Wanachama wa
Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Wilaya ya
Simanjiro Mkoani Manyara, katika kusherehekea miaka 41 ya kuzaliwa CCM, wametoa
msaada wa vyakula kwenye kituo cha kulea watoto yatima cha Light in Africa cha
Mji mdogo wa Mirerani na kupanda miti 20 kwenye taasisi za jamii.
Mwenyekiti wa UWT
Wilayani Simanjiro, Naitapwaki Lemeya Tukai, akiongoza zoezi hilo kwa
wanawake wa Kata za Endiamtu, Naisinyai na Mirerani, alisema jamii inapaswa
kuwajali yatima na wanyonge.
Tukai alisema
watanzania ni jamii ya watu wanaopendana hivyo, watoto hao wanapaswa kuangaliwa
kwa hali na mali ili wasihisi upweke wa kuwakosa wazazi wanapaswa kuangaliwa
kwa jicho la tatu kwani hao ni wanyonge.
Alisema ili
kuwajali wanyonge kuanzia mwezi ujao wa Machi, yeye binafsi anajitolea sh50,000
kwa ajili ya kuongeza mishahara ya wafanyakazi watatu wa kituo hicho
wanaowahudumia watoto hao.
Mlezi wa watoto
hao wa kituo cha New Light, Eliese Munuo amewashukuru wanawake hao waliojitolea
msaada huo kwa manufaa ya watoto hao wanyonge na yatima.
Munuo alisema
kituo hicho cha Light in Africa kilichopo Mirerani, kinahudumia watoto wanyonge
na yatima 69 wakiwemo wavulana 25 na wasichana 44.
Mjumbe wa Mkutano
mkuu wa UWT ngazi ya Taifa, Jackline Momo alisema kila mmoja kwa nafasi yake
binafsi anapaswa kutoa msaada kwa wahitaji hasa watoto yatima na wanyonge.
Momo alisema
inampasa kila mmoja kwa wakati wake kurudi mwenyewe na kuangalia namna ya
kuwasaidia watoto hao wanyonge, kwani nao wanahitaji upendo na misaada mingine
kama watoto wenye kulelewa na baba na mama.
Katibu wa UWT
wilaya ya Simanjiro, Zariha Mwinyi alisema wamepanda miti 10 kata ya Mirerani
na miti 10 kwenye kata ya Endiamtu na kutoa zawadi ya mchele, unga, sabuni,
sukari, mayai na juisi, kwa wanyonge kwenye kituo cha Light in Africa.
Mwinyi alisema pia
katika maadhimisho hayo wamepokea wanachama wapya 40 wa CCM, wengi wao wakiwa
wanafunzi wa shule za sekondari na wajasiriamali.
Diwani wa Tarafa
ya Moipo, Paulina Makeseni alipongeza maadhimisho hayo kwa wanawake wa UWT wa
kata tatu za Naisinyai, Mirerani na Endiamtu, kushiriki pamoja kwa nguvu moja
kwa kutembelea yatima na wanyonge.
"Tunashukuru
kupitia ngazi ya wilaya, tarafa na kata tumeshiriki pamoja maadhimisho haya,
tunaiomba serikali iwape misaada watoto yatima na wanyonge, kupitia elimu na matibabu,"
alisema Makeseni.
No comments:
Post a Comment