Mkazi wa kata ya Daudi Wilayani Mbulu Mkoani
Manyara, Aloyce Bura amesema alifurahi na kuchinja nguruwe mara baada ya kusikia
kwenye vyombo vya habari kuwa Rais John Magufuli amemteua Alexander Mnyeti kuwa
mkuu wa Mkoa huo, kwani wananchi wanyonge hivi sasa watakuwa wamepata mtetezi
wao.
Bura aliyasema hayo mbele ya Mnyeti, wakati
akizungumzia kero yake ya kunyang'anywa ardhi yenye makaburi ya familia yake na
kigogo wa eneo hilo kwa ushirikiano na ofisa ardhi.
Alisema miezi mitatu iliyopita aliposikia
kwenye vyombo vya habari kuwa Mnyeti ameteuliwa na Rais Magufuli kuwa mkuu wa
mkoa huo, alichinja nguruwe na kusherehekea na ndugu zake.
Alisema alichinja nguruwe huyo na kusherehekea
na familia yake kwani aliamini wanyonge watapata msaada kama alivyowasaidia
wananchi wa Arumeru, wakati akiwa mkuu wa wilaya hiyo.
"Mimi nimekaa Arumeru kwa muda mfupi
nimesikia sifa za Mnyeti kutetea wanyonge akiwemo kijana aitwaye Nyangusi wa
Ngaramtoni alidhulumiwa ardhi lakini alisaidiwa na Mnyeti na kurudishiwa eneo
lake," alisema Bura.
Alimuomba Mnyeti amsaidie arudishwe eneo lake
ambalo lina makaburi ya babu na bibi yake lakini likaporwa na mtu mwenye fedha
ambaye alisaidiwa na mmoja kati ya maofisa ardhi wa wilaya hiyo.
"Nimefuatilia suala hili kwa muda mrefu
hadi ofisi ya ardhi ngazi ya kanda kule Moshi lakini sijapata msaada, tunaomba
mheshimiwa mkuu wa mkoa tusaidie kama ulivyowasaidia watu wa Arumeru,"
alisema Bura.
Alisema rushwa imetumika kumuondoa kwenye eneo
hilo na yeye kunyimwa haki yake ila kutokana na utendaji kazi mzuri wa Mnyeti,
ana matarajio makubwa ya kupatiwa ardhi yake na kuendelea kuimiliki upya.
“Haihitaji hata elimu ya shahada kujua kuwa
sisi ndiyo tunamiliki eneo hilo kwani hata mtu wa darasa la saba atatambua hilo
kwani kuna makaburi ya babu na bibi yetu, tunaomba mkuu wa mkoa utusaidie hilo
sisi wanyonge,” alisema Bura.
Hata hivyo, Mnyeti alimuagiza mkuu wa kitengo
cha sheria wa ofisi yake Peter Mangala kupitia nyaraka za Bura ili kama
zinaonyesha ndiye mmiliki halali wa eneo hilo apatiwe haki yake.
"Mpe mwanasheria wangu nakala ya hizo
nyaraka zako ili azipitie na kuzifanyia kazi na ninakuhakikishia kama haki ni
yako utarudishiwa eneo lako bila mashaka wala wasiwasi wowote," alisema
Mnyeti.
Aliwataka watumishi wa idara ya ardhi kwenye
halmashauri za mkoa huo kufanya kazi zao kwa haki, weledi na hofu ya Mungu
kwani kwenye maeneo mengi wananchi wanawalalamikia kuwa wenyewe ndiyo
wanaosababaisha migogoro ya ardhi.
"Ninyi maofisa ardhi ndiyo mnasababisha
wananchi waichukie serikali yao kwani mnachukua virushwa na kupindisha haki
sasa mimi nitapambana nanyi nione mwisho wenu kwani mnasemwa sana,"
alisema Mnyeti.
Wanawake vikongwe wajasiriamali wa Kata ya
Uhuru Mjini Mbulu, wakiwa wamepiga magoti mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara,
Alexander Mnyeti, wakimuomba awasaidie wapate ardhi yao walioporwa na mfanyabiashara
wa mjini hapo.
Mkazi
wa Kata ya Daudi Wilayani Mbulu, Aloyce Bura akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa
wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, juu ya ardhi yake yenye makaburi
iliyoporwa na mfanyabiashara wa eneo hilo ambapo miezi mitatu iliyopita aliamua
kuchinja nguruwe akifurahia uteuzi wa Rais John Magufuli alioufanya kwa Mnyeti
ili awatetee wananchi wa mkoa huo.
No comments:
Post a Comment