Thursday, 31 May 2018

MNYETI AAGIZA MANYARA IKAMILISHE VIWANDA 100

MNYETI AAGIZA MANYARA IKAMILISHE VIWANDA 100

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, wakiwemo maofisa tarafa, madiwani, watendaji wa kata, vijiji, walimu na wenyeviti wa vijiji, juu ya kufanya kazi kwa uadilifu na kutumikia jamii, kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo mhandisi Raymond Mushi.
Mkuu wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Mhandisi Raymond Mushi akizungumza na wananchi wa Kata ya Madunga juu ya kufanya kazi na kuwahusia kuwa siku mbili ambazo mtu hawezi kufanya chochote ni jana na kesho hivyo waitumie siku ya leo kwa kutimiza wajibu wao, kulia ni Mkuu wa Mkoa huo Alexander Mnyeti na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Nicodemus Tarmo.
Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini Mkoani Manyara, Vrajilal Jituson, akizungumza na wananchi wa Kata ya Madunga ambao wanachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo yao ikiwemo suala la elimu.
Mbunge wa viti maalum wa mkoa wa Manyara, Esta Mahawe akizungumza na wananchi wa Kata ya Madunga ambapo alijitoa mashuka 10 kwa ajili ya wagonjwa watakaotumia kwenye zahanati ya kijiji hicho iliyozinduliwa na Mkuu wa mkoa huo Alexander Mnyeti.


Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti ameziagiza Halmashauri za Wilaya za Mkoa huo kuhakikisha zinatekeleza agizo la uanzishwaji wa viwanda 100 na hadi mwezi Septemba mwaka huu viwe vimekamilika. 

Mnyeti akizungumza na watumishi na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, alisema kila halmashauri ya mkoa huo wenye halmashauri saba, inapaswa iwe na viwanda 15. Mnyeti alisema serikali ilitoa agizo la kila mkoa uanzishe viwanda 100 hivyo na mkoa wa Manyara nao unapaswa kuhakikisha unatekeleza agizo hilo kwa kila halmashauri kuwa na viwanda 15. 

Alisema agizo hilo linatakiwa kutekelezwa kwa kila sekta ikiwemo kilimo na mifugo ambazo ndizo shughuli kuu za kiuchumi kwa wananchi wengi wa mkoa huo. “Watumishi wa umma wanapaswa kutambua kila taaluma waliyoisomea wanapaswa kuwekeza kwenye fikra ya viwanda kwa kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa sekta hiyo,” alisema Mnyeti. 

Aliwapongeza mkuu wa wilaya hiyo mhandisi Raymond Mushi na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Hamis Malinga kwa kutekeleza agizo hilo la uanzishwaji wa viwanda vipya. “Kwenye miezi mitatu iliyopita Halmashauri ya Babati mlikuwa mmeshafanikisha uanzishwaji wa viwanda nane na hadi kufikia mwezi Septemba mtakuwa mmekamilisha viwanda 15 hongereni sana,” alisema Mnyeti. 
 
Mkuu wa wilaya ya Babati, mhandisi Raymond Mushi alisema wananchi wa eneo hilo ni wachapakazi wazuri na hujishughulisha na shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, ujasiriamali na nyinginezo.

Mushi alisema kwa kiasi kikubwa wananchi wa wilaya yake ni wachapakazi huku wakishirikiana na serikali katika kufanikisha maendeleo mbalimbali.Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Vrajilal Jitu Son alisema wameshajipanga kutekeleza hilo kupitia viwanda mbalimbali vilivyopo jimboni humo.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Babati, Hamis Malinga alisema kwa kiasi kikubwa wamefanikisha utekelezaji wa vipaumbele mbalimbali ikiwemo elimu, afya na maji.“Kwenye suala la migogoro ya ardhi, kamati ya ulinzi na usalama chini ya Mwenyekiti wake mheshimiwa mkuu wa wilaya kwa kiasi kikubwa imefanikisha kusuluhisha japo kuwa maeneo machache yaliyobaki na yanaendelea kufanyiwa kazi,” alisema.

Jituson alisema kwenye eneo hilo kuna viwanda mbalimbali vipya vilivyojengwa vikiwemo vya mafuta, sukari, kukoboa mpunga, unga, na kiwanda cha vyakula vya mifugo. Alisema kupitia nafasi ya vijiji vingine 30 kupatiwa umeme wa Rea awamu ya tatu, itasaidia kuanzisha viwanda vidogo na vya kati kwa wajasiriamali mbalimbali waliopo kwenye jimbo hilo. 

