Wednesday, 21 February 2018

DCC LUSHOTO YASITISHA MPANGO WA UJENZI WA JENGO LA HALMASHAURI YA BUMBULI

Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Lushoto (DCC) imeamua kusitisha mpango wa ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Bumbuli lilokuwa lijengwe kwenye eneo jipya la Kwehangala hadi hapo suluhu ya mgogoro baina ya viongozi wa halmashauri hiyo itakapopatikana. 

Mwenyekiti wa Kikao hicho ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Lushoto January Lugangika (Pichani Juu) alisema kuwa maamuzi hayo yamefikiwa baada ya kuwepo sintofahamu kati ya Madiwani wa halmashauri hiyo na viongozi wengine juu ya suala hilo. .

Hivi karibuni kumekuwepo na mvutano mkubwa kati ya viongozi hao juu ya wapi pajengwe majango ya makao makuu ya Halmashauri hiyo. Baadhi ya viongozi wanadai utaratibu wa fedha za manunuzi haukufuatwa katika kufikia maamuzi ya kujenga jengo la Halmashauri katika eneo la Kwehangala na kuacha majengo yaliyokwisha jengwa Bumbuli kwa gharama ya Sh. milioni 700.

Kutokana na mvutano huo, Mkuu huyo wa Wilaya amesema kikao kiliafiki kisitishe zoezi hilo mpaka maelewano yatakapopatikana." Wajumbe wameshauri suala la kuhamisha makao makuu lisitishwe hadi hapo utakapopatikana utangamano,kwani tayari imeonekana kuna mgogoro ambao umeleta utengano kwa viongozi" Alisema Lugangika .

Mbunge wa jimbo hilo, January Makamba alikiri kuwepo kwa mvutano huo ambao alisema hauna tija katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Bumbuli.Makamba alisema ni vyema kama viongozi wakazungumzia suala la maendeleo mfano;maji,barabara,umeme,nyumba za watumishi badala ya kila siku kuzungumzia wapi kujengwe jengo la halmashauri. 

Alishauri kuwa wananchi washirikishwe katika suala hilo, ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu ya kutosha juu ya hoja ya kuhamisha halmashauri kwa kuwa ndio wenye chombo chao badala ya viongozi kuamua wao pekee.

"Suala hilo nakubaliana na maoni wa kikao cha DCC tulisitishe kwani kwa sasa hatuna shida na majengo ya halmashauri kwa sababu majengo tunayo ambayo hatulipii kodi ya pango. Sasa hivi tuzungumzie maendeleo kwani wananchi mwaka 2020 hawatatudai majengo ya halmashauri bali watatudai maendeleo juu ya huduma muhimu za jamii alisema Makamba.

Hivi karibuni baadhi ya Madiwani wa Halmashauri hiyo walipiga kura ya kupitisha azimio la kujenga jengo hilo la halmashauri huku Madiwani nane wakigoma kupiga kura kwa madai kuwa hawawezi kupiga kura wakati kuna ukiukwaji wa kanuni na utaratibu ktk kitengo cha manunuzi.

Madiwani hao nane ambao waligoma kupiga kura kupitisha azimio hilo mnamo January 18 mwaka huu walimuomba Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi kuingilia kati mgogoro na kuzuia walichokiita ukiukwaji wa utaratibu wa manunuzi pamoja na maelekezo mbalimbali ya viongozi juu ya mpango huo.

Pia walimuomba aingilie kati na kuchukua hatua dhidi ya ubadhirifu wa fedha za umma na ukiukwaji wa utaratibu wa uendeshaji wa halmashauri na kudharau kwa makusudi maelekezo yaliyotolewa na viongozi mbalimbali wa serikali kuu.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Amir Shehiza alisema kuwa baraza ni chombo chenye maamuzi sahihi hivyo alikitaka Kikao hicho cha DCC kuacha kuingilia Kazi za baraza .

No comments:

Post a Comment