Friday, 2 February 2018

HALMASHAURI YA MJI WA MBULU YAPITISHA BAJETI YA SHILINGI BILIONI 16



Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu Mkoani Manyara, limepitisha bajeti ya shilingi 16, 225,661,581 kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019. 




Mkurugenzi wa Mji wa Mbulu, Anna Mbogo akizungumza wakati wa kupitishwa kwa bajeti hiyo amesema fedha hizo zitatumika kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Halmashauri hiyo na miradi ya maendeleo.

Mbogo amesema bajeti hiyo imelenga kuwezesha miradi ya elimu, afya na maji kwenye baadhi ya kata za Halmashauri ya Mji huo. 

Alisema bajeti hiyo haijahusisha fedha za ujenzi wa barabara kwani zimehamishiwa serikali kuu kupitia wakala wa barabara wa mjini na vijijini (Tarura). 





Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Valerian Gidshanga alisema kupitishwa kwa bajeti hiyo ni jambo moja na utekelezaji wake ni mwingine hivyo kila mmoja atimize wajibu wake. 

"Sisi madiwani kwa pande wetu tutekeleze wajibu wetu, watumishi wa halmashauri nao wafanye kazi kwa nafasi yao na wananchi kwa ujumla watuunge mkono katika kufanikisha bajeti yetu," alisema Gidshanga. 



Diwani wa Kata ya Tsawi, Anthony Genda amesema bajeti hiyo imejikita kwenye sekta tofauti za miradi ya maendeleo. 

Genda amesema kwa upande wa kata yake bajeti hiyo imezingatia suala la ujenzi wa kituo cha afya hivyo kuwa na manufaa kwa jamii. 

No comments:

Post a Comment