Mkazi wa Kijiji cha Endanachang’ John Lorry alisema serikali na sekta binafsi zinapaswa kujipanga na kuanzisha kiwanda cha biskuti ili zao la mbaazi lipate soko. Lorry alisema changamoto ya soko la mbaazi imekuwa kero kwa jamii ila kupitia viwanda wakulima wengi wa eneo hilo wataweza kunufaika kwa kupata sehemu ya uhakika ya kuuza zao hilo.

Thursday, 24 May 2018

KATIBU MKUU WIZARA YA HABARI AWATEMBELEA WANANCHI JAMII YA WAHADZABE NA WATATOGA HUKO ESHKESH WILAYANI MBULU MKOA WA MANYARA

Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi akizungumza na wananchi wa jamii za Wahdzabe Watatoga na Wasukuma wakati alipotembelea Kata ya Eshkesh kijiji cha Dumanga Yaeda Chini wilayani Mbulu mkoa wa Manyara wakati alipozitembelea jamii hizo ili kuzungumza nao kuhusu maisha yao pamoja na uhifazi wa tamaduni na mila zao ambao unaweza kuwa Kivutio cha Utalii pia lakini pia kujua mahitaji yao ya muhimu katika maisha ya jamii hizo.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi akizungumza na wananchi wa jamii za Wahdzabe Watatoga na Wasukuma wakati alipotembelea Kata ya Eshkesh kijiji cha Dumanga kutoka kushoto ni Gesso Bajuta diwani wa kata ya Endamilay wilayani Mbulu, Kaimu Mkurugenzi wa Utamaduzi Wizara ya habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi Beleko na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Bw. Hudson Kamoga.
Wananchi wa Eshkesh Jamii ya Watatoga wakiwa katika mkutano huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Bw. Hudson Kamoga akizungumza katika mkutano huo.
Gesso Bajuta diwani wa kata ya Endamilay wilayani Mbulu akizungumza katika mkutano huo.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi akimtunza mmoja wa vijana aliyekuwa akicheza ngoma ya kisukuma katika mkutano huo.
Mmoja wa vijana wapiga ngoma akipiga ngoma kwa mbwembwe wakati kikundi cha ngoma ya kisukuma kikitumbuiza.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi akijadiliana jambo na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbulu Bw. Hudson Kamoga.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi. Suzan katikati na Kaimu Mkurugenzi wa Utamaduni Wizara ya Habari Sanaa na Utamaduni Bi. Liliano Beleko wa pili kutoka kushoto wakicheza ngoma na akina mama wa jamiii ya Wahadzabe katika kijiji cha Dumanga.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi akimpa pole mama aliyejifungua na kupoteza manaye alifariki baada ya kuzaliw.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi akizungumza na Mmoja wa akina mama wa kihazabe nyumbani kwake Jamii ya Wahadzabe wananawake ndiyo wanaojenga nyumba kazi ya wanaume ni kuwinda wanyama na kurina asali pamoja na kutafuta mizizi kwa ajili ya chakula.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi akitoka katika moja ya nyumba ya familia ya kihdzabe.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi akifurahia jambo baada ya kuvaliswa zawadi ya mkanda uliotengenezwa kwa Shanga na Bi.Chrstina Paulo mama wa jamii ya Kihadzabe.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi akivishwa mkanda uliotengenezwa kwa Shanga na Bi.Chrstina Paulo mama wa jamii ya Kihadzabe.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbulu wakikimbia na akina mama wa Kihadzabe huku wakiimba kuelekea eneo la makazi yao mara baada ya kupokelewa.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbulu wakicheza na akina mama wa Kihadzabe huku wakiimba kuelekea eneo la makazi yao mara baada ya kupokelewa.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbulu wakipokelewa na wananchi wa Dumanga wa jamii ya Kitatoga mara baada ya kuwasili kijijini hapo.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbulu wakipokelewa na ngoma ya akina mama wa Kihadzabe 
Vijana wa Kitatoga wakiimba katika mapokezi hayo.

