MKUU wa Mkoa wa Manyara, Alexander
Pastory Mnyeti amewapongeza Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga na
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Hudson Kamoga kwa kutimiza
wajibu wao ipasavyo wakati wanapowatumikia wananchi wa eneo hilo.
Alisema tangu akiwa mkuu wa wilaya ya
Arumeru mkoani Arusha kabla ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mkuu wa
Mkoa wa Manyara, alikuwa anawasiliana na Mofuga kutokana na utendaji kazi bora
anaoufanya.
Alisema Mofuga ni kiongozi mwadilifu
mwenye kuwatumikia wananchi wa Mbulu hivyo viongozi na wananchi wa wilaya hiyo
wanapaswa kumpa ushirikiano wa kutosha.
Hata hivyo, aliwataka viongozi hao
kuhakikisha wanatekeleza maelekozo na maagizo yote alioyatoa kwenye ziara hiyo
kwa kadiri muda alioupanga ili kuhakikisha wananchi wanapata majawabu ya
changamoto na matatizo waliyotoa kwa wakati muafaka.
Mnyeti akizungumza kwenye majumuisho
ya ziara yake ya siku tano ya kutembelea halmashauri ya wilaya hiyo, alisema
viongozi hao wanastahili pongezi kutokana na utendaji kazi bora wao kwa jamii.
"Mheshimiwa mkuu wa wilaya
kupitia nafasi hii nakupongeza kwa dhati kutokana na utendaji kazi wako,
nakutakia kila la heri ili siku moja upande cheo uwe mkuu wa mkoa,"
alisema Mnyeti.
“Ukiona kiongozi anabishana na mkuu
wa wilaya basi huyo atakuwa na matatizo, wewe mkuu wa wilaya chapa kazi kwani
hakuna mtu mwenye mapembe au sharubu kwenye wilaya hii ya Mbulu zaidi yako wewe
Mofuga,” alisema Mnyeti.
Alisema Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga ni kiongozi mchapakazi
anayetekeleza wajibu wake ipasavyo na miaka ijayo atapandishwa cheo na Rais
John Magufuli.
“Mkurugenzi wewe chapa kazi, Rais
anavyombo vyake vingi vya uchunguzi atakuona tuu hata kama hayupo hapa kuna
watu wake wanaandika andika na kufikisha taarifa ipo siku atakuona zaidi na
kukupandisha cheo,” alisema Mnyeti.
Alisema Kamoga japokuwa ana muda
mchache tangu ateuliwe na Rais Magufuli kushikilia nafasi hiyo ametimiza wajibu
wake ipasavyo kwa kuwatembelea wananchi na kusikiliza matatizo yao huku
akisimamia vyema miradi ya maendeleo.
“Sina shaka na uadilifu wako kwani
unafanya kazi kwa uadilifu umeanza vizuri wewe chapa kazi, mimi nilikuwa mkuu
wa wilaya na leo ni mkuu wa mkoa kutokana na kufanya kazi hivyo fanya kazi
utapanda cheo tuu,” alisema Mnyeti.
Alisema ameanza kazi yake ya
ukurugenzi wa halmashauri vizuri hivyo aendelee hivyo hivyo kwa kuwasimamia
wakuu wa idara ili kuhakikisha wananchi wananufaika kwa kuwafanyia kazi.
No comments:
Post a Comment