Monday 31 July 2017

MCHIMBAJI KWENYEMADINI YA TANZANITE AFARIKI DUNIA

 Mchimbaji wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, amefariki dunia kwa kukosa hewa na wengine 13 kujeruhiwa baada ya kudaiwa kupigwa bomu la kutengeneza kienyeji na kulipuliwa mgodini kwao na walinzi wa kampuni ya TanzaniteOne. 

Pia, askari polisi wa kituo cha Mirerani walijeruhiwa na kupata majeruhi usoni, kichwani na mikononi wakati wakiingia kwenye mgodi huo kwa kukwaruzwa na miamba wakati wakikagua chanzo cha tatizo hilo. 

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi Francis Massawe alisema tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia Julai 29 mwaka huu. 

Kamanda Massawe alimtaja marehemu huyo kuwa ni Lembris Mbatia (22) mkazi wa Sekei jijini Arusha, ambaye mwili wake umehifadhiwa kwenye hospitali ya rufaa ya mount Meru. 

Alisema kuna baadhi ya wafanyakazi wa mgodi huo walioishiwa hewa na kupandishwa mgodini kisha wakapelekwa hospitali kupatiwa huduma ya kwanza. 

"Bado tutafanya uchunguzi wa tukio hilo ila chanzo ni mtobozano wa mgodi huo na mgodi wa CT unaomilikiwa na kampuni ya TanzaniteOne," alisema kamanda Massawe. 

Mkuu wa wilaya hiyo, mhandisi Zephania Chaula aliwataka wachimbaji hao kuwa watulivu kipindi hiki cha kuondokewa na mwenzao na wengine kujeruhiwa baada ya kutokea tatizo hilo. 

"Ninyi ni wangu na TanzaniteOne ni wangu mimi ndiyo baba yenu hivyo nimesikiliza malalamiko yenu ila fanyeni subira tunafanya kikao na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya na kamishna msaidizi wa madini na RPC yupo tutatoa maamuzi," alisema mhandisi Chaula. 


Kamishna Msaidizi wa madini kanda ya kaskazini, mhandisi Adam Juma alisema hawezi kuongea chochote hadi hapo watu wote waliopo kwenye migodi hiyo miwili wapandishwe juu ndiyo ataweza kutoa tamko lolote. 

"Bado nafanya mawasiliano na kamishna wa madini mhandisi Benjamini Mchwampaka, juu ya tukio hilo hivyo vuta subira nitatoa tamko juu kinachofuata," alisema Juma. 

  
Hata hivyo, meneja ulinzi wa kampuni ya TanzaniteOne, Abubakary Yombe alisema hawezi kuzungumza chochote kwani anashughulikia suala la usalama wa wafanyakazi wake waliokuwa eneo la tukio. 

"Tufanye mawasiliano baadaye kwani nazama kwenye mgodi wa CT kuangalia mambo yanavyokwenda nitaongea na waandishi wa habari nikipanda juu, " alisema Yombe huku akijiandaa kuzama kwenye mgodi huo. 

Meneja wa mgodi huo wa Gem & Rock wenye PML namba 0002333 Joel Saitoti alisema mgogoro na kampuni hiyo ndiyo umesababisha hali hiyo kwani walitumia mtobozano na mgodi wa jirani yao kufanya fujo. 

Saitoti alisema wao hawajatobozana nao kwani wanafanya kazi sehemu yao ila waliposikia hali ya mgodi ipo vizuri wakawafanyia fujo na kusababisha matatizo hayo. 

No comments:

Post a Comment