TFF YATANGAZA MAJINA YA WACHEZAJI 30 WATAKAOWANIA TUZO YA MCHEZAJI BORA MSIMU HUU

Na Agnes Francis Blogu ya Jamii.

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)limetangaza majina ya wachezaji 30 katika kuelekea mwisho wa Ligi  kuu  ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ambao watawania Tuzo za Mchezaji Bora mwaka huu.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Msemaji wa TFF Clifford Ndimbo amesema utaratibu huo hufanyika kila mwaka baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya Vodacom kwa kushirikiana na Kampuni ya Simu ya Mkononi ya Vodacom.

Ndimbo amefafanua wachezaji hao 30 watachujwa na kubaki 10 na baadae watabaki wachezaji wa tatu wataoinga hatua ya fainali ili kumpata Mchezaji bora kwa msimu huu.

Amewataja wachezaji wanaowania tuzo hiyo ni Habibu Kyombo (Mbao),Khamis Mcha,(RuvuShooting),Yahya Zayd(Azam),Razack Abalora(Azam), Bruce  Kangwa(Azam) Aggrey Morris(Azam),Himid Mao (Azam),Awesu Awesu(Mwadui) na Adam Salamba(Lipuli).

Wengine ni Mohammed Rashid(Prisons), Shafiq Batambuze(Singida),Mudathir Yahya (Singida), Marcel Kaheza(Majimaji),Ditram Nchimbi(Njombe Mji) na Eliud Ambokile(Mbeya City).

Pia Shaaban Nditi(Mtibwa), Tafadzwa Kutinyu(Singida) Ibrahim Ajibu(Yanga), Gadiel Michael(Yanga),Papy Tshishimbi(Yanga),Kelvin Yondani(Yanga),Obrey Chirwa(Yanga),Aishi Manula(Simba), Emmanuel Okwi(Simba),John Bocco(Simba), Jonas Mkude(Simba),
Erasto Nyoni(Simba),Shiza Kichuya(Simba),Asante Kwasi(Simba),Hassan Dilunga(Mtibwa).

"Mchakato wa kupata mchezaji bora unatarajia kufanyika Juni 23 mwaka huu katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam. Ambapo msimu huu kutakuwa na washirika wengine Azam Tv, Benki ya KCB na Premier Bet,"amefafanua

Pia amesema licha ya tuzo ya Mchezaji Bora wa mwaka wa ligi, kutatolewa tuzo mbalimbali, ambapo kwa mwaka huu tuzo moja imeondolewa na nyingine imeongezwa ikiwa ni katika uboreshaji

"Tuzo iliyoondolewa ni ya Mchezaji Bora wa Kigeni na imefanyika hivyo ili kuwapa fursa wachezaji wote kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa VPL badala ya kuwatenganisha, vile vilee msimu huu imeongezwa Tuzo ya Mwamuzi Bora Msaidizi ambayo haikuwepo msimu uliopita.Hiyo ni kutokana na kuthamini nafasi ya waamuzi wasaidizi,"amesema Ndimbo

Kwa mazingira hayo tuzo zitakazotolewa siku hiyo ambapo wadhamini wakuu ni Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom ni Bingwa,Mshindi wa Pili,Mshindi wa Tatu,Mshindi wa Nne, Mfungaji Bora,Timu yenye nidhamu,U20 Player (Tuzo ya Ismail Khalfan),Mchezaji Bora Chipukizi, Mwamuzi Bora Msaidizi,Mwamuzi BoraKipa Bora,Kocha Bora,Goli Bora VPL,Best Eleven,pamoja na Mchezaji wa heshima.

Ndimbo amesema zawadi kwa kila kategori pamoja na majina ya wanaowania tuzo ukiacha bingwa, mshindi wa pili, wa tatu, wa nne na mfungaji bora ambao hujulikana kulingana na ligi inavyoendelea zitatangazwa siku za usoni.

"Kila mwezi Kamati ya Tuzo, imekuwa ikitangaza jina la mchezaji aliyefanya vizuri kwa mwezi husika kutokana na vigezo mbalimbali na pia ripoti kutoka kwa makocha waliopo katika viwanja ambavyo ligi hiyo inachezwa.

"Wachezaji  ambao  walishinda tuzo za mwezi ligi ya msimu huu ni nimshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi (Agosti), beki wa Singida United, Shafiq Batambuze (Septemba) na mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa (Oktoba). 

