Monday 26 February 2018

WATUMISHI WA UMMA MSINYANYASE WACHIMBAJI WADOGO – BITEKO

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (mwenye kipaza sauti) akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu kwenye machimbo ya Kitunda ya Wilayani Sikonge, Mkoani Tabora. Biteko alifanya ziara kwenye machimbo hayo ili kujionea shughuli zinazoendelea sambamba na kuzungumza na wachimbaji.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Peres Magiri wakiwa kwenye mkutano na wachimbaji wadogo wa machimbo ya dhahabu ya Kitunda yaliyopo Wilayani Sikonge, Mkoani Katavi.
Wachimbaji wadogo wa dhahabu kwenye machimbo ya Kitunda wilayani Sikonge wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) alipofika kwenye machimbo hayo ili kujionea shughuli wanazofanya pamona na kujadiliana nao masuala mbalimbali ikiwemo ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali za Serikali.
Baadhi ya Wachimbaji wadogo wa dhahabu kwenye machimbo ya Kitunda wilayani Sikonge wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) alipofika kwenye machimbo hayo ili kujionea shughuli wanazofanya pamona na kujadiliana nao masuala mbalimbali ikiwemo ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali za Serikali.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) akiwasilikiza baadhi ya Wachimbaji wadogo wa dhahabu kwenye machimbo ya Kitunda wilayani Sikonge wakiuliza maswali na kuelezea changamoto mbalimbali ziazowakabili kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (mwenye kipaza sauti) akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu kwenye machimbo ya Kitunda ya Wilayani Sikonge, Mkoani Tabora. Biteko alifanya ziara kwenye machimbo hayo ili kujionea shughuli zinazoendelea sambamba na kuzungumza na wachimbaji.

……………….

Serikali imesema itawachukulia hatua za kinidhamu watendaji wanaotumia madaraka yao vibaya kwa kuwanyanyasa wachimbaji wadogo wa madini nchini ili kujipatia kipato kinyume na taratibu.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko kwenye mkutano na wachimbaji wadogo wa madini katika machimbo ya Dhahabu ya Kitunda yaliyopo Wilayani Sikonge, Mkoani Tabora.

Wakielezea changamoto zinazowakabili, wachimbaji wa machimbo hayo kwa nyakati tofauti walimueleza Biteko masikitiko yao juu ya unanyasaji wanayofanyiwa na baadhi ya Maafisa wa Serikali wasiowaaminifu wakiwemo Askari Polisi na Maafisa Madini.

Wachimbaji hao walisema kumekuwepo na tabia ya kushinikizwa kutoa rushwa ama kugawana faida kwa vitisho kuwa watazuiwa kuendelea kufanya shughuli zao kwenye maeneo husika.

“Kuna baadhi ya Maafisa Madini na Askari Polisi wamekuwa wakitulazimisha nao tuwape mgawo wa mawe tunayochimba vinginevyo watafukia maduara yetu,” alisema Alfred Kulwa mmoja wa wachimbaji kwenye machimbo hayo.

Kufuatia malalamiko hayo, Naibu Waziri Biteko alitoa onyo kwa watendaji wenye tabia hiyo kuacha mara moja na alimuagiza Afisa Madini kushirikiana na Mkuu wa Polisi wa Wilaya husika kuhakikisha wanafuatilia suala hilo na watakaobainika hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

“OCD, tendeni haki, hawa wawe salama. Askari atakayebainika ananyanyasa mchimbaji madini achukuliwe hatua za kinidhamu haraka bila kuchelewa,” aliagiza Naibu Waziri Biteko.

Biteko alisema Afisa yeyote anayehitaji kujishughulisha na biashara ya madini aache kazi ili ajikite katika biashara hiyo na sio kutumia cheo chake kuwanyanyasa wachimbaji.

Aliongeza kuwa hairuhusiwi Mtumishi wa Umma kutumia cheo kujinufaisha. “Marufuku watendaji wa Serikali ama wamiliki wa leseni za uchimbaji madini kutumia madaraka yao vibaya. Kama unataka ingia uchimbe mwenyewe. Serikali hii ya Awamu ya Tano inatutaka tuondoe manyanyaso,” alisema Biteko.

Biteko alisema mchimbaji atakayenyanyaswa atoe taarifa Polisi na pia amfahamishe kwa njia ya simu kuhusiana na manyanyaso hayo ambapo alitaja namba zake za simu ili kukitokea hali ya sintofahamu wasisite kumfahamisha.

Hata hivyo, Biteko aliwataka wachimbaji hao kuacha kuwasilisha taarifa za uwongo ikiwemo kusingiziana na mara zote wasimamie haki ili kuepusha migogoro baina yao na Serikali.

No comments:

Post a Comment