Thursday, 16 February 2012

STORY MANYARA


MWANAMKE NA MWANAUME WAKAMATWA NA KETE 100 ZINAZODAIWA NI DAWA ZA KULEVYA.

WATU wawili wakazi wa mtaa wa Zaire,mji mdogo wa Mirerani,Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani humo wakidaiwa kukutwa na kete 100 za dawa za kulevya aina ya cocaine.

Wafanyabiashara hao ambao ni mwanamke na mwanaume walikamatwa na mkuu wa kituo cha polisi Mirerani,Elisha Saenda,msaidizi wake Wenceslaus Gumha na makachero Athuman Bakary,Julius Makasi na Naendwa Mnzava.

Imeelezwa kwamba,wafanyabiashara hao wanadaiwa kuwa wanaendesha biashara hiyo ya kuuza dawa za kulevya baada ya kuletewa dawa hizo na mfanyabiashara maarufu wa mjini Arusha.

Kamanda wa polisi mkoani Manyara,Kamishna msaidizi Liberatus Sabas alithibitisha kukamatwa kwa wafanyabiashara hao wawili na kutaja majina yao kuwa na Jenny Heri (30) Bakari Omary (35) wote wakazi wa wilaya  hiyo.

Kamanda Sabas alisema tukio hilo lilitokea Februari 14 saa 3:20 usiku katika kitongoji cha Kazamoyo mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro baada ya askari polisi kuendesha msako wa kutafuta dawa za kulevya.

Alisema askari hao baada ya kupata taarifa ya kufanyika kwa biashara hiyo walifika na kufanya upekuzi kwenye eneo linalotumiwa na wafanyabiashara hao na kukuta kete hizo 100 za dawa za kulevya. 

“Kete hizo 100 zinazodaiwa kuwa ni dawa za kulevya zitapelekwa kwa mkemia wa Serikali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wake ambaya ndiye ataelezea vizuri kupitia taarifa yake atakayoleta kwetu,” alisema Kamanda Sabas.

Alisema Jeshi lake bado linawashikilia watuhumiwa hao na wanaendelea na uchunguzi wa tukio kabla ya kuwafikisha mahakamani kusomewa shtaka baada ya uchunguzi wa tukio hilo kukamilika.

MWISHO.

MFANYABIASHARA WA MADINI YA TANZANITE MIRERANI AJINYONGA KWA KUDAIWA DENI LA SHILINGI LAKI NANE.

MFANYABIASHARA wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro mkoani Manyara,amefariki dunia kwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya viatu vyake akiwa chumbani kwake kwa kinachodaiwa deni la sh800,000. 

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi mkoani Manyara,Kamishna msaidizi Liberatus Sabas mtu huyo ametambulika kwa jina la Thobias John (35) mkazi wa kitongoji cha Songambele mji mdogo wa Mirerani.

Kamanda Sabas alisema tukio hilo lilitokea Februari 13 mwaka huu saa 9 alasiria kwenye chumba alichokuwa amepangisha John ambapo askari polisi walipewa taarifa baada ya watoto wa nyumba ya jirani kuona dirishani mtu ananing’ia chumbani kwake. 

Hata hivyo,alisema chanzo cha kifo hicho hakijajulikana mara moja na jeshi lake linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo huku mwili wa marehemu huyo ukihifadhiwa kwenye hospitali ya rufaa ya KCMC ya mjini Moshi kwa uchunguzi.

Uchunguzi uliofanywa na www.mireranitanzanite.blogspot.com umebaini kuwa John alijinyonga kwa kutumia kamba za viatu kutokana na deni la sh800,000 alilokuwa anadaiwa baada ya kukopeshwa na mfanyabiashara mmoja wa madini ya Tanzanite.

Inadaiwa kuwa John ambaye alikuwa mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite alikopa deni hilo kwa lengo la kununua madini hayo na kuyauza ili alipe fedha hizo ambazo zilikuwa mtaji wa kununua lakini alishindwa kuzirejesha.

“Siku ya tukio hilo alimwagiza mke wake aondoke na watoto wake wawili waende kwa ndugu yake ndipo yeye akachukua kamba za viatu hivyo na kujinyonga kwenye chumba chao,” alisema mmoja kati ya ndugu yake.

Alidai kuwa taratibu za mazishi zinaendelea kwa ajili ya kuusafirisha mwili wa marehemu huo uliopo KCMC hivi sasa kwenda wilayani Rorya mkoani Mara ambapo ndipo nyumbani kwa marehemu huyo.