"Wengine ni kiungo wa Singida United, Mudathir Yahya (Novemba), mshambuliaji wa Mbao FC ya Mwanza, Habibu Kiyombo (Desemba), mshambuliaji wa Simba, John Bocco(Januari), kiungo wa Yanga, Papy Tshishimbi (Februari), mshambuliaji wa  Lipuli, Adam Salamba (Machi) na mshambuliaji wa Majimaji, Marcel Kaheza (Aprili),"amesema Ndimbo.

Ambapo wachezaji hao kila mmoja amepewa zawadi ya tuzo, king'amuzi cha Azam na fedha Sh.milioni moja kutoka kwa wadhamini Vodacom.

Tuesday, 22 May 2018

KATIBU MKUU WA WIZARA YA HABARI, SUSAN MLAWI ATEMBELEA 4CCP

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Susan Mlawi (kushoto) akifurahia jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Kamoga, kwenye nyumba ya jamii ya wabantu kituo cha pembe nne za utamaduni Haydom (4CCP), kulia ni mwakilishi wa jamii hiyo Salimu Shabani.

WAJASIRIAMALI WAASWA

 Wajasiriamali nchini wametakiwa kuwa na nia ya ushindi wa mafanikio kwa uthubutu kufanya jambo la maendeleo kwa lengo thabiti bila kujali vikwazo vilivyopo kwani kukata tamaa ndiyo mwanzo wa kushindwa.

Mkurugenzi wa asasi ya IBN LLC ya jijini Washington nchini Marekani, mhandisi Elic Elisha Bahunde aliyasema hayo kwenye mafunzo ya ujasiriamali yaliyofanyika mji mdogo wa Haydom Wilayani Mbulu Mkoani Manyara na kuandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Hudson Kamoga.

 Mhandisi Bahunde alisema uthubutu na ubunifu ndiyo siri ya mafanikio yeyote yale hivyo wajasiriamali wawe na moyo wa kujaribu jambo ili wafanikiwe maishani.

"Mshindi huwa hakati tamaa, tuthubutu, tujitume, tusikate tamaa na matatizo ni fursa yatumie kuyatatua kwa kuongeza kipato chako," alisema mhandisi Balance.

Ofisa maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Amoniche Mtweve alisema ujasiriamali ni uwezo wa kukubali kuingia katika biashara na kusimamia jambo kwa ujasiri.

Mtweve alisema mjasiriamali anapaswa kuwa na aina tatu za umiliki wa biashara ikiwemo umiliki wa pekee, ubia wa kawaida na ushirika.



 Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu Hudson Kamoga aliwataka vijana kutoishi maisha yao kwa ndoto za mtu mwingine.

"Jitambue kuwa wewe ni wewe na jitahidi kuishi maisha yako kupitia ndoto ulizonazo huku ukimtanguliza Mungu na kuongeza juhudi kwa kile unachokifanya kwa moyo wa dhati utafanikiwa," alisema Kamoga. 
Mratibu wa kituo cha pembe nne za utamaduni Haydom (4CCP) Eliminata Awet amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa wajasiriamali hivyo wangepaswa kujitokeza kwa wingi.

Awet alisema baadhi ya vijana huwa wanalalamika kuwa serikali haiwapi fursa, lakini Kamoga amejitolea kuandaa mafunzo ya ujasiriamali bila malipo wakajitokeza wachache.

Mmoja kati ya washiriki wa Neema Joel alisema kupitia semina hiyo anatarajia kupiga hatua ya maendeleo kwenye ujasiriamali.

Joel alisema amejengewa uwezo zaidi wa ujasiriamali tofauti na awali alipokuwa akijishughulisha na ufugaji wa kuku wa nyama.

Mwanafunzi wa kidato cha tano wa shule ya sekondari Dk Olsen Carren Amani alisema kupitia mafunzo hayo amebaini kuwa siyo lazima uajiriwe serikali au sekta binafsi ila kupitia ujasiriamali unaweza kujiajiri.


