Diwani
wa Kata ya Hayderer Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, Justin Masuja (Chadema)
ambaye amejiuzulu nafasi hiyo, kwa kujitoa kwenye chama hicho na kujiunga na
CCM amesema hajanunuliwa ili kuondoka kwenye chama hicho.
Masuja ambaye ni diwani wa pili wa Chadema
Mkoani Manyara, kujiuzulu kwenye kipindi cha wiki moja, baada ya diwani wa kata
ya Bagara Mjini Babati, Nicodemus Tlaghasi kujiuzulu, amesema ameondoka Chadema
kwa utashi wake mwenyewe.
Alisema hata alipokuwa Chadema aliingia kwenye
chama hicho kwa hiyari na utashi wake, hivyo hata CCM amejiunga nayo kwa ridhaa
yake.
"Wakati najiunga na Chadema nilikuja kwa
ridhaa yangu hivyo hata kuhamia CCM nimefanya hivyo mwenyewe kwa haiba na
utashi wangu," alisema Masuja.
Alisema anapenda kuunga mkono harakati za Rais
John Magufuli la kupambana na upigaji, rushwa na kuwatumikia wananchi hasa
wanyonge ndiyo sababu akajiunga na CCM.
Alisema akiwa Chadema hakuna mtu aliyempeleka
hivyo amemtumia haki yake ya msingi kujiunga na CCM hivyo amehamia huko ili
kufanikisha maendeleo ya wananchi wa eneo hilo.
"Nawaomba CCM wanipokee kwa moyo mmoja
kwani nilikuwa natekeleza ilani ya CCM nikiwa Chadema hivyo nimekuja kwenye
chama hicho tukawatumikie wananchi ipasavyo," alisema Masuja.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
ya Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga alithibitisha kupokea nakala ya barua ya
kujiuzulu kwa diwani huyo.
Kamoga alisema yeye kama msimamizi wa uchaguzi
wa wilaya hiyo, atakijulisha chama alichotoka diwani huyo kuwa kata hiyo ipo
wazi kwa sasa.
Alisema pia wataiandikia barua tume ya Taifa
ya uchaguzi ili mchakato wa uchaguzi mdogo wa udiwani kwenye kata hiyo uanze
mara moja.
No comments:
Post a Comment