Thursday 13 July 2017

TALGWU YAONYA KUHAMISHWA WANACHAMA WAKE



Chama cha wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) Mkoa wa Manyara, kimelalamikia kitendo cha baadhi ya maofisa utumishi wanaoshuhulikia mishahara kuwahamisha kwenye chama chao baadhi ya watumishi ambao ni wanachama wake na kuwahamishia katika chama kingine.

Mwenyekiti wa Talgwu wa mkoa wa Manyara Dk Martin Kongola akizungumza mjini Babati alisema wanalaani kitendo cha maofisa utumishi hao kuwatoa watumishi wa serikali za mitaa katika chama chao.

Dk Kongola alisema baadhi ya maofisa hao wa utumishi huwaamisha wafanyakazi wa serikali za mitaa ambao siyo walimu na kuwaamisha kwenye chama cha wafanyakazi wa serikali kuu bila kufuata sheria.

Alisema wafanyakazi wa serikali za mitaa ambao wapo kwenye halmashauri wanapaswa kuwa kwenye chama cha Talgwu hivyo kitendo cha kuwahamisha kwenye chama kingine ni kufanya makosa.

Katibu wa Talgwu mkoa wa Manyara, Raymond Chimbuya alisema haina haja ya kugombania fito kwa sababu wanajenga nyumba moja hivyo kitendo cha maofisa utumishi hao kinapaswa kukemewa vikali.

Chimbuya alisema watumishi wa vituo vya afya na zahanati ambao wapo chini ya halmashauri za wilaya wanapaswa kuwa kwenye Talgwu na watumishi wa hospitali hao wapo serikali kuu.

Alisema wanafuatilia suala hilo na endapo watagundua kuwa kuna mazingira yamefanyika kwa kumuondoa mwanachama wa Talgwu na kumpeleka sehemu nyingine watalifikisha kwenye vyombo vya sheria.

“Kuna waraka uliotoka Tamisemi na upo wazi kabisa kuwa watumishi wa halmashauri wawe kwenye Talgwu na waliopo ngazi ya mkoa wawe serikali kuu na ndivyo inavyopaswa kuwa,” alisema Chimbuya.

Mwenyekiti wa kamati ya ushauri ya Talgwu mkoa huo, Mwanaid Shaban alisema lengo la chama chao ni kuwatetea watumishi wote wanaofanya kazi kwenye serikali za mitaa na ndivyo wanavyofanya.

Shaban alisema pia wanatetea haki za watumishi hao kwenye utendaji wao wa kila siku na kuhakikisha wanapatiwa stahiki zao zote na kusimamia na kutekeleza wajibu wao katika kutumikia Taifa.

No comments:

Post a Comment