WATUMISHI MBULU KUFANYA MAZOEZI KILA MWISHO WA WIKI

 Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara wamejipanga na utaratibu wa kufanya mazoezi kila mwisho wa wiki kwa lengo la kuimarisha afya ya mwili, akili, moyo na kupambana na magonjwa yasiyoambukizwa ikiwemo shinikizo la damu, kisukari na magonjwa ya moyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Hudson Kamoga akizungumza wakati wa kufanya mazoezi hayo mji mdogo wa Haydom, alisema wameanzisha utaratibu huo wa kufanya mazoezi kila mwisho wa wiki badala ya mara moja kwa mwezi ili waweze kuimarisha afya zao.

 Kamoga alisema kupitia mazoezi wanayofanya watumishi hao, hata ari ya kufanya kazi huongezeka zaidi kwani mwili na akili huwa  zinashirikiana ipasavyo.

Alisema binadamu bila kuwa na afya bora hawezi kufanya jambo lolote la maana zaidi ya kuitwa mgonjwa hivyo waepuke hayo kwa kufanya mazoezi kila mwisho wa wiki.

"Sisi watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, tunamuunga mkono Makamu ya Rais mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa agizo lake kufanya mazoezi kila mwisho wa mwezi Kwan kushiriki kila wiki," alisema Kamoga.

Mkurugenzi wa hospitali ya rufaa ya Haydom Dk Emmanuel Nuwass alisema mazoezi ni jambo jema kwa binadamu ambaye anatakiwa kufanya mazoezi nusu saa kwa kila siku.

Dk Nuwass alisema kupitia mazoezi, binadamu huwa na amani moyoni na kuepukana na hasira, msongo wa mawazo na damu kupita kwenye mishipa ya mwili ipasavyo.


Ofisa mtendaji wa kijiji cha Harara, Bertila Mwinuka alisema kufanya mazoezi husababisha kuimarisha mwili na kuongeza upendo na umoja.


MARDADI ALIA NA MAJI LOIBORSIRET

Diwani wa Kata ya Loiborsiret Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Ezekiel Lesenga (Mardadi) ameitaka Halmashauri ya Wilaya hiyo kuwaangalia wananchi wake kwa jicho la huruma ili waweze kupata huduma ya uhakika wa maji kwani wengi wao wanatumia maji kidogo yaliyopo kwa kushirikiana na mifugo.

Mardadi alisema wananchi wa kata yake wanaishi kwenye nyanda kame hivyo halmashauri hiyo ifanye jitihada za kuwezesha upatikanaji wa huduma hiyo ili waondokane na kero ya maji.

Alisema suala la tatizo la maji ni kero ya muda mrefu na yeye kama diwani wa eneo husika ataendelea kulisemea hilo hadi ufumbuzi upatikane kwa wananchi wake wa kata ya Loiborsiret.

"Hali ya wananchi wa eneo hilo kwenye huduma ya maji ni ndogo kwani hivi sasa wanategemea mabwawa yaliyojaa maji kutokana na mvua ndiyo wanatumia wao na mifugo," alisema Mardadi.

Alisema wakati wa kiangazi unapofika maji ya kwenye mabwawa hukauka na kuwapa wakati mgumu binadamu na mifugo kupata huduma ya maji.

Alisema kwenye kata yake ya Loiborsiret suala la maji ni tatizo kubwa kwenye vijiji vyote vya Loiborsiret, Kimotorok na Narakauwo.

Alisema anatarajia halmashauri ya wilaya ya Simanjiro italiangalia suala hilo kwa upana zaidi ili huduma ya maji kwenye eneo hilo iwe ya uhakika tofauti na sasa.

"Wakati wa kiangazi jamii ya eneo hilo hupata wakati mgumu kwani maji yanapatikana kwa shida hivyo kusababisha mifugo kufa na wananchi nao wanateseka," alisema Mardadi.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa kamati ya Elimu, Afya na Maji wa baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo Sendeu Laizer akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita alisema wamepanga kuchimba kisima kimoja kwenye kata hiyo.


"Kamati yetu kwenye mapendekezo yake iliazimia kuchimbwe kisima kimoja katika kijiji cha Narakauwo kata ya Loiborsiret ili jamii ya eneo hilo na mifugo waweze kupata huduma ya maji," alisema Laizer. 

MWENYEKITI UVCCM MANYARA NA MIKAKATI YA KUWANYANYUA KIUCHUMI

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Manyara, Mosses Komba akizungumza na wanawake wa jumuiya ya UWT wa kata ya Naisinyai juu ya mikakati ya kuwajengea uwezo kwa kupatiwa mchanga wa kuchekecha mabaki ya madini ya Tanzanite.