MWISHO.
 
APONEA CHUPUCHUPU KUFARIKI DUNIA KWA KUJINYONGA NA BAADA YA KAMBA KUKATIKA ATOKA BERENGE

MKAZI wa Kata ya Endiamtu mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro mkoani Manyara ameponea chupuchupu kufariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani lakini kamba hiyo ikakatika kabla ya kifo chake.

Wakizungumza na www.mireranitanzaniteblogspot.com baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa baada ya kutaka kujiua kwa kutumia kamba na baadaye kamba hiyo ya katani kukatika mtu huyo alitoroka kwa kukimbilia sehemu isiyofahamika.

Mashuhuda hao walidai kuwa tukio hilo lilitokea Februari 13 mwaka huu saa 4:30 asubuhi kwenye mtaa wa Endiamtu ambapo mtu huyo ambaye ni mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite alitaka kujiua kwa kujinyonga bila kujulikana sababu ya kujinyonga kwake.

Walidai kuwa baada ya mtu huyo kujifunga shingoni na kitanzi cha kamba ya katani alipanda kwenye stuli na kuiangusha ambapo alianza kuning’inia hewani chumbani kwake anapoishi lakini kabla hajafa kamba hiyo ikakatika yenyewe.

Walisema mtu huyo ambaye jina lake tunalihifadhi hakuamini macho yake kama ameponea chupuchupu kufa baada ya kamba hiyo kukatika na kumjeruhi shigoni kwake kisha akatimua mbio mithili ya mwanariadha wa Marathon.

“Hatuelewi kilichomsaidia asife ni nini,labla ni ubovu wa kamba ndiyo umesababisha kwani hakuamini macho yake kama amepona kifo na akatimua mbio hadi  hivi sasa hajulikani mahali alipo,” alisema mmoja kati ya shuhuda.

Hata hivyo,Kamanda wa polisi mkoani Manyara,Kamishna msaidizi Liberatus Sabas alipoulizwa juu ya tukio hilo alisema kuwa jeshi lake bado halijapata taarifa zozote za kutaka kujiua kwa kujinyonga kwa mtu huyo.

Mtu huyo anafikisha idadi ya watu watatu wenyeji wa mkoa wa Mara wanaoishi mji mdogo wa Mirerani waliojinyonga mwanzoni mwa mwezi huu ambapo kati yao watu wawili walifariki dunia baada ya kujinyonga huko. 

MWISHO.

WACHIMBAJI WA GREAN TOMARINE WAFIA MGODINI KWA KUFUKIWA NA NGEMA 

WACHIMBAJI wawili wadogo wa madini ya Tomarini ya kijani wa kijiji cha Riroda wilayani Babati mkoani Manyara wamefariki dunia na wengine watatu wamejeruhiwa vibaya baada ya kufukiwa na kifusi wakiwa mgodini.

Wakizungumza na www.mireranitanzanite.blogspot.com kwenye eneo la mgodi huo,baadhi ya wachimbaji wadogo walioshuhudia tukio hilo walidai kuwa chanzo cha kifo hicho ni wachimbaji hao kuangukiwa na kifusi baada ya kutochimba kitaalamu.

Mmoja kati ya wachimbaji hao Farouq Suleimani alisema tukio hilo lilitokea juzi asubuhi wakati wachimbaji hao wakiendelea na kazi ya kuchimba udongo wa madini mgodini hapo ili wapate madini hayo.

Suleimani alisema wachimbaji hao walikuwa wanachimba mgodi huo ambao udongo wake ni mwepesi bila kuchukua tahadhari ndipo wakati wakiendelea na kazi hiyo udongo huo ukawaangukia ndani ya mgodi wakati wakifanya kazi zao.

Aliwataja wachimbaji hao waliofariki dunia kuwa ni Nada Eddy (20) na Soghore Sandi (38) na majeruhi ni Isaka Mayo (24) Daudi Darabe (35) na Dorobo Harweri (30) wote wakazi wa kijiji hicho cha Riroda.

“Miili hiyo imeshaondolewa kwenye mgodi huo na imehifadhiwa kwenye chumba cha maiti cha hospitali ya mji wa Babati - Mrara na majeruhi hao wanaendelea kupatiwa matibabu kwenye hospitali hiyo,” alisema Suleimani.

Akizungumza na www.mireraniblogspot.com baada ya kutokea vifo hivyo,Diwani wa kata ya Riroda,Yohana Baraye alisema atakutana na wachimbaji hao wadogo wa madini ili kupanga namna nzuri ya kuchimba madini hayo kwa usalama zaidi.

