Rais wa shirikisho la vyama vya madini
nchini (Femata) John Bina akizungumza na wachimbaji madini ya Tanzanite wa Mji
mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Idadi ya vigogo wa madini ya
Tanzanite waliokamatwa kwa amri ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti,
imeongezeka baada ya wengine wawili kukamatwa hivyo kufikisha idadi ya
wachimbaji saba wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro
na jijini Arusha, kushikiliwa na polisi wakidai kudhamini uchimbaji haramu wa
madini hayo.
Awali, Mnyeti aliagiza vigogo hao
watano wa madini hayo kukamatwa na kushikiliwa kwenye kituo cha polisi Mirerani
ila wameongezeka wengine wawili na kufikia saba wakidaiwa kufadhili uchimbaji
huo haramu.
Akizungumza juu ya hilo, Kamanda wa
polisi wa Mkoa wa Manyara, Agostino Senga alithibitisha kukamatwa kwa vigogo
hao na kulazwa kituo cha polisi Mirerani.
Kamanda Senga alisema wanawashikilia
baada ya kamati iliyoundwa na mkuu wa mkoa huo kupata taarifa kuwa vigogo hao
wanashiriki kuwadhamini vijana wanaoingia kwa wizi kwenye migodi ya kampuni ya
TanzaniteOne yenye ubia na serikali kwa asilimia 50 kwa 50 na shirika la madini
la Taifa (Stamico).
Alisema bado wanaendelea na
wanachunguza suala hilo na endapo utakamilika vigogo hao (majina yao
tunayahifadhi) watafikishwa mahakamani.
"Bado tunaendelea na uchunguzi
wa tukio hilo kwani watuhumiwa hao wanadaiwa kuwadhamini wachimbaji hao haramu
ambao wanaingia migodini bila halali," alisema Senga.
Alisema kuna kamati maalum iliundwa
na mkuu wa mkoa huo kwa ajili ya kuchunguza suala hilo hivyo baada ya uchunguzi
wa awali, ikabidi vigogo hao wakamatwe.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa chama cha
wachimbaji madini wa mkoa wa Manyara (Marema) Sadiki Mneney alisema wamepata
taarifa za kukamatwa na kushikiliwa polisi kwa wachimbaji hao.
Mneney alisema wao kama Marema
wamepanga kwenye makao makuu ya mkoa huo mjini Babati kwa lengo la kuzungumza
na mkuu wa mkoa huo juu ya kukamatwa kwa wachimbaji hao.
"Jumatatu ijayo tunaenda Babati
kufuatilia suala hilo kwani hadi sasa hatujui ni sababu gani iliyofanya
wachimbaji hao wa madini wakakamatwa na kushikiliwa na polisi," alisema.
No comments:
Post a Comment