Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Kamoga amesema watanzania wanapaswa kumuunga mkono Rais John Magufuli kwenye vita ya kulinda rasilimali za nchi aliyoianzisha.
Kamoga anasema vita ya kulinda rasilimali ya nchi inapaswa kuungwa
mkono kwani utajiri wa nchi ya Tanzania haulingani na hali halisi
iliyopo kutokana na watu wachache kupora utajiri kupitia madini
mbalimbali.
Anasema ana imani Rais Magufuli na watanzania kwa ujumla watashinda vita ya kulinda rasilimali kwani kupitia ripoti ya kwanza na ya pili ya makinikia imeonyesha namna wananchi wanyonge wanavyoibiwa.
“Watanzania wote tunapaswa kusimama pamoja na Rais wetu John Magufuli katika vita hii ya kusimamia na kulinda rasilimali za nchi kupitia madini yetu kwani nia ya dhati ameionyesha hivyo nasi tunapaswa kuwa naye kwa dhati kabisa,” anasema Kamoga.
Anasema Tanzania imepata Rais mwenye uchungu na nchi yake mwenye nia ya dhati ya kuwatumikia watanzania, anaipenda na anatamani wananchi wake waishi kwenye maisha bora yenye huduma zote za msingi.
“Tangu tumepata uhuru, mwalimu Julius Nyerere alitangaza maadui watatu ikiwemo maradhi, umasikini na ujinga, vitu ambavyo bado havijamalizika na bado Rais Magufuli anapambana kwa ajili ya kutokomeza hayo kwani ni shauku ya baba wa Taifa kumalizika hayo,” anasema Kamoga.
Anasema kwa miaka yote Tanzania imekuwa ikipambana na hayo yote lakini tangu kuachwa kwa azimio la Arusha na kutangazwa kwa azimio la Zanzibar kuliibuka ubinafsi hivyo nia na shauku ya kupambana na hayo ilionyesha kulegalega na sasa Rais Magufuli amezindua upya falsafa ya kupambana na maadui hao watatu kupitia rasilimali za nchi yetu wenyewe.
“Shauku, kiu na hamu ya mwalimu Nyerere ya kuhakikisha watanzania wanaishi kwenye maisha yaliyo bora kwa kutegemea rasilimali walizonazo ilikuwa njema na ndivyo hivi sasa Rais Magufuli anavyofanya hivyo wananchi kwa ujumla wanatakiwa kumuunga mkono ili tufike kule ambapo anatarajia kutufikisha kwenye Tanzania mpya yenye neema,” anaeleza Kamoga.
Jamii iache kelele zisizo na msingi ila kumuunga mkono Rais Magufuli
Anasema watu wanapaswa kuacha kelele, minongono maneno mengi na kumuunga mkono Rais Magufuli katika kuhakikisha wananchi wanajiletea maendeleo yao wenyewe kwa kufanya kazi na siyo kukaa hivi hivi na kufikiri kuna mtu atakayemletea maendeleo mwenzake.
Anasema hivi sasa bado kuna watu wanashindwa kufanya kazi na kumuunga mkono Rais Magufuli na siyo kubaki mtaani na vijiweni kwa kuzungumza mambo yasiyo yale ya msingi ambayo hayawezi kuleta maendeleo yoyote.
“Hata Rais Magufuli anasema tumechelewa kujiletea maendeleo wenyewe hivyo tuache kupiga fumzo na kufanya kazi, japokuwa hatujachelewa sana tunapaswa tukimbie ili kufikia malengo yetu tuliyojiwekea,” anasema Kamoga.
Anasema hata watu wanaokimbia hawawezi kuwa na mafanikio kwenye mbio zao endapo watakuwa wanazungumza na wakati wote huo huo wawe wanakimbia, lazima watashindwa kukimbia ipasavyo.
“Rais anaposema tukimbie tukiwa na uzalendo ndani yetu tukiwa na
dhamira njema na uadilifu ili tufikie malengo yetu na yeye hapendi
watu wanaozungumza sana kuliko kufanya kazi ambayo mwisho wa siku tutakuwa tumejiletea maendeleo yetu wenyewe,” anasema Kamoga.