BARAZA LA MADIWANI SIMANJIRO LAPITISHA KUTOLEWA MILIONI 100 ZA MIKOPO

 Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, limepitisha kutolewa kwa zaidi ya sh100 milioni kwa ajili ya mikopo ya kuwezesha wanawake na vijana kwa lengo la kuwanyanyua kiuchumi.



Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Jackson Sipitieck akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani kilichofanyika mji mdogo wa Orkesumet, alisema fedha hizo zimetokana na asilimia 10 za mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.



Sipitieck alisema baraza la madiwani wa halmashauri hiyo wamekuwa na kawaida ya kupitisha fedha hizo ambazo kwa namna moja au nyingine zitafanikiwa kubadili maisha ya vijana na wanawake wa eneo hilo.



“Tumefanikiwa kugawa fedha hizo kwenye kata mbalimbali za halmashauri ya wilaya yetu ambayo  ina kata 18 na tutaendelea kuzigawa kwa haki kwa vikundi vingine vilivyokidhi masharti na vigezo vya kupatiwa,” alisema Sipitieck.



Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Yefred Myenzi alisema hadi hivi sasa fedha hizo sh100 milioni zimetolewa kwa vipindi tofauti na kikao cha baraza hilo kimepitisha fedha nyingine sh32.6 milioni zitakazopatiwa kwenye kata sita.



Myenzi alitaja kata hizo sita za Mirerani, Oljoro namba tano, Shambarai, Komolo, Loiborsiret na Msitu wa Tembo ambapo vimetolewa kwa vikundi 16 vya wanawake na vijana wa Simanjiro.



Alisema halmashauri hiyo itaendelea kutoa fedha hizo pindi itakapokuwa inakusanya makusanyo yake ya ndani hivyo wanawake na vijana wachangamkie fursa hiyo kupitia asilimia 10 za mapato ya ndani.



Diwani wa kata ya Loiborsiret, Ezekiel Lesenga Mardadi amewataka wanawake na vijana wa kata hiyo waliopatiwa mikopo hiyo kuitumia kwa malengo sahihi ili waweze kurejesha kwa wakati.



Mardadi alisema endapo vijana na wanawake hao wataitumia vizuri mikopo hiyo watajinyanyua kwenye biashara zao na watarejesha kwa wakati ili wengine nao waweze kufaidika.



Diwani wa kata ya Shambarai Julius Mamasita alisema vijana na wanawake wa kata yake wana ari kubwa ya kutumia mikopo hiyo kwa lengo la kujinyanyua kiuchumi na wametoa ahadi kuwa watafanikisha hilo.



“Naishukuru halmashauri ya wilaya ya Simanjiro kwa kutupatia mikopo hii nasi wananchi wa kata ya Shambarai tutaweza kutumia mikopo hii ipasavyo na kisha kuirejesha kwa wakati,” alisema Mamasita  



SERIKALI YAHIMIZA HALMASHAURI KUBUNI MIRADI YA KIMKAKATI ILI KUJIONGEZEA MAPATO

Serikali imeeleza kuwa Uchukuaji wa baadhi ya vyanzo vya mapato katika halmashauri ulifanyika kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti iliyoridhiwa na Bunge ya mwaka 2015 kifungu namba 58 ikiwa na lengo la kuongeza ufanisi wa ukusanyaji na matumizi ya mapato hayo.

Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Suzana Mgonukulima, aliyependekeza itungwe sheria ya kuibana serikali ikiwa haitarejesha fedha zilizotokana na vyanzo vya mapato vilivyopo kwenye Miji, Halmashauri, Manispaa na Majiji zitakazokusanywa na kuwekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 44 cha Sheria ya Bajeti, mgao wa fedha kutoka katika Mfuko Mkuu wa Serikali utazingatia bajeti iliyoidhinishwa, upatikanaji na mtiririko wa fedha, utekelezaji mpango wa ununuzi na mpango wa kuajiri hivyo hakuna Fungu litakaloruhusiwa kufanya matumizi ya aina yoyote mpaka kuwe na fedha za kulipa matumizi husika.

