Mkuu wa Mkoa wa
Manyara, Alexander Mnyeti amewataka watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Mbulu, ambao hawaungi mkono Serikali inayoongozwa na CCM kuachia nafasi zao
kwani atawachukulia hatua kali kwa kutotimiza wajibu wao ipasavyo kwa kufanya
kazi kizembe na kuingiza siasa chafu kazini.
Kutokana na hali
hiyo alimuagiza kaimu katibu Tawala wa mkoa huo Arnold Msuya kumsimamisha kazi
ofisa Tarafa ya Dongobesh Bayo Banka hadi hapo atakapotoa maelezo ya kushindwa
kutimiza wajibu wake kwa kuchanganya siasa na kazi.
Mnyeti alitoa
agizo hilo wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya
Mbulu kwenye ziara yake ya siku saba.
Alisema CCM
ilifanyika kampeni na kuinadi ilani yake kwa wananchi na kushinda uchaguzi
kisha wakawakabidhi watumishi wawatumikie wananchi huku wakipewa mishahara na
posho lakini wanashindwa kutekeleza kwa vitendo.
"Mnakaa
ofisini na kulipwa mishahara na posho nyingi lakini mnashindwa kuwatumikia
wananchi badala yake mnaingiza siasa chafu, natoa onyo kwa wote wasirudie jambo
hilo hata mara moja nitawachukulia hatua kali," alisema Mnyeti.
Mnyeti alisema
anayo majina na taarifa za baadhi ya watumishi wanafanya kazi kilegelege na
kuzorotesha shughuli za serikali kwa kuingiza siasa kwenye kazi zao na
kumkabidhi Msuya majina hayo.
"Pamoja na
ofisa tarafa huyo pia nakukabidhi majina mengine ya watumishi ambao
wanatekeleza maagizo ya viongozi wa vyama vingine vya kisasa badala ya
kutekeleza maagizo ya viongozi wa serikali inayoongozwa na CCM," alisema
Mnyeti.
Akisoma taarifa
ya Wilaya ya Mbulu, Mkuu wa Wilaya hiyo Chelestino Mofuga alisema wilaya hiyo
yenye halmashauri mbili ni miongoni mwa wilaya tano za mkoa huo.
Mofuga alisema
wananchi wa eneo hilo ni wafugaji na wakulima, wenye kufanya shughuli zao
katika maeneo tofauti kupitia halmashauri mbili za wilaya zilizopo Mbulu.
Alisema wilaya
hiyo ina migogoro mbalimbali ya mipaka ikiwemo na Wilaya jirani za Hanang'
Babati, Karatu Mkoani Arusha na Mkalama Mkoani Singida.
Alisema
wamefanikiwa kutatua migogoro mingi ya ardhi wilayani humo kwani kila siku ya
alhamisi akishirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na baadhi ya
wakuu wa idara hukutana na wananchi wenye matatizo mbalimbali.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga alisema watumishi wa
Halmashauri hiyo wamejipanga kuhakikisha wanawatumikia wananchi ipasavyo.
Kamoga alisema
watumishi wa Halmashauri hiyo wapo tayari kutekeleza maagizo, maelekezo na
ushauri katika kuwatumikia wananchi.
No comments:
Post a Comment