WACHIMBAJI wadogo
wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani
Manyara, wameiomba Serikali kuhakikisha nia ya kujenga ukuta unaozunguka migodi
ya madini hayo unakuwa na manufaa kwao na maendeleo ya nchi.
Wakizungumza
kwenye kikao cha wadau wa madini ya Tanzanite, wachimbaji hao wamedai kuwa nia
ya kujenga ukuta isiwe kuwakandamiza wachimbaji wadogo ila kuhakikisha
rasilimali hiyo inanufaisha Taifa.
Katibu wa chama
cha madalali wa madini mkoa wa Manyara, Mohamed Mughanja alisema ukuta huo
usibadili utaratibu uliozoeleka wa madalali na wachimbaji wadogo kukutana
migodini kwani wanategemeana.
Mughanja alisema
kwa miaka mingi wananchi wa mji mdogo wa Mirerani, wachimbaji wadogo wa madini
hayo na madalali waliishi kwa kutegemeana hivyo ukuta huo usije kuwatenganisha.
Alisema wadau
wote wanaouzunguka ukuta huo wanatarajia kunufaika kama miaka iliyopita hivyo
wataendelea kutoa ushirikiano kama miaka iliyopita ikiwemo kulipa kodi ya
serikali.
Mchimbaji mdogo wa
madini ya Tanzanite Amos Andrew alisema ukuta huo unapaswa kuchochea maendeleo
ya wachimbaji hao na siyo kuwadhoofisha.
Andrew alisema
wachimbaji wa madini wanatambua kuwa ukuta huo una lengo la kudhibiti
utoroshwaji wa madini ya Tanzanite hivyo hawaipingi serikali ila nao wanapaswa
kusikilizwa.
Alisema pamoja na
hayo, alitarajia kungekuwa na lango lingine kwenye eneo la Kilimanjaro mine ili
wenye migodi ya pembezoni waweze kuingia kwa urahisi tofauti na sasa kwani
ukuta huo una lango moja pekee.
Mwenyekiti wa
chama cha wachimbaji wa madini Mkoani Manyara (Marema) Sadiki Mneney alisema
wachimbaji madini wanapaswa kupewa ushirikiano wa kutosha juu ya ukuta huo.
Mneney alisema
wachimbaji wadogo wameshatambua umuhimu wa kulipa kodi kwani walishakaa kikao
na viongozi wa serikali na kuazimia kufungua ukurasa mpya na kuachana na yote
yaliyopita.
No comments:
Post a Comment