“Usimamizi wa Mapato hayo kwa mujibu ya Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2015 Kifungu namba 58 unazingatia mapato kuingizwa kwenye Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Fedha za Serikali, aliyepewa mamlaka ya kukusanya mapato ya Serikali atawajibika katika ukusanyaji wenye ufanisi, utunzaji wa hesabu, utoaji wa taarifa na kuzuia ufujaji wa mapato”, alisema Dkt. Kijaji. 

Alisema Usimamizi wa mapato na matumizi umebainishwa vizuri na hivyo hakuna haja ya kutunga sheria nyingine ya kuibana Serikali ikiwa haitapeleka fedha kwenye, Miji, Halmashauri, Manispaa na Majiji.

Aidha akijibu swali la nyongezai la Mhe. Mgonukulima kuhusu kutokuwa na usawa katika utoaji wa fedha za maendeleo katika Wilaya, Dkt. Kijaji alisema kuwa tarehe 5 Mei, 2018 Serikali ilizindua Mkakati wa kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza miradi yenye kuchochea upatikanaji wa Mapato ili ziweze kujitegemea hivyo ni vema Halmashauri zikabuni miradi ya maendeleo itakayoongeza mapato.

Akieleza kuhusu utaratibu wa malipo ya Kodi ya Majengo kutoka katika Halmashauri nchini Naibu Waziri Dkt. Kijaji, alisema kuwa Majengo yasiyofanyiwa tathimini yanatakiwa kutozwa kiwango sawa cha Sh. 10,000 na majengo ya juu (ghorofa) yanatakiwa kutozwa kiwango sawa cha Sh. 50,000.

Alisema majengo yaliyofanyiwa tahimini ndiyo yanayoweza kulipiwa kodi zaidi ya kiasi hicho, hivyo wakurugenzi wa Halmashauri wanapaswa kuzingatia utaratibu huo uliowekwa katika ukusanyaji wa kodi hiyo, alieleza Dkt. Kijaji.

Imetolewa na;
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango

WAKULIMA KITETO WAJENGEWA UWEZO WA KUPAMBANA NA VIWAVIJESHI VAMIZI

 Wataalamu wa kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani ( FAO) wamewajengea uwezo wakulima wa wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara juu ya namna ya kupambana na viwavijeshi vamizi vinavyoshambulia zao la mahindi.

Sehemu mbalimbali za mkoa wa Manyara wakulima wengi wanalalamikia mazao yao ya mahindi yaliyopo mashambani hivi yameshambuliwa na wadudu hao.

Wataalamu hao waliwasilisha mada tatu juzi wilayani Kiteto ambazo ni  utambuzi, uchunguzi, ufuatiliaji na udhibiti wa wadudu hao viwavijeshi vamizi.

Akiwasilisha mada ya kwanza ambayo ni utambuzi , Ofisa kilimo Sergea Mutahiwa  alielezea namna ya kumtambua kiwavijeshi vamizi, mzunguko wa maisha yake, tabia zake na muonekano wake.

Pia ameeleza kuhusu hali ya viwavi jeshi nchini, ushirikishwaji wadau, usambazaji wa machapisho, ushiriki wa vyombo vya habari na mtazamo wa jamii kuhusu viwavijeshi vamizi .

Alisema mtazamo wa jamii na uelewa mdogo ni tatizo juu ya uelewa kwa viuatilifu vinavyopendekezwa na jinsi ya kutumia dawa za kuangamiza wadudu hao hatari kwa kushambulia mazao.

Alisema wakulima wameendelea  kutumia viatilifu  vingi vya aina mbalimbali  na katika maeneo mengine wakulima hutumia dozi kubwa kutokana na mashambulizi kujirudia .

Mutahiwa alisisitiza kuwa  matumizi  yasiyo sahihi ya viatilifu yanaweza kusababisha  kuua wadudu wasiolengwa  na  kudhuru afya za binadamu, vilevile kusababisha usugu  kwa visumbufu vya mimea.

Alisema viatilifu vinavyoshauriwa na  Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu (TPRI) na serikali kupitia wizara ya kilimo inatarajia kuzichukua ili  kudhibiti kisumbufu hicho.

Ofisa kilimo Grace David alitoa mada ya ukaguzi na ufuatiliaji kwa kufuatilia ukuaji wa mimea shambani, kwamba mimea inatakiwa kufuatiliwa katika ukuaji wake.