Anasema hata vijana wengi hivi sasa wamekuwa wanashinda kuangalia mitandao ya kijamii, kwenye suala ambalo halina faida au maana yoyote kwao na jamii kwa ujumla, hivyo kushikwa na sintofahamu ya jambo hilo lililokithiri sehemu tofauti tofauti hapa nchini.
“Watu wapo ambao ukiwaona kwenye mitandao ya kijamii, ukiangalia vitu vinavyotupiwa huko unagundua kuwa siyo ya msingi na hata huku vijijini ukiangalia mitandao hiyo haina mambo ambayo yanaweza kuwavusha watanzania wa vijijini sehemu walipo ambapo kuna changamoto kubwa mno,” anasema Kamoga na kuongeza;
“Maneno mengi yanayozungumzwa siyo ya msingi na hata ukienda vijijini unakuta tumechelewa mno kwani bado jamii inaishi kwenye changamoto kubwa ya umasikini mkubwa hivyo tuwe tunafikiria na kuzungumza mambo ya msingi na yenye kutuletea maendeleo.”
Amejitolea kuacha alama Mbulu
Mara baada ya Rais John Magufuli
kuniteua kuwa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani
Manyara, niliona ninalo deni kubwa la kuwatumikia watanzania wa Mbulu kupitia
nafasi hii,” anasema Kamoga.
Kamoga yeye kama kijana amejitolea kwa
uwezo wake wote kuhakikisha kuwa anaacha alama ya maendeleo kupitia nafasi
aliyonayo ya ukurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu.
Anasema yeye kama kijana, ameaminiwa
na Rais na kupatiwa madaraka hayo hivyo atahakikisha anatumia nafasi hiyo kwa
kuwatumikia wananchi wote wa Mbulu bila ubaguzi wowote ule ili kuhakikisha kuwa
gurudumu la maendeleo linapatikana.
Anasema viongozi wa wilaya ndiyo
wasaidizi wakubwa wa Rais Magufuli na kupitia nafasi walizonazo, jamii
inatarajia kumuona Rais Magufuli akiwatumikia wao kupitia nafasi walizonazo
viongozi hao.
“Ili mwananchi wa kule Yaeda Chini,
Haydom, Dongobesh au Murkuchida aweze kuona uwepo wa Rais Magufuli kwa hapa
Mbulu inatubidi sisi viongozi wa wilaya tutekeleze ipasavyo wajibu wetu kwa
kuwatumikia na kuwatendea haki na hivi ndivyo tunavyofanya,” anasema Kamoga.
Anaeleza kuwa yeye kama kijana ana
malengo makubwa na halmashauri ya wilaya ya Mbulu, kwa kuhakikisha anatumia
uwezo wake wote kuhakikisha anashirikiana kuwatumikia wananchi wote ili mwisho
wa siku aache alama kubwa ya kukumbukwa.
“Kuna fursa nyingi mno zilizopo kwenye
wilaya ya Mbulu, ikiwemo madini, mifugo, kilimo na rasilimali nyingine hivyo
kupitia nafasi hiyo, ana matumaini makubwa kuwa eneo hilo litasonga mbele na
kupiga hatua kubwa ya maendeleo,” anasema Kamoga.
Anasema watanzania hasa waliopo
vijijini wamechelewa mno kupata maendeleo ikiwemo huduma za afya, elimu na
maji, hivyo kupitia wananchi na viongozi wa eneo hilo watahakikisha kuwa
wanatumia rasilimali zilizopo kwa ajili ya kufanikisha hayo.
Historia yake kwa ufupi
Kamoga alizaliwa mwaka 1978 kwenye hospitali ya Kilimatinde wilayani Manyoni, mkoani Singida na alihitimu darasa la saba kwenye shule ya msingi Kange na sekondari ya Galanosi mkoani Tanga.
Alisomea stashahada ya masoko katika chuo cha CBE jijini Dar es
salaam, alisomea maendeleo ya jamii kwenye MAM Training Centre, Advance diploma in child development and psychology na akasomea shahada yapili ya Mass Communication kwenye Tumaini University ya jijini Dar es salaam.
Alifanya kazi kwenye kampuni ya Clouds media na kupata umaarufu mkubwa kupitia kipindi cha asubuhi alichokuwa anakiongoza cha 360 kwenye Clouds TV na mwaka 2016 akateuliwa na Rais Magufuli kuwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu.
No comments:
Post a Comment