Wednesday, 21 February 2018

KITETO WAPITISHA BAJETI YA SHILINGI BILIONI 33.432

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, Lairumbe Mollel akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la madiwani waliopitisha mpango wa bajeti ya shilingi bilioni 33.432 kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, Tamim Kambona akisoma mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2018/2019 ambapo madiwani wa Halmashauri hiyo walipitisha kiasi cha shilingi bilioni 33.432. 
Diwani wa kata ya Sunya Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, Mussa Brython akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, Tamim Kambona akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo, ambapo alisema amepatiwa rasmi barua ya kuthibitishwa kazini baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo. 
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, wakiwa kwenye kikao cha Baraza la madiwani ambapo walipitisha kiasi cha shilingi bilioni 33.432 za mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2018/2019. 

Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, limepitisha mpango wa bajeti ya shilingi bilioni 33.432 kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Tamim Kambona akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani alisema bajeti hiyo imelenga kufanikisha mambo mbalimbali ikiwemo miradi ya maendeleo. 

Kambona alisema wamelenga kuboresha mapato ya ndani kwa kutumia mfumo wa kielektroniki na kukamilisha miradi viporo ili kuweza kutoa huduma iliyokusudiwa. 

Alisema wametenga asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya utoaji mikopo ya maendeleo ya vijana asilimia 4, wanawake asilimia 4 na watu wenye ulemavu asilimia 2.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Lairumbe Mollel alisema vipaumbele vya bajeti hiyo ni pamoja na kuwezesha uanzishwaji wa viwanda vipya vidogo na vya kati 15, kuongeza utoaji wa elimu bila malipo na kuongeza upatikanaji wa maji. 

Mollel alisema wamelenga kufanya mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa vijiji 41 vilivyosalia na kusimamia amani, utulivu, ili kuweka mazingira mazuri kwa wadau wa maendeleo na ufanisi. 

Diwani wa kata ya Sunya Mussa Brython (CCM) alisema kwenye bajeti hiyo kata yake imepangiwa fedha kwenye miradi ya afya elimu na maji. 

Brython alisema mradi wa maji umetengewa shilingi milioni 100 mradi wa zahanati utapatiwa shilingi milioni 400 na bweni la shule ya sekondari Sunya litamaliziwa kupitia mpango wa bajeti hiyo. 

Diwani wa kata ya Makame, Yakobo Niini (Chadema) alisema mpango wa bajeti hiyo umenufaisha uboreshaji wa upande wa sekta ya elimu kupitia shule ya sekondari ya kata hiyo. 

"Kata yangu inatatizo kwa upande wa miundombinu ya barabara kwani ni mibovu mno hakuna mawasiliano kabisa, naomba Tarura waliangalie hili," alisema Niini. 

Diwani wa kata ya Kaloleni, Christopher Parmet (CCM) alisema mara nyingi bajeti inapitishwa na madiwani lakini serikali kuu haifikishi fedha hizo kwa wakati hivyo kukwamisha miradi ya maendeleo. 

"Huku vijijini wananchi wanataka maji, shule na zahanati, ukiwaambia mmejikita kwenye mambo ya ununuzi wa ndege za Bombardier, reli na barabara za juu hawatakuelewa kabisa," alisema Parmet. 

Alisema serikali inapaswa kutambua kuwa bado mwaka mmoja wa kutekeleza ahadi ili mwaka unaofuata uchaguzi ufanyike na hivi sasa wananchi wa vijijini ni wajanja wanataka maendeleo siyo maneno. 

No comments:

Post a Comment