Alielekeza namna ya kufanya ukaguzi kuwa ufanyike zigizaga, usifuate mstari  ili kuwakilisha shamba zima  na usichukue zaidi ya dakika 15.

Alisema ukaguzi ni muhimu ili kubaini  uwepo na kiasi cha viwavijeshi vamizi, na kufanya tathmini ya madhara ili kuweza kujua njia sahihi ya kufanya udhibiti.

Pia, aliwaelezea wakulima hao namna ya kutumia mtego maalum wenye harufu kwa ajili ya kukamata viwavijeshi vamizi.

Ayubu  Nchimbi akitoa mada ya tatu ya udhibiti viwavijeshi vamizi alisema udhibiti wa kiwavijeshi vamizi unaanza na utambuzi.

Nchimbi alisema lazima kumtambua kisumbufu, mzunguko wa maisha yake, dalili za mashambulizi na kiasi gani mashambulizi yamefanyika.

Alisema dalili za  mashambulizi ndizo zitakazomuongoza mkulima  kujua kiasi cha mashambulizi na njia atakazotumia ili kudhibiti kisumbufu.

Alisema udhibiti sahihi wa viwavijeshi vamizi  katika ukuaji wa mimea ya mahindi unategemea na muda wa utambuzi wa mashambulizi ya mdudu kupitia ufuatiliaji na ukaguzi wa mimea shambani.


DONGOBESH FC YATWAA UBINGWA WA KURUGENZI CUP '18

 Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi akimkabidhi kombe kapteni wa timu ya Dongobesh FC ya Dongobesh Iddi Podoksi mara baada ya timu hiyo kuibuka na ushindi wa magoli 3-1 dhidi ya Rema 1000 FC ya Haydom katika mchezo wa fainali Kombe la Kurugenzi Cup 2018 uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi Haydom mjini Haydom wilaya ya Mbulu mkoani Manyara Michuano ya Kurugenzi Cup 2018
 Kapteni wa timu ya Dongobesh FC ya Dongobesh Iddi Podoksi akinyanyua kombe juu mara baada
ya timu yake kuibuka na ushindi wa magoli 3-1 dhidi ya Rema 1000 FC ya
Haydom katika mchezo wa fainali Kombe la Kurugenzi Cup 2018 uliofanyika
kwenye uwanja wa shule ya msingi Haydom
 Wachezaji wa Dongobesh FC wakifurahia kombe lao mara baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 3-1 kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Rema 1000 FC kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Haydom katika fainali ya Kurugenzi Cup 2018.
 Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi akikabidhi jezi kwa timu ya   Rema 1000 FC ya Haydom baada ya kuibuka mshindi wa pili  katika mchezo wa fainali Kombe la Kurugenzi Cup 2018 uliofanyikakwenye uwanja wa shule ya msingi Haydom
 Mashabiki wa timu ya Dongobesh wakimnyanyua juujuu golikipa wao anayejulikana kwa jina la Mapilau baada ya timu yao kuibuka bingwa wa michuano hiyo na kuibuka kuwa golikipa bora wa michuano hiyo.
 Wachezaji wa timu ya Rema 1000 wakiwania mpira wakati mchezo huo ukiendelea.
  Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi akipiga mpira golini kuashiria uzinduzi wa fainali hizo.
 Kikosi cha timu ya Dongobesh FC kikiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kwa mchezo huo.
 Kikosi cha timu ya Rema 1000 kikiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kwa mchezo huo.
  Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi akiwa katika picha ya pamoja na kamati ya maandalizi ya michuano hiyo.
  Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi akikagua timu ya Dongobesh FC kabla ya kuanza kwa mchezo huo.
  Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi akikagua timu ya Rema 1000 FC kabla ya kuanza kwa mchezo huo.
  Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi akizungumza kabla ya kuanza kwa mchezo huo.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbulu Bw. Hudson Kamoga akizungumza na kumshukuru  Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi kwa kushiriki kwake katika fainali za michuano hiyo.
 Baadhi ya wananchi wakifuatilia mchezo huo.
  Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi na Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Bw. Hudson Kamoga wakiwasili kwenye uwanja wa shule ya msingi ya Haydomtayari kwa kushuhudia mchezo wa fainali.
 Baadhi ya mashabiki wakiwa wamefurika uwanjani hapo kushuhudia mchezo wa fainali katika ya Dongobesh FC na Rema 1000 FC.