Baraye alisema atashirikisha viongozi wa Serikali ili kusimamia taratibu,kanuni na sheria kwa wachimbaji hao wadogo ili kuepusha madhara zaidi yasitokee kwenye machimbo hayo kijiji hapo kama ilivyotokea kwa vifo hivyo.

Baadhi ya wachimbaji hao wadogo walidai kuwa tangu madini hayo yagundulike miezi sita iliyopita hakuna hatua sahihi na madhubuti zilizochukuliwa kwani wanachimba bila utaalamu hivyo kutishia hali ya usalama wao.

Walisema wachimbaji wazoefu wamekuwa wakiwaelekeza wachimbaji wasio na uzoefu lakini wamekuwa wabishi hivyo kusababisha matatizo kutokea kila mara na waliiomba Serikali kuwashirikisha ili ajali zakuepukika zisitokee tena.

Hata hivyo,Kamanda wa polisi mkoani Manyara,Kamishna Msaidizi Liberatus Materu Sabas alithibitisha kutokea kwa vifo hivyo na kudai kuwa yupo safarini hivyo hawezi kuzungumzia tukio hilo kwa undani zaidi.

MWISHO.

MAMEC YAPATA VIONGOZI

WANACHAMA wa klabu ya waandishi wa habari wa mkoa wa Manyara (MAMEC) wamemchagua mwakilishi wa Shirika la utangazaji nchini TBC mkoani humo,Benny Mwaipaja kuwa Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari wa mkoa wa Manyara (MAMEC).

Katika uchaguzi huo uliofanyika Februari 12 mjini Babati na kusimamiwa na Zilipa Joseph,Makamu wa Rais wa Muungano wa klabu za waandishi wa habari nchini (UTPC),Mwaipaja aliyekosa mpinzani alipata kura 12 kati ya kura 15 zilizopigwa.

Akitangaza matokeo hayo,Makamu huyo wa Rais wa UTPC alisema mwandishi wa gazeti la Majira,Mary Margwe alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Mamec,baada ya kupata kura zote 15 za waandishi wote mkoani humo.

Alisema mwakilishi wa Star Tv na Radio Free Africa mkoani Manyara,Zacharia Mtigandi alichaguliwa kuwa Katibu Mtendaji kwa kura 12 dhidi ya kura tatu za Charles Masayanyika mwandishi wa ITV na Radio One,kampuni ya IPP.

Alisema kuwa Fortunatha Ringo mwandishi wa gazeti la Kiongozi alichaguliwa kuwa Katibu msaidizi wa Mamec,kwa kupata kura tisa dhidi ya Tabia Daffo wa Radio uhuru aliyepata kura tano huku kura moja ikiharibika.

Zilipa alisema Julieth Peter mwandishi wa habari wa gazeti la Jambo Leo alichaguliwa kuwa Mtunza hazina kwa kupata kura 14 baada ya kukosa mpinzani kwenye nafasi hiyo huku kura moja ikimkataa.

Alisema mwandishi wa gazeti la Majira,Mohamed Hamad,ambaye pia hakuwa na mpinzani kwenye nafasi yake,alichaguliwa kuwa Mweka hazina msaidizi kwa kupata kura 14 na ambaye nay kura moja ilimkataa.

Makamu huyo wa Rais aliwatangaza wajumbe wa Kamati tendaji na vyombo vyao kwenye mabano ni Joseph Lyimo (www.mireranitanzaniteblogspot.com) Grace Msovela (Ofisa habari Babati) Abraham Mlundi (kujitegemea) Hamida Khalid (Tanzania Daima) na Peter Ringi (Majira).

Akizungumza na www.mireranitanzanite.blogspot.com baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mamec,Mwaipaja alisema waandishi wa habari wa mkoa huo wanatakiwa kuongeza bidii katika utendaji wao wa kazi ili waweze kutoa huduma ya kuipasha habari jamii.

Alisema vyama vingi vya waandishi wa habari wa mikoa tofauti hapa nchini vinashindwa kuendelea kutokana na kuwa na migogoro mingi isiyo na tija hivyo aliwapongeza waandishi wa mkoa huo kwa kuwa na upendo,umoja na mshikamano.

MWISHO.

SERIKALI YAINGIA MKATABA NA HOSPITALI YA DAREDA MISSION

SERIKALI imetiliana saini na kuingia mkataba na hospitali ya Mission ya Dareda inayomilikiwa na Kanisa katoliki Jimbo la Mbulu,iliyopo Wilaya ya Babati mkoani Manyara kwa kuifanya kuwa hospitali Teule ya wilaya.

Kutokana na hospitali hiyo kuingia mkataba huo kutawezesha jamii inayozunguka eneo hilo kufaidika na huduma ya afya ambapo hivi sasa itakuwa inashirikiana na halmashauri ya wilaya ya Babati vijijini katika uendeshaji wake.

Akizungumza wakati wa kutia saini mkataba huo,Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo,Elly Jesse Mlaki alisema Serikali itakuwa inaipatia kila mwaka hospitali hiyo sh300 milioni ili iweze kujiendesha.

Mlaki alitoa wito kwa watumishi wa hospitali hiyo kuwajibika ipasavyo wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa kama walivyokubaliana wakati wa kutia saini mkataba huo wa ushirikiano baina ya Serikali na hospitali hiyo.

Alitaja miongoni mwa makubaliano hayo ni kutoa bure huduma za tiba kwa ajili ya kina mama wajawazito,wazee wasiojiweza na watoto wenye umri wa kuanzia miaka mitano hadi kushuka chini.

Hospitali Teule ya Dareda Mission ilianzishwa zaidi ya miaka 25 iliyopita na inatoa huduma zake kwa wakazi wa mkoa huo na baadhi ya wakazi wa sehemu ya mikoa ya Singida na Dodoma.

Hata hivyo,baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo wakizungumza na www.mireranitanzanite.blogspot.com wameipongeza Serikali kwa kitendo hicho cha kuifanya hospitali hiyo kuwa Teule ya wilaya kwani hali hiyo itasogeza huduma karibu nao.

 Walidai kuwa,baada ya hospitali hiyo ya Dareda kufanywa kuwa hospitali Teule ya wilaya kutafanya iboreshwe zaidi hivyo kuwawezesha wananchi hususani walio na kipato cha hali ya chini kufaidika na mpango huo.    

MWISHO.

WAANDISHI MANYARA WAASWA

WANACHAMA wa Chama cha waandishi wa habari wa mkoa wa Manyara (MAMEC) wametakiwa kuandika habari za uchunguzi ambazo zitaibua changamoto zinazowakabili wananchi wa vijijini.

Hayo yamesemwa na Mkutubi wa chuo kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) Peter Mataba kwenye mafunzo ya kuandika makala kwa wanachama wa Mamec,yaliyofanyika kwa muda wa siku tatu mjini Babati.

Mataba ambaye pia ni Mhariri wa gazeti la Kiongozi alisema waandishi wengi wanatabia ya kuandika habari za polisi kila wakati wakati habari nyingi za kuibua changamoto na mafanikio zipo vijijini.

Alisema kuwa waandishi wazuri wanaandika habari za vijijini kwani huko ndipo kwenye changamoto nyingi za kimaisha ikiwemo watu wengi kutotambua haki zao kuliko kung’ang’ania kuandika habari za mjini.

Alisema waandishi wakiendelea kuandika habari za mjini na kuacha za vijijini maendeleo yatakuwa ndoto kupatikana kwani hakutakuwa na kiongozi atakayefahamu kwa urahisi matatizo yanayowakabili wananchi.

“Mara nyingi viongozi wetu hupenda kutazama tv au kusoma magazeti na pindi wanapokutana na habari zilizoandikwa juu ya matatizo ya wananchi ndipo wanaanza kutatua changamoto hizo,” alisema Mataba.

Naye,Makamu wa Rais wa Muungano wa vilabu vya waandishi wa habari nchini (UTPC) Zilipa Joseph aliwataka waandishi hao watumie mafunzo hayo kwa ajili ya kuibua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa mkoa huo.

“Kupitia mafunzo haya mkoa wa Manyara utanufaika kwa waandishi wa habari kuutangazwa habari zake ili jamii nchini na hata nje ya nchi itambue sifa nyingi nzuri za mkoa huu ambao bado ni mchanga,” alisema Zilipa.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa MAMEC,Benny Mwaipaja aliwataka waandishi hao wa habari kujifunza kwa umakini zaidi wakati wa mafunzo hayo ya siku tatu ili kuandika habari nyingi za makala.

Mwaipaja alisema waandishi hao wanapaswa kutumia mafunzo hayo ipasavyo ili kuibua changamoto za jamii ya wafugaji na wakulima wa mkoa huo za kiuchumi,kiafya,kielimu na kiutamaduni pamoja na mafanikio yao. 

MWISHO

No comments:

Post a Comment