
madini kanda ya kaskazini, Adam Juma alisema amesitishwa
shughuli za uchimbaji kwenye migodi hiyo miwili ili kupisha uchunguzi ufanyike
juu ya mgogoro uliopo hivi sasa.
Juma alisema wameamua
kusitisha kwa muda shughuli za uchimbaji wa madini kwenye migodi hiyo miwili
ili kufanyike mazungumzo baina ya pande hizo mbili na kufikiwe muafaka wa
uchimbaji salama.
Alisema wafanyakazi wa
Wizara ya Nishati na Madini, kutoka kitengo cha ukaguzi wa migodi wanatarajia
kufika kwenye eneo hilo na kukagua migodi hiyo miwili kwa lengo la kupata
suluhu.
Mkuu wa wilaya hiyo,
mhandisi Zephania Chaula alizitaka pande hizo mbili kukaa pamoja na kupata ili
kupata suluhu ya mgogoro huo ambao umesababisha kifo cha mchimbaji mmoja na
wengine kujeruhiwa.
"Pamoja na hayo,
bado nasisitiza kutotumika kwa matumizi ya mabomu ya kutengeneza kienyeji kwani
nimeshaagiza polisi wawachukulie hatua kali wale wote watakaobainika kuwa
wanajihusisha na vitendo hivyo viovu," alisema mhandisi Chaula.
Alisema suala la usalama
katika migodini linapaswa kupewa kipaumbele kwani endapo kutatokea matatizo
kwenye machimbo hayo ya Tanzanite, shughuli za uchimbaji hazitafanyika.
Meneja wa mgodi wa Gem
& Rock Venture, Joel Saitoti alisema ni kawaida ya wafanyakazi wa kampuni
ya TanzaniteOne kuteka migodi mara baada ya kupata tetesi kuwa mgodi unaopakana
nao unatoa madini.
Saitoti alisema kampuni
ya TanzaniteOne inavyofanya siyo jambo sahihi kwani ni migodi mingi ya
wachimbaji wadogo ambayo imedhulumiwa haki zao kwa kuporwa njia zinazotoa
madini.
"Japo tumefungiwa
kwa muda katika migodi yote miwili lakini wao TanzaniteOne wanaendelea na kazi
kwenye migodi yao mingine na tunasubiri tukutane nao tuzungumze ili tupate
suluhu," alisema.
Hata hivyo, meneja wa
ulinzi wa kampuni ya TanzaniteOne Abubakary Yombe alikanusha vikali wafanyakazi
wa kampuni yake kutuhumiwa kumuua mchimbaji wa mgodi huo wa Gem & Rock
Venture, Mbatia.
Alisema wenyewe
wanafanya kazi kwenye eneo la leseni yao ila wachimbaji wa mgodi wa Gem &
Rock Venture ndiyo wamewaingilia katika mtobozano na kufanyia kazi sehemu
ambayo siyo ya kwao.
"Habari
zinazotolewa kuwa tunateka migodi ya wachimbaji wadogo siyo za kweli kwani wao
ndiyo wanaingia ndani ya eneo letu la leseni kupitia mtobozano na serikali
inapaswa kuchukua hatua juu ya hilo ili kukomesha tatizo hilo," alisema
Abubakary.
No comments:
Post a Comment