Friday 2 February 2018

WANANCHI 744 WAPATIWA HUDUMA YA VIPIMO VYA MACHO, KISUKARI NA SHINIKIZO LA DAMU



Wananchi 744 wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, wamepatiwa huduma ya vipimo vya macho, kisukari na shinikizo la damu bila kulipia gharama, kwa muda wa siku mbili kwenye kituo cha afya Magugu. 

Mbunge wa jimbo la Babati vijijini, Vrajilal Jituson akizungumza kwenye kituo cha afya Magugu, alisema huduma hiyo imeletwa kwa ushirikiano na Lions Club ya jijini Arusha. 

Jituson alisema huduma hizo zilitolewa bila wananchi kuchangia fedha, ambapo wagonjwa 54 watafanyiwa upasuaji na 36 watasubiri hadi mwezi wa tatu. 

Alisema hao 36 watasubiri hadi mwezi Machi ili waende kufanyiwa upasuaji kwenye hospitali ya mji wa Babati (Mrara) kwani tatizo lao la mtoto wa jicho halijafikia hatua ya upasuaji. 



"Wataalamu hao wa afya kutoka Lions Club pamoja na kutoa huduma ya upimaji macho, pia walitoa elimu juu ya kisukari na shinikizo la damu," alisema Jituson. 

Alisema mara baada ya kufanyika kwa vipimo hivyo, wataalamu hao wamebaini kuwa baadhi ya vijana wadogo wa eneo hilo, wana tatizo la ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu. 

Alisema vijana hao walipatiwa elimu ya namna ya kuishi na kuepukana na magonjwa hayo ya kisukari na shinikizo la damu kwani siyo maradhi ya kurithi. 




Mmoja kati ya wagonjwa aliyefanyiwa vipimo vya macho, Husna Ramadhani alishukuru kutolewa huduma hiyo kwani wengine wasingeweza kusafiri hadi jijini Arusha kwa ajili ya kupata huduma hiyo. 

"Tunashukuru sana kwa watu wa Lions Club na mbunge wetu Jituson kwani kwa muda mrefu tumekuwa tunapata huduma hii bila kulipia chochote, tunaomba waendelee hivi," alisema Ramadhani. 

John Mosses alisema kuna wagonjwa wengi wamefanyiwa vipimo kwa gharama ambazo wasingeweza kutimiza kutokana na kipato chao kidogo ila sababu ya Lions Club wamefanikiwa. 

No comments:

